Mwaka 2006 China na Afrika zimevutia uangalifu mkubwa wa duniani. Mwezi Novemba mwaka huu, ujumbe wa nchi 48 za Afrika, wakuu na viongozi 41 wa serikali za Afrika walikusanyika mjini Beijing, kuhudhuria mkutano wa kwanza wa wakuu kati ya China na Afrika. Huu ni mkutano mkubwa kabisa kati ya viongozi wa Afrika nje ya bara la Afrika, pia ni mkutano wa kimataifa ambao ni mkubwa kabisa kuliko hapo kabla katika historia ya China. Kwenye mkutano huo viongozi wa China na nchi za Afrika walitangaza kwa pamoja kuanzisha uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi wenye usawa na kuaminiana kisiasa, kufanya ushirikiano wa kunufaishana kiuchumi na kuwa na maingiliano ya kiutamaduni.
Viongozi wa nchi za Afrika walipewa heshima kubwa hapa Beijing. Rais Hu Jintao wa China kwenye tafrija ya kuwakaribisha viongozi wa Afrika alishurukuru sana uaminifu na urafiki uliopo kati ya China na nchi za Afrika. Machoni mwa wachina, waafrika ni watu wenye maadili, waliisaidia Jamhuri ya watu wa China kurejeshewa kiti chake kwenye Umoja wa Mataifa, wanaunga mkono China katika masuala makubwa kama vile suala la Taiwan na haki za binadamu, na kuisaidia China kupata nafasi ya kuandaa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 ya Beijing na maonesho ya biashara ya kimataifa ya Shanghai ya mwaka 2010. Ikiwa nchi pekee inayoendelea kati ya nchi wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, China siku zote iliziunga mkono nchi za Afrika katika juhudi zao za kujipatia ukombozi na uhuru, kulinda mamlaka ya nchi na uhuru wa taifa. Kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Afrika katika mambo ya kikanda, na kuunga mkono Mpango wa NEPAD ambao ni dira ya kuliongoza bara la Afrika kuondokana na umaskini na kulifanya lishiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia.
Kuanzia kushikana mikono kwa mara ya kwanza kati ya viongozi wa China na nchi za Afrika kwenye mkutano wa Bandung miaka zaidi ya 50 iliyopita hadi kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika mwaka huu, uaminifu wa kisiasa kati ya China na Afrika umekuwa ukiimarika siku hadi siku.
Rais Hu Jintao wa China kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika alidhihirisha kuwa, kutokana na hali ilivyo sasa, kuimarika kwa uhusiano kati ya China na Afrika si kama tu kutasaidia kujiendeleza kwa China na Afrika, bali pia kutahimiza mshikamano na ushirikiano kati ya nchi zinazoendelea, kuhimiza ujenzi wa utaratibu mpya wa kimataifa wa kisiasa na kiuchumi wenye haki. China siku zote inapendekeza kujenga dunia yenye masikilizano na yenye amani ya kudumu na ustawi wa pamoja, pendekezo hilo linaungwa mkono na nchi za Afrika. Kwenye taarifa ya mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, viongozi wa China na Afrika wamesisitiza kuheshimu na kulinda kuwepo kwa aina nyingi za utamaduni duniani, nchi zenye ustaarabu na aina tofauti za kujiendeleza zifundishane, kuhimizana na kuishi kwa pamoja kwa masikilizano.
Hivi sasa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika una mustakabali mzuri. Jumla ya thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili huenda itazidi dola za kimarekani bilioni 50, ushirikiano wa kirafiki wa kunufaishana kati ya pande hizo mbili umeanza kuzaa matunda.
Wakati China inapotumia rasilimali kutoka Afrika, pia inawafahamisha watu wa Afrika uzoefu wake mzuri na teknolojia zenye matumizi halisi ilizopata katika mchakato wa kujenga mambo ya kisasa, ili kuzisaidia nchi za Afrika kuinua uwezo wao wa kujiendeleza. Katika miaka mitatu ijayo, China itaanzisha sehemu tatu hadi tano za ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara barani Afrika, kuwatuma wataalamu mia moja wa kilimo wa China katika nchi za Afrika, na kuanzisha vituo kumi vya vielelezo vya ufanisi wa kilimo, kama vile kuwafundisha wakulima wa Afrika jinsi ya kulima mpunga chotara na mahindi chotara yenye mavuno makubwa.
Serikali ya China pia inayahimiza makampuni yenye uwezo wa China kuwekeza katika nchi za Afrika na kuanzisha mfuko wa maendeleo wa China na Afrika wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni tano. Katika miaka ya karibuni China kwa jumla imewekeza dola za kimarekani bilioni 6.27 barani Afrika katika sekta za biashara, uzalishaji na utengenezaji, uchimbaji wa madini, mawasiliano ya simu na kilimo. Mwezi Novemba mwaka huu wajumbe zaidi ya 1,500 wa makampuni ya China na nchi za Afrika walihudhuria mkutano wa wanakampuni wa China na Afrika uliofanyika hapa Beijing, ambao walisaini makubaliano ya ushirikiano yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.9.
Ingawa hivi sasa kuna pengo kubwa la biashara kati ya China na Afrika, lakini China inaendelea kufungua soko lake kwa Afrika, inasamehe ushuru wa aina zaidi ya 440 za bidhaa zilizosafirishwa na nchi zilizoko nyuma kimaendeleo za Afrika.
Ushirikiano kati ya China na Afrika ni wa dhati, viongozi wa China wanasisitiza mara kwa mara kuwa, China bado ni nchi inayoendelea, ina watu maskini milioni 26 waishio vijijini na watu milioni 21 wenye kipato kidogo waishio mijini. Inatakiwa kuimarisha ushirikiano na nchi zilizo nyuma kimaendeleo ili kulinda kwa pamoja haki na maslahi ya nchi zinazoendelea, ili kuweka mazingira mazuri ya kimataifa ya kujiendeleza. Rais Hu Jintao wa China alisema, bila ya amani na maendeleo ya China na Afrika, hakuna amani na maendeleo ya dunia nzima. Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya China ilitoa kwa mara ya kwanza waraka wa sera za China kwa Afrika, na kuelezea sababu ya kustawi kwa ushirikiano na urafiki wa kudumu kati ya China na Afrika kama ni kutendeana kwa dhati, kuwa na usawa na kunufaishana, kushirikiana na kuleta maendeleo ya pamoja.
China siku zote inashikilia kutoa misaada kwa nchi za Afrika bila ya masharti yoyote. Urafiki kati ya wananchi wa China na wa Afrika ulianzia tangu enzi na dahari. Tangu China mpya iasisiwe mwaka 1949, China kwa jumla imetuma madaktari zaidi ya 15,000 kwa nchi 47 za Afrika ambao wametoa huduma za matibabu kwa watu milioni 170 wa Afrika. Siku za baadaye China itaendelea kuzisaidia nchi za Afrika kujenga hospitali 30 na kutoa misaada yenye thamani ya Yuan milioni 300 kwa ajili ya kuanzisha vituo 30 vya kutibu malaria.
Vijana ni kizazi kipya cha urafiki kati ya China na Afrika, kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, China iliahidi kutuma vijana 300 wanaojitolea katika nchi za Afrika, kuzisaidia nchi za Afrika kujenga shule 100 vijijini, ifikapo mwaka 2009, idadi ya wanafunzi wa Afrika watakaopewa udhamini wa kuja kusoma nchini China itafikia 4000 kutoka 2000 ya mwaka 2000.
Idhaa ya kiswahili 2006-12-29
|