Katika sehemu ya mpaka kati ya Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ya kaskazini mashariki ya China na nchi za Russia na Mongolia kuna mji mdogo unaoitwa Manzhouli, ambao ni mji mnadhifu wa kupendeza. Mji huo uko nchini China, lakini mtindo dhahiri wa kirussia unaonekana mjini humo.
Ukitembea barabarani mjini Manzhouli, popote unapokwenda utakutana na warussia wenye nywele ya rangi dhahabu na macho ya kibuluu, na mabango ya majina yaliyobandikwa kwenye milango ya maduka mengi madogo ya aina mbalilmbali yote ni ya maandishi ya Kichina, Kirussia na Kimongolia, hali hii huwababaisha watu na kuwafanya waone kama wako katika nchi za nje. Bi.Xin Mei anayefanya kazi katika hoteli moja mjini Manzhouli alisema:
Hivi sasa warussia wanaokuja mji wetu Manzhouli ni wengi zaidi, hasa wakati wa siku za baridi, kwani mwezi Desemba kuna sikukuu ya Krismas, warussia wengi wanakuja kununua zawadi za siku ya Krismas, kununua nguo, viatu na kofia, kwani bidhaa hizo ziko nyingi nchini China.
Harufu ya kirussia imejaa pote mjini Manzhouli, Uwanja wa Taowa uliojengwa mahsusi mjini humo umekuwa uwanja wenye vivutio kwa watalii kutoka sehemu mbalimbali nchini China. Uwanja huo ni uwanja pekee nchini China wa kufanya utalii, mapumziko na burudani ambapo sanaa za jadi ya Russia za seti moja moja za wanasesere zinaonekana pote uwanjani humo, eneo la uwanja ni mita elfu 60 za mraba, jengo kuu katikati ya uwanja ni seti moja kubwa ya mwanasesere yenye urefu wa mita 30 ambao ni urefu mkubwa zaidi kuliko ule wa seti zote za wanasesere duniani. Seti hiyo kubwa ya mwanasesere inazungukwa na seti zaidi ya 200 za wanasesere na mayai ya rangi ya sikukuu ya Pasaka ya Russia inayoeleza urafiki, ufuatiliaji, heri na baraka. Na katika sehemu inayozunguka chemchemi ya muziki ya uwanja huo pia kuna vinyago vya wanyama 12 wanaowakilisha kila mwaka wa kilimo wa China na alama za nyota 12 zinazoonesha bahati na maendeleo. Kama watalii wanaona uchovu katika matembezi, wanaweza kula chakula kwenye mkahawa ulioko ndani ya seti ya mwanasesere au kuonesha maonesho ya michezo ya sanaa kwenye ukumbi wa kufanyia maonesho.
Katika siku za baridi, mji wa Manzhouli hufunikwa na theluji inayoanguka kila mara. Wakati wa usiku halijoto nje ya nyumba huwa ni nyuzi chini ya 30, lakini hali ya baridi haiwezi kuwazuia watu wasifikie mjini humo kufanya utalii, ambapo utalii kwenye barafu na theluji huwa ni shughuli maalum mjini Manzhouli. Kila ifikapo majira ya siku za baridi, Sikukuu ya barafu na theluji huandaliwa mjini Manzhouli, ambapo wasanii wa China wanatumia barafu na theluji kutengeneza michongo ya aina mbalimbali ya barafu na theluji kama vile watu maarufu katika historia ya China, pamoja na majengo maarufu ya nchi mbalimbali duniani. Na ngazi za kuteleza zilizotengenezwa kwa barafu huwa chombo kizuri kabisa cha kuchezea kwa watoto wakati wa siku za baridi. Mwanafunzi wa shule ya msingi Li Dongsheng aliyezaliwa na kukulia mjini Manzhouli alisema:
Kila ifikapo Sikukuu ya barafu na theluji wakati wa majira ya siku za baridi, watu wengi kutoka nchini China, au kutoka Mongolia na nchi nyingine mbalimbali wanakusanyika mjini kwetu kuimba nyimbo, kucheza ngoma ya jadi ya Yangge, kuchonga michongo ya barafu na theluji ya aina mbalimbali, sisi watoto tunacheza kwenye ngazi za barafu, tunafurahi kweli.
Sherehe ya ufunguzi wa Sikukuu ya barafu na theluji husherehekewa katika hali ya shamrashamra zaidi, kila mwaka watalii kutoka Russia, Mongolia na sehemu nyingine za China huja Manzhouli kushiriki kwenye sherehe hiyo. Mbali na kutembelea maonesho ya michongo mbalimbali ya kupendeza iliyochongwa kwa barafu na theluji, watalii pia wanaweza kutazama maonesho murua ya michezo ya sanaa ya wasanii wa China, Russia na Mongolia, ambapo watu wanacheza ngoma ya jadi ya Yangge, na wasanii wa Mongolia wanafanya maonesho ya mavazi ya kitaifa, na ngoma za makabila ya Russia pia ni maonesho ya kila mwaka katika siku hiyo. Msichana wa Russia Nastya aliyefika Manzhouli kutazama sherehe ya ufunguzi wa Siku ya barafu na theluji alisema:
Napenda michongo ya theluji na maonesho ya michezo ya sanaa kwenye sherehe hiyo, kweli yananivutia sana. Katika miaka ya karibuni warussia wanaokuja Manzhouli kushiriki kwenye Sikukuu ya Barafu na Theluji wanaongezeka mwaka hadi mwaka. Wakati wa Sikukuu hiyo, Manzhouli ina mvuto zaidi kwa warussia.
Mjini Manzhouli pia kuna bidhaa nyingi za aina mbalimbali, kama vile zawadi ndogondogo, kofia za manyoya ya wanyama, bidhaa za Russia na Mongolia, viatu vya ngozi, vioo vidogo vilivyopambwa kwa ngozi za ng'ombe na kondoo na kadhalika.
Manzhouli kweli ni mji mdogo wa China unaoonesha mtindo dhahiri wa kirussia, watalii wakitembelea mji mdogo wataona kama wametembelea nchi moja. Meya wa mji wa Manzhouli Bwana Wu Haofeng alisema:
Mji wa Manzhouli uko katika sehemu za mipaka kati ya China, Russia na Mongolia, hivyo utamaduni wa nchi hizo tatu unaingiliana na kupatana, na Siku ya Barafu na Theluji ya Manzhouli ni siku ya kimataifa, hali hii haionekani katika miji mingi ya ndani nchini China.
Idhaa ya Kiswahili 2007-01-15
|