Msemaji wa wizara ya biashara ya China hivi karibuni amesema, China itaongeza misaada kwa nchi za Afrika hatua kwa hatua, wakati huo huo idara husika za China ziko mbioni kushughulikia upunguzaji wa madeni kwa baadhi ya nchi za Afrika. Baada ya kufungwa kwa mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, wizara ya biashara ya China imeanza kutekeleza hatua 8 za sera kwa Afrika zilizotolewa kwenye mkutano huo. Misaada iliyotolewa na serikali ya China kwa nchi zinazoendelea zikiwemo nchi za Afrika haina masharti, ni misaada ya dhati kati ya marafiki. Kutokana na kuendelezwa kwa uchumi nchini China, China itaongeza hatua kwa hatua msaada kwa nchi za Afrika ili kuzihimiza nchi za Afrika zijiendeleze kiuchumi na kijamii.
Kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, serikali ya China imeahidi kuongeza maradufu msaada kwa nchi za Afrika ifikapo mwaka 2009 kuliko ule wa mwaka 2006. Kuendelea kuzisaidia nchi za Afrika kujenga miradi ya miundo mbinu na ya huduma za umma kama vile majengo ya kiserikali, barabara, hospitali, majumba ya michezo na shule. Pia itatoa mafunzo ya elimu mbalimbali kwa watu elfu 15 wa Afrika ili kuzisaidia nchi za Afrika kuharakisha kuinua uwezo wao wa kujiendeleza na kupambana na maradhi.
Msemaji huyo alisema, China bado ni nchi inayoendelea, pia inakabiliwa na shinikizo kubwa la kupunguza umaskini na kujiendeleza, lakini China itaendelea kutoa misaada kwa nchi za Afrika kama ilivyofanya zamani. China itashirikiana na nchi za Afrika na kufanya majadiliano ya kirafiki na kutekeleza miradi mbalimbali.
Viongozi wa kibiashara kutoka barani Afrika wanazidi kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati yao na bara la Asia, hasa China. Kwa mujibu wa makala iliyochapishwa kwenye gazeti la kibiashara The Financial Standard, Uhusiano huo wa kiuchumi umetiliwa mkazo kutokana na mazungumzo yaliyofanywa kati ya wafanyabiashara mbalimbali kutoka bara la Afrika na wanakampuni wa China, wakati wafanyabiashara hao walipoitembelea China.
Nigeria ni moja kati ya nchi kadhaa za bara la Afrika zinazonufaika zaidi kutokana na uhusiano wa kibiashara kati yake na China. Wakati wa mkutano uliofanyika hivi karibuni wa wakuu wa nchi wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, ambao ulihudhuriwa na viongozi wa nchi 48 za Afrika na wenzao wa China, kampuni moja ya China ilitangaza kuwa itajenga njia ya reli yenye kuunganisha mji wa Kano na bandari ya Lagos, kwa gharama ya dola za kimarekani bilioni 8.3. Aidha katika mji huo wa Kano ambao una wakazi zaidi ya milioni 3.5, kwa sasa mji huo umejaa na mikahawa na maduka mengi ya kuuzia bidhaa za China.
Hali kadhalika mji huo unajivunia kuwa na kiwanda cha wachina cha kutengeneza viatu, ambacho kimewaajiri watu wapatao 2,000, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuliko kampuni nyingine yoyote binafsi, kaskazini mwa Nigeria. Mfanyibiashara mmoja katika mji huo Bw. Saidu Dattijo Adhama alipohojiwa alisema, "kampuni za China zina mashine nzuri na za kisasa, miundo mbinu mizuri ya nishati na hivyo uzalishaji wake ni madhubuti".
Wakati huo huo soko la mavazi la Kwari, ambalo ni soko kubwa kabisa kwenye sehemu ya Afrika magharibi, limepanuka zaidi kutokana na mavazi na bidhaa za aina mbalimbali za nguo kutoka China.
Mbali na hayo pia njia za uchukuzi nchini Nigeria zimeimarishwa sana, kwa kuwa sasa miji kadhaa ya Nigeria imeshamiri teksi za kutoka China. Na unafuu wa bei za teksi hizo mpya kutoka China, umezifanya teksi zilizokuwepo hapo kabla kutoka nchini nyingine kupungua, kwa kuwa teksi za Vespa kutoka Italia zilikuwa zikiuzwa mara tatu zaidi ikilinganishwa na bei ya teksi kutoka nchini China, punguzo hilo limewafanya watu wengi zaidi watumie teksi za China.
Naibu mkuu wa chama cha wafanyabiashara nchini Nigeria Bw. Ahmed Rabiu alisema, China imesaidia kwa kiwango kikubwa kufufua uchumi nchini humo.
Mfanyabiashara mwingine Bw. Ibrahim Garba mwenye umri wa miaka 50, alisema kuwa hali yake ya kibiashara imekuwa nzuri zaidi kutokana na ziara zake alizofanya nchini China, ambako sasa anaweza kuuza magari na vipuri vyake, na kupata faida ya asilimia 70 zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2006-12-22
|