Fainali ya mashindano ya tatu ya kumtafuta mwanamitindo mrembo wa China ilimalizika hivi karibuni huko Sanya, mkoani Hainan, kusini mwa China. Wasichana wapatao 48 kutoka kila kona ya China walishiriki kwenye kinyang'anyiro hicho. Msichana Gulpiye mwenye umri wa miaka 14 tu kutoka kabila la Wauygur ni mmoja kati ya wasichana hao. Yeye ni msichana mdogo kuliko wenzake wengine walioshiriki.
Msichana Gulpiye ni mrefu, ana nywele ndefu zenye rangi ya manjano kwa kiasi, sura yake inaonesha umaalumu dhahiri wa wasichana wa kabila la Wauygur. Katika mashindano hayo, alishinda taji la mwanamitindo bora na tuzo ya waamuzi. Gulpiye alisema "Nafurahi sana kupata tuzo ya waamuzi. Katika mashindano haya sikuwa na wasiwasi, nilijiamini sana. Mimi bado nina umri mdogo, nitapata nafasi nyingine nyingi katika siku zijazo, kwa hiyo nisingejisikia vibaya hata kama nisingepata tuzo yoyote."
Msichana Gulpiye hivi sasa ni mwanafunzi wa shule moja ya sekondari mjini Urumuqi, mkoani unaojiendesha wa Xinjiang Uygur. Alisema anapenda muziki na dansi. Katika mashindano ya kanda ya Xinjiang ya kinyang'anyiro cha kumtafuta mwanamitindo mrembo wa China, Gulpiye alipata ubingwa wa kanda. Kwenye fainali ya mashindano hayo iliyowashirikisha wasichana kutoka sehemu mbalimbali za China, msichan Gulpiye aliwavutia waamuzi na kushangliwa na watazamaji wengi kwa kucheza ngoma ya kabila la Wauygur.
Ngoma hiyo ilibuniwa na mama yake hasa kwa ajili ya mashindano hayo. Wazazi wa Gulpiye walikuwa wakiambatana naye siku zote kwenye mashindano hayo. Mama yake Bibi Bahargul alisema "Kutokana na kushiriki kwenye mashindano hayo, amepata uzoefu na kuhakikishwa uwezo wake. Hii vile vile ilikuwa fursa kwake kuonesha uzuri wake. Naona jambo muhimu zaidi ni kushiriki. Kwa hakika tumefurahia sana tuzo aliyopata. Hii ni mara yake ya kwanza kushiriki kwenye mashindano ya nchi nzima, na kupata tuzo, sisi wazazi tunaridhika sana."
Kinyang'nyiro cha kumtafuta mwanamitindo mrembo wa China kinafanyika kila mwaka, ni mashindano ya ngazi ya taifa yanayowashirikisha wasichana wa hali mbalimbali, ama ni wanamitindo au hawajaingia sekta hiyo.
Msichana Gulpiye anapenda kujipamba tangu alipokuwa mtoto mdogo. Alitizama vipindi vya televisheni kuhusu wanamitindo walivyoonesha jukwaani, Gulpiye alikuwa na ndoto kuwa siku moja yeye mwenyewe angeweza kuonesha jukwaani. Kutokana na uungaji mkono wa wazazi wake, msichana Gulpiye mwenye umri wa miaka 14 alianza kupata mafunzo kutoka kwa kampuni moja ya wanamitindo huko Xinjiang. Mama yake Bibi Bahargul alisema "Alipenda sana kujipamba tangu alipokuwa mtoto mdogo. Alikuwa anavaa nguo zangu na kutembea kama wanamitindo wanavyoonesha jukwaani, huku akisema mama niangalie, mama niangalie. Niliona kuwa, aliiga vizuri mfano wa wanamitindo. Kila mara nikimnunulia mwanasesere, alitengeneza nguo kwa mwanasesere, kama vile nguo za kushiriki kwenye sherehe na nguo za starehe, nguo za aina fulani ziliambatana na mtindo fulani ya nywele. Alivutiwa na shughuli za namna hii tangu utotoni mwake. Naona ana kipaji. Sasa anakua siku hadi siku, tunatumai kuwa anaweza kupata uzoefu mwingi na kuonesha uzuri wake, kwa hiyo tulimpeleka kwenye kampuni ya wanamitindo ili apate mafunzo rasmi."
Akiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari, msichana Gulpiye anapaswa kusoma darasani kama wanafunzi wenzake wanavyofanya, kwa hiyo anashiriki kwenye mafunzo ya mitindo katika siku za wikiendi. Katika mafunzo hayo, alipaswa kufanya mazoezi ya kutembea jukwaani mara kwa mara, akivaa viatu vyenye visigino virefu, miguu yake ilisumbuliwa sana. Lakini dada Gulpiye alivumilia usumbufu kutokana na ndoto yake. Alisema "Nilifanya mazoezi ya kutembea jukwaani nikiwa nimevaa viatu vyenye visigino virefu, ambavyo viliharibu miguu yangu mara kwa mara, hata nilitokwa damu. Kwa sababu napenda kazi hiyo ya kuonesha mitindo, sikuona uchungu katika mazoezi hayo."
Mazoezi hayo yalimsaidia msichana Gulpiye apate maendeleo kwa haraka sana. Kushiriki kwenye mashindano ya ngazi ya taifa pia ni fursa muhimu. Kabla ya mashindano hayo, msichana Gulpiye na wazazi wake walifanya maandalizi yote. Jitihada zake na uungaji mkono wa wazazi wake zilizaa matunda. Gulpiye alisema "Ninafurahi sana kupata tuzo. Kwanza ninawashukuru baba na mama. Nilipoanza kushiriki kwenye mafunzo ya kuonesha mitindo, wazazi wangu walikuwa wananiunga mkono sana katika kila upande. Naona bila ya uungaji mkono wao, nisingeweza kuonesha moyo wa kujiamini jukwaani. Mafanikio niliyopata pia yanatokana na juhudi zao."
Shule ya dada huyo pia inamwunga mkono. Gulpiye alipokwenda miji mingine kushiriki kwenye mashindano, alikosa masomo kwa siku kadhaa. Walimu walimfundisha masomo hayo wakati wa mapumziko. Walimu wake walieleza kufurahia mwanafunzi wa namna hii aliyependa sekta ya kuonesha mitindo. Mkuu wa shule hiyo ya sekondari Bw. Chen Tao alisema "Shule yetu inawahamasisha wanafunzi wapate maendeleo katika shughuli zote. Gulpiye ana kipaji katika sekta ya kuonesha mitindo, sisi viongozi wa shule tunafuatilia maendeleo yake. Siku nyingine akienda kushiriki kwenye mashindano, mazoezi au kwenye harakati mbalimbali, upande wa shule unamwunga mkono."
Mbali na kusoma shuleni, msichana Gulpiye pia anapenda kupiga piano. Mliyosikia ni rekodi ya muziki aliyopiga. Katika mashindano yaliyomalizika hivi karibuni, Gulpiye mwenye umri wa miaka 14 aling'ara kwenye sekta ya kuonesha mitindo ya China. Na hivi sasa amerudi darasani na kukabiliana na mtihani wa kuingia sekondari ya juu. Gulpiye alisema, anatoa kipaumbele kwa masomo, kupata ujuzi mwingi zaidi na kuinua uwezo.
Idhaa ya kiswahili 2007-01-18
|