Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-16 14:55:22    
Kilimo cha kisasa chabadilisha hali ya unyonge wa sehemu ya vijiji nchini China

cri

Kuanzia mwaka huu China itafanya ujenzi kamambe wa kujenga vijiji vipya kote nchini na kutoa ruzuku kubwa kwa ajili ya kuboresha zana za uzalishaji mazao na maisha ya wakulima ili kupunguza tofauti kati ya miji na vijiji. Kati ya kazi hizo, kazi ya kubadilisha kilimo cha jadi kilichopitwa na wakati na kuanzisha kilimo cha kisasa chenye ufanisi mzuri, ni moja ya kazi muhimu za kujenga vijiji vipya.

Kwenye mkoa wa Helongjiang ulioko kwenye sehemu ya kaskazini mashariki mwa China, kuna kijiji kinachojulikana kwa jina la "Xing Shisi". Kijiji hicho kilijengwa na wahamiaji waliotoka sehemu nyingine miaka 50 iliyopita, hapo mwanzo eneo la kijiji hicho lilikuwa ni pori, na hakukuwa na nyumba wala shamba. Lakini hivi sasa kijiji cha Xing Shisi kimekuwa ni kijiji tajiri kinachojulikana sana huko. Mwandishi wetu wa habari alipofika huko aliona barabara ya saruji inayopita kwenye kijiji pamoja na nyumba nyingi nzuri zenye bustani zilizojengwa kwenye kando mbili za barabara. Alipoingia kwenye nyumba za wakulima zenye eneo la mita za mraba zaidi ya 200, aliona vyombo vya umeme vya kisasa pamoja na magari madogo.

Mzee Zhang Weiliang mwenye umri wa miaka 75 alikuwa mmoja wa kundi la kwanza la watu waliohamia huko. Alipotaja hali ya kijiji hicho kabla ya miaka 50 iliyopita, alisema,

"Nilipofika hapa palikuwa ni pori kubwa kabisa, hakukuwa na chochote isipokuwa nyasi tu. Tulijenga vibanda vya nyasi na kuishi kwenye vibanda hivyo, usiku ukivuma upepo, asubuhi ya siku iliyofuata nyuso zetu zilikuwa na vumbi jingi."

Wakati mwingine mzee Zhang Weiliang haamini kama maisha yake mazuri ya sasa ni ya kweli, anasema anadhani kama anaota. Hivi sasa karibu familia 200, ambazo ni 80% ya familia za wakazi wa kijiji hicho, zinaishi katika nyumba nzuri zenye bustani, na pato la wakulima linaongezeka mwaka hadi mwaka. Takwimu zinaonesha kuwa, jumla ya pato la kijiji cha Xing Shisi lilifikia Yuan bilioni 1 mwaka 2005.

Chanzo kikuu cha mabadiliko ya kijiji cha Xing Shisi ni kuendeleza kilimo cha kisasa. Kabla ya miaka mingi iliyopita, kijiji cha Xing Shisi kilianza kuendeleza matumizi ya mitambo ya kilimo na kujenga miradi ya kumwagilia maji mashamba, na mashamba zaidi ya hekta 1,000 yalipewa kwa familia 18 kwa utaratibu wa kandarasi. Pato la familia ya mzee Liu Hongwei katika mwaka 2006 linatarajiwa kufikia Yuan karibu laki 5. Pato kubwa linamfurahisha mzee Liu, anasema yote hayo yanatokana na kilimo cha kisasa.

"Wataalamu wa kilimo wa wilaya yetu wanatuletea masomo kila mwaka, wanatueleza mazao yanayofaa kupandwa katika sehemu yetu. Sisi tunaozalisha nafaka, kila mwaka tunakwenda sehemu ya nje kujifunza."

Pato kubwa limeongeza juhudi za familia zinazozalisha nafaka za kijijini humo. Mzee Liu Hongwei alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa mwaka 2007 amenuia kutumia mbegu mpya za mahindi, ambazo kila hekta inaweza kuwa na ongezeko la mavuno ya tani 7.5 hivi.

Baada ya kutumia mitambo katika shughuli za kilimo, watu wengi wa kijiji cha Xing Shisi wameanzisha shughuli za usindikaji wa mazao ya kilimo. Hivi sasa kijiji hicho kimeanzisha kampuni ya Fuhua ya Helongjiang ya ngazi ya taifa ikishughulikia kazi za kilimo, misitu, ufugaji mifugo na utalii. Naibu kiongozi wa kiwanda cha dawa cha Fuhua Bw. Zhang Kecheng alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, maendeleo ya kampuni ya kijiji hicho yanatoa uungaji mkono mkubwa kwa kilimo cha huko na kuhimiza maendeleo ya uchumi wa sehemu ya vijiji kwa jumla.

"Kampuni yetu inahusiana na usindikaji wa chakula, hivyo wakulima wanapata bei nzuri ya mazao yao; Pili, ziada ya nguvu-kazi ya kijijini inaweza kupangwa katika kazi za kiwandani, licha ya kuweza kuongeza pato lao, wanaweza kujifunza ufundi."

Zhang Kecheng alipata mafanikio ya kusoma katika chuo kikuu katika miaka ya 80 ya karne iliyopita. Baada ya kumaliza masomo yake, alirudi kufanya kazi katika kiwanda cha kijiji akiona maendeleo ya kampuni yataweza kuhimiza maendeleo ya uchumi wa kijiji. Anatarajia kutoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa kijiji kwa kutumia elimu aliyopata. Katika kijiji cha Xing Shisi kuna wanafunzi wengi waliomaliza masomo ya chuo kikuu, licha ya hayo kampuni ya kijiji imeajiri wataalamu kutoka sehemu nyingine za China.

Kijiji cha Xing Shisi kinazingatia umuhimu wa mgawanyiko wa viumbe na kujitahidi kuboresha mazingira ya asili. Licha ya kupanda majani na maua kwenye sehemu za mbele na nyuma za nyumba, wanakijiji wamepanda msitu wa kuzuia upepo na mchanga. Kiongozi mmoja wa kijiji hicho Bw. Fu Huating alisema, hivi sasa eneo la msitu huo limefikia zaidi ya hekta 600, ambao licha ya kuleta hali nzuri ya mgawanyiko wa viumbe kwenye kijiji cha Xing Shisi, bali pia wamewawekea mali ya urithi kwa vizazi vyao. Alisema,

"Kujenga baadhi ya nyumba siyo kujenga kijiji kipya, kitu muhimu sana ni mazingira ya mgawanyo wa viumbe. Tukipanda majani na maua mengi mbele na nyuma za nyumba zetu, mazingira yataboreshwa, na ujenzi wa kijiji utaweza kufikia kiwango cha juu. Kwa hiyo tukitaka kubadilisha kabisa sura ya kijiji, hatuna budi kupanda miti mingi na kuboresha mazingira."

Pamoja na maendeleo ya uchumi wa kijiji cha Xing Shisi, kijiji hicho kimeharakisha hatua za kukuza huduma za umma. Kijiji cha Xing Shisi cha hivi sasa licha ya kuwa na barabara safi, miundo-mbinu kamili na kijiji hicho kinaelekea kuwa mji mdogo wa sehemu ya vijijini. Kijiji cha Xing Shisi kimejenga jumba la utamaduni na uwanja wa michezo, vitu ambavyo vimeboresha maisha ya utamaduni kwa wakulima. Kiongozi wa kijiji cha Xing Shisi Bw. Fu Huating alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa kijiji hicho kimebuni mpango wa maendeleo wa miaka 5 ijayo, kikitarajia kuleta manufaa makubwa zaidi kwa wanakijiji wao:

"Kwanza ni kufanya jumla ya pato la kijiji kuongezeka kwa Yuan bilioni 4; Pili, kufikisha wastani wa pato la kila mkazi kuwa Yuan elfu 20; Tatu, kila familia iwe na nyumba moja nzuri yenye bustani; Nne, huduma kwa wanakijiji wote zifikie kiwango cha watumishi wa serikalini, na kuwa na kiunua mgongo cha uzeeni ndani ya miaka 2 au 3 ijayo ili kuwafanya wakulima wasiwe na wasiwasi kuhusu maisha yao ya uzeeni.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-16