Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-29 16:49:42    
Ushirikiano kati ya KBC na CRI una mustakabali mzuri

cri

Bwana David Waweru ni meneja mkuu wa shirika la utangazaji la Kenya KBC, alikuwa ameitembelea China kwa mara mbili mwaka huu, ana mawazo mazuri kuhusu jinsi ya kufanya ushirikiano kati ya shirika la utangazaji la Kenya na Radio China Kimataifa ili kuwafahamisha vizuri wananchi wa China na wa Kenya mambo halisi ya nchi hizo mbili.

CRI: Mheshimiwa Waweru, safari hii umekuja Beijing kuhudhuria mkutano wa kuadhimisha miaka 65 ya CRI, tafadhali uwaelezee kidogo wasikilizaji wetu kuhusu mkutano huo.

Bw. Waweru: Cha kwanza ni kusema kuwa nimefurahia sana kwa mwaliko wa Radio China Kimataifa, walitualika tuje tusherehekee nao miaka 65 tangu kituo hicho cha kwanza cha Radio kilipoanzishwa. Mimi ni pekee yangu kutoka mashirika ya radio ya Kenya pamoja na msikilizaji mmoja wa Kenya. Ni jambo la furaha kualikwa na CRI, kwa hivyo tumefurahia ushirikiano kati yetu na CRI. Natumaini kuwa ushirikiano kati yetu utaendelea vivyo hivyo kwa sababu malengo yetu yanalingana.

CRI: Dakika chache tu kabla ya kufunguliwa kwa mkutano wa maadhimisho, rais Hu Jintao wa China alileta salama za pongezi, na amewaagiza wafanyakazi wa Radio China Kimataifa kuendelea na juhudi kuandaa vizuri zaidi vipindi vya matangazo ya CRI ili kuwahudumia vizuri zaidi wasikilizaji wake popote walipo duniani. Wewe unaonaje? Umeelewa nini?

Bw. Waweru: Nilisikia vizuri na nilikuwa makini kwa sababu tukija hapa Uchina kitu cha kwanza ni kuangalia maendeleo yaliyoendelea na pia kufungua macho kuona yale tunaweza kuiga tukirudi kwetu nyumbani, na kuona rais mwenyewe anafurahia jinsi CRI inavyoweka jitihada za kueneza mambo ya Uchina ili Uchina ijulikane duniani na pia wachina waweze kujua mambo ya nchi nyingine. Nafikiri hiyo ni desturi nzuri sana ya kueneza maendeleo hapa Uchina na pia kujulisha wananchi wengine mambo yanavyoendelea hapa Uchina. Na kweli kuna mambo mengi sana watu wa Kenya wanaweza kujifundisha kwa kulingana na mambo ya Radio.

Nafikiri CRI imeendelea sana kwa sababu sisi Kenya tunataka pia kuwa na kituo cha radio inayosikika Afrika nzima. Na pia tukiendelea hapo mbele tuwe na kituo kinachoweza kurusha matangazo duniani kote. Nafikiri mambo niliyosoma hapa yataniwezesha na kuwezesha KBC kuendelea na mpango wa kuunda KBC International ili tuweze kusikika na pia kueneza mambo ya Kenya kwenye nchi nyingine. Kenya ina mambo mengi sana ya utalii na kilimo. Watu wengi duniani bado hawajaelewa Kenya iko wapi? Ina vifaa vya aina gani vya utalii?

CRI: Wewe unajua kituo cha FM cha CRI huko Nairobi Kenya ni kituo cha kwanza kilichoanzishwa na CRI, na hivi karibuni kituo cha pili cha FM cha CRI kimezinduliwa nchini Laos, umepata habari hiyo?

Bw. Waweru: Ndiyo. Sisi tunaona kuwa katika jitihada za CRI kueneza matangazo yake, wachina wanaona Kenya ni nchi muhimu kwanza kwenye bara la Afrika. Wakenya watajua mambo mengi zaidi kuhusu China.

CRI: KBC inawezekana kutusaidia kuandaa vipindi fulani fulani kama vile tiba na kinga ya ukimwi au maendeleo yaliyopatikana nchini Kenya katika sekta mbalimbali. Unaonaje ushirikiano huo?

Bw. Waweru: Kitu muhimu kwanza ni tuboreshe ule ushirikiano, halafu tunaweza kufanya mambo mengi pamoja ya kunufaisha kampuni zetu mbili. Kituo cha kwanza ni kutoa vipindi pamoja, kuna vipindi vingi tunaweza kushirikiana ambavyo vitaboresha matangazo yenu. Sisi KBC tutawasaidieni kujua vile vipindi wakenya wangependa kusikiliza, pia tushirikiane kutengeneza vipindi ili kuwafahamisha wachina utalii, mila za wakenya, kufanya biashara katika nchi hizo mbili. Kuna mambo mengi tunayoweza kushirikiana ili kufanya vipindi bora zaidi ili mtu akisikiliza CRI kwenye idhaa ya taifa anapendezwa na hicho kipindi, na anapata mawazo zaidi kuhusu mambo ya Uchina.

CRI: Mimi naona kama tunaweza kufanya ushirikiano kama huo, matangazo yetu yatawavutia zaidi wasikilizaji wetu wa Kenya. Sisi tuna imani na tunasubiri juhudi za KBC.

Bw. Waweru: Sasa tunaangalia vipi tunaweza kushirikiana zaidi. Tunaweza hata kubadilisha watangazaji, watangazaji wetu wakija hapa kwenu kubuni vipindi kwa sababu wakiwa hapa wataelewa mambo ya Uchina na pia mambo ya kule Kenya. Pia mnaweza mkatuma watu kwenye KBC ili waongee lugha yetu, yaani watangazaji wa lugha ya Kiswahili ingawa ni wachina. Watajua mambo mengi wakiwa kule, na pia watashirikiana na wakenya wataungana nao na kujua mila zao ili wakati wanapotangaza na mambo mengine kama ya utangazaji ni lazima ujue mila za watu usije ukawakosea. Pia tunaona tukiendelea mbele na michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, nataka tushirikiane, tutatuma watangazaji kadhaa wa michezo kuja hapa ili wakusanye habari na kutengeneza vipindi husika.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-29