Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-26 18:54:06    
Kilimo mkoani Hainan kimekuwa sekta inayowekezwa sana na wafanyabiashara kutoka Taiwan

cri

Mwaka 1999 mkoa wa Hainan ulioko kusini mwa China ulithibitishwa na serikali kuwa ni mkoa pekee wa majaribio ya ushirikiano katika sekta ya kilimo kati ya pande mbili za mlango bahari wa Taiwan. Tokea hapo uwekezaji wa wafanyabiashara wa Taiwan kwenye mkoa wa Hainan uliongezeka kwa haraka. Mwanzoni ilikuwa ni shughuli za ufugaji samaki, uzalishaji matunda, upandaji maua na miche ya miti pamoja na kupanda mboga za majira ya joto kwenye majira ya baridi hapo mwanzoni, na sasa imefikia hadi kuendeleza uzalishaji wa mazao kwenye bahari karibu na pwani na uzalishaji bidhaa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya uhandisi wa viumbe kwa hivi sasa..

Meneja mkuu wa kampuni ya maendeleo ya kilimo ya Jindefeng ya mkoani Hainan Bw. Huang Yifeng ni mcheshi na anapenda sana kuongea na watu. Kwenye shamba la kilimo lililoko kwenye kiunga cha mji wa Haikou, mji mkuu wa mkoa wa Hainan, Bw. Huang Yifeng alikuwa anaongea na mwandishi wetu wa habari huku mkononi akiwa na matunda maalumu ya kutoka Taiwan ya Lianwu, alisema

"Kuna wafanyabiashara wengi kutoka Taiwan waliowekeza katika sekta ya kilimo mjini Haikou, na pia kuna aina za matunda wanayolima huko, lakini matunda yaliyo mazuri zaidi ni aina ya 'Lianwu'."

Bw. Huang Yifeng alizaliwa katika wilaya ya Pingdong kisiwani Taiwan, na alikuwa anajishughulisha na kilimo cha matunda ya Lianwu huko Taiwan kabla ya kufika mkoani Hainan. Yeye alivutiwa na ardhi ya Hainan wakati alipofika huko kufanya uchunguzi mwaka 1998, na alipata wazo la kuanzisha shamba la matunda ya Lianwu huko Hainan. Mwaka 2001 aliona shamba moja lenye hekta 50 kwenye kiunga cha mji wa Haikou na alitaka kukodi shamba hilo. Bw. Huang Yifeng alisema,

"Serikali ya hapa inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, baada ya siku chache tu nikapata ardhi niliyoitaka, katika mwaka wa pili tulipanda miche elfu 20 na mwaka wa tatu tulianza kuvuna, mavuno yalifikia kilo zaidi ya laki 4. Sasa shamba letu limepanuka na kuwa zaidi ya hekta 80."

Bw. Huang Yifeng alisema, Lianwu ni tunda zuri sana, umbo lake linapendeza, tena lina vitamin nyingi za kujenga mwili, anaamini kuwa mji wa Haikou utakuwa kituo cha kwanza cha kuzalisha matunda ya ya Lianwu kwenye Asia. Hadi hivi sasa kuna zaidi ya aina 80 za aina kubwa zaidi ya 50 za mbegu na miche bora zilizopelekwa mkoani Hainan na wafanyabiashara kutoka Taiwan. Mfanyabiashara kutoka Taiwan Bw. Wu Jinmu na mkewe walifanikiwa kupeleka mbegu bora za mapapai ya Taiwan huko Hainan. Kwenye shamba la mipapai la Bw. Wu Jinmu hakuna majani yanayoota ovyo, ila tu mipapai mirefu iliyozaa mapapai mengi.

Kabla ya kufika Hinan, Bw. Wu Jinmu na mkewe walifungua duka moja la sonara la kuuza mapambo ya dhahabu ya wanawake kwenye mji wa Gaoxing, Taiwan. Mwaka 1999 waliacha biashara ya mapambo ya dhahabu na kwenda mkoa wa Hainan kushughulikia kilimo cha mapapai, jambo ambalo liliwashangaza sana jamaa na marafiki zao. Bw. Wu alimweleza mwandishi wetu wa habari kuhusu mpango wake,

"Wakati ule mapapai yalichukuliwa kama ni mboga mkoani Hainan, na bado hakukuwa na soko la mapapai kwenye soko la China bara, tulijaribu zaidi ya aina 20 za mbegu za mapapai tulizoleta kutoka Taiwan, hatimaye tuliona aina ya mbegu inayojulikana kama 'Risheng' inafaa sana kuota kisiwani Hainan, sasa soko la mapapai limeanzishwa na kuendelezwa katika soko la China bara, mapapai yanayozalishwa kwenye shamba la hekta mia kadhaa haliwezi kukidhi mahitaji ya watu. Sasa tunafikiria kuanzisha shirika la usafirishaji na uuzaji wa mapapai kwa kushirikisha wafanyabiashara wote pamoja na wakulima wenyeji wa Hainan wanaolima mapapai mkoani Hainan, bila shaka tutakuwa na maendeleo mazuri."

Pamoja na kuimarika kwa kilimo cha Hainan, shughuli zinazohusika na kilimo zinakuzwa hatua kwa hatua, hivi sasa wafanyabiashara kutoka Taiwan wanaona nafasi kubwa ya maendeleo.

Kampuni ya Quanxing ni moja ya kampuni maarufu na yenye nguvu kisiwani Taiwan, ambayo ilianzishwa miaka zaidi ya 30 iliyopita, na imeanzisha matawi zaidi ya 20 ya ufugaji na usindikaji wa mazao ya majini duniani. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, kampuni ya Quanxing ilijiendeleza na kujenga viwanda katika baadhi ya nchi za Asia ya kusini mashariki zikiwemo Indonesia, Thailand, Malaysia, Vietnam na Philippines. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zanazingatia usalama wa chakula cha majini, baada ya kufanya utafiti kampuni hiyo inaona kuwa Hainan ni sehemu nzuri yenye hewa na maji bora kwa uzalishaji na usindikaji wa chakula cha majini.

Mwezi Juni mwaka 2003, kampuni ya Quanxing ilianzisha kampuni ya chakula cha baharini ya Hainan kwenye eneo la ustawishaji uchumi la mji wa Haikou, ikishughulikia usindikaji wa chakula cha majini. Kiwanda cha usindikaji cha mitambo ya barafu chenye eneo la mita za mraba elfu 55, kilichojengwa kwa gharama ya Yuan milioni 60, pato la mwaka uliopita lilifikia dola za kimarekani milioni 10, na linatarajiwa kufikia dola za kimarekani milioni 30 mwaka 2006. Naibu meneja mkuu wa kampuni hiyo Bibi Yang Huayin alisema,

"Kampuni yetu imekuwa na pato kubwa, kama tunapata malighafi ya kutosha, tutakuwa na faida katika mwaka wa tatu."

Bibi Yang Huayin alizaliwa huko Gaoxing, Taiwan, alihitimu katika chuo cha mazao ya baharini cha mji wa Gaoxing, na alijishughulisha na uvuvi huko Taiwan. Mwaka 1998 kutokana na kufahamishwa na rafiki yake, alikwenda mjini Haikou kufanya uchunguzi kuhusu mazao ya baharini, hakutazamia kama angevutiwa sana na hali ya Haikou na kuwa mmoja wa wafanyabiashara waliotangulia kwenda Hainan kujishughulisha na uzalishaji wa mazao ya baharini. Bibi Yang alisema hivi sasa mazao ya baharini ya kampuni yake yanauzwa Marekani, Japan na nchi za Umoja wa Ulaya, na kuwa mazao muhimu ya Hainan yanayosafirishwa kwa nchi za nje.

Katika miaka 5 iliyopita, kilimo cha Hainan kilikuwa na ongezeko la 8.3% kwa mwaka, na kinatarajiwa kuwa na ongezeko la zaidi ya 6% katika miaka 5 ijayo, hivi sasa kampuni zenye mitaji ya Taiwan zimepata nafasi nzuri sana ya maendeleo. Wafanyabiashara wanajiendeleza katika sekta ya kilimo ya mkoa wa Hainan kwa kutegemea rasilimali, mitaji na uhodari wao, kwa upande mwingine wakulima wa Hainan nao wamenufaika kutokana na shughuli za wafanyabiashara hao waliotoka Taiwan, hivi sasa kilimo cha Hainan kinapiga hatua kubwa, na ushirikiano huo wa kunufaisha pande zote mbili unapendwa sana na wakulima wa pande mbili za mlango bahari wa Taiwan.

Ofisa wa serikali ya mji wa Haikou anayeshughulikia mambo ya watu kutoka Taiwan, Bw. Zhang Jun alisema, kadiri sera zenye nafuu kwa wafanyabiashara wa Taiwan zinavyotekelezwa, wafanyabiashara hao watakuwa na mustakabali mzuri zaidi kwa maendeleo yao katika Hainan.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-26