Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-25 15:19:07    
Kuwatembelea Wamaonan nyumbani kwao

cri

Kabila la Wamaonan lina watu wapatao elfu 80 tu, ni moja kati ya makabila madogomadogo 22 yenye watu wachache nchini China. Wamaonan wanaishi kwenye mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi, kusini mwa China. Awali watu wa kabila hilo walikuwa wakiishi milimani wakitengana na wengine, na maisha yao yalikuwa magumu sana. Katika miaka ya hivi karibuni, Wamaonan walihamia na kuishi kwenye sehemu ya tambarare, pia walianza kuwasiliana na watu wa makabila mengine. Je, watu hao sasa wanaendelea vipi?

Mwandishi wa habari alipanda basi huko Nanning, mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi. Baada ya safari ya saa zaidi ya 4 alifika Huanjiang ambayo ni wilaya inayojiendesha ya kabila la Wamaonan. Huanjiang ni mji unaozungukwa na mto na milima. Katika kijiji cha Chengshuang kilichopo umbali wa kilomita 10 na mji wa Huanjiang, mwandishi wetu wa habari alikaribishwa kuingia kwenye nyumba ya matofali yenye ghorofa mbili. Mwenye nyumba hiyo anaitwa Lu Jiangbei, ambaye ana umri wa miaka zaidi ya 50. Bwana huyo alisema miaka 10 iliyopita familia yake ilikuwa ikiishi milimani. Alikumbusha akisema "Sehemu tuliyoishi iko milimani ambapo hakuna barabara. Ilikuwa inatubidi tutembee kwa miguu milimani. Tukienda sokoni, tulibeba mizigo ya kilo 25 na kutembea kwa miguu kwa saa 5. Tuliondoka nyumbani kabla hakujapambazuka, na kurudi nyumbani baada ya saa 5 usiku, tukiwa na mwenge au tochi. Tulisumbuliwa sana, kwani hakuna barabara ilitubidi tukanyange mawe, na milimani kuna miti mingi, baada ya mvua ilikuwa ni rahisi kuteremka. Wazee wenye umri unaozidi miaka 50 na 60 walishindwa kutembea katika hali hiyo."

Ili kuboresha maisha ya Wamaonan, tangu mwishoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, serikali ya China ilianza kuwahamisha kutoka milimani hatua kwa hatua. Serikali ilijenga nyumba kwenye sehemu ya tambarare na kuwapanga Wamaonan katika nyumba hizo. Zaidi ya hayo barabara ilijengwa katika sehemu hiyo, huduma za umeme na maji pia ziliboreshwa. Bw. Lu alieleza kuridhika na sehemu wanapoishi hivi sasa, alisema  "Hapa ni bora, kuna barabara safi na umeme, tumenunua televisheni, simu na motokaa. Wenzangu pia wamenunua vitu hivyo. Tukienda kwenye mji wa Huanjiang, inatuchukua muda usiozidi nusu saa."

Tangu kuhama kutoka milimani, watu wa kabila la Wamaonan walianza kupata ufahamu kuhusu dunia na kuvutiwa na dunia hii. Wamaonan wengi wameondoka makwao wakifanya kazi katika sehemu ya pwani ya kusini mashariki ya China ambayo imeendelezwa zaidi kiuchumi. Mtoto wa Bw. Lu aitwaye Lu Kang ni mmoja kati yao. Mwaka 1990 Lu Kang alikuwa hajatimiza umri wa miaka 20, alikwenda Shenzhen, mji wa kusini mashariki ya China. Huko Shenzhen, kijana huyo aliwahi kufanya kazi za vibarua viwandani, kuwa mpishi kwenye mikahawa, na baadaye alipokuwa na akiba kiasi, alijifunza udereva kwa kutumia fedha hizo. Miaka kadhaa baadaye, Lu Kang alirudi makwao na kuanzisha biashara yake ya mawasiliano.

Kijana huyo alisema "Nataka kuendeleza biashara hiyo ya mawasiliano. Ndugu yangu mdogo pia alifanya kazi huko Shenzhen. Nilimwita arudi nyumbani na nimfundishe udereva. Mume wa dada yangu mdogo anafanya biashara ya kukarabati magari, familia yake yote inafanya shughuli zinazohusu magari. Mimi pia nataka kufanya biashara inayohusiana na magari, na kuiendeleza sana."

Katika wilaya ya Huanjiang, kuna Wamaonan wengi mfano wa Bw. Lu Kang, ambao walitafuta ajira nje na baadaye kurudi makwao kuanzisha biashara yao. Walipokuwa wanafanya kazi nje waliweka akiba ya fedha, kujifunza ufundi wa kazi, na kupata mawazo mapya. Hivi sasa huko Huanjiang, asilimia zaidi ya 60 ya viwanda vya huko vilianzishwa na watu wa kabila la Wamaonan waliowahi kufanya kazi nje.

Wakati mazungumzo kati ya mwandishi wetu wa habari na mzee Lu na mwanae yalipoendelea, kijana mmoja aliingia kwenye nyumba hiyo. Mzee Lu akiwa na majivuno alimtambulisha kijana huyo kwamba yeye ni mtu wa kwanza wa familia yake aliyesoma chuo kikuu. Kijana huyo anaitwa Lu Jie ni mpwa wa mzee Lu, hivi sasa ni mtumishi wa serikali anayefanya kazi katika serikali ya wilaya ya Huanjiang. Lu Jie alikumbusha jinsi alivyopata barua iliyomwarifu kuwa ameandikishwa na chuo kikuu kimoja, alisema  "Nilipopata barua hiyo wazazi wangu walikwenda kuwaarifu jamaa zetu na kuwaalika kwenye chakula. Kuandikishwa na chuo kikuu kulimaanisha kuwa hatma yangu imebadilika kabisa, nilidhani kuwa kwa hakika sitaishi milimani."

Lakini baada ya kusoma chuo kikuu huko Shanghai, ambao ni mji mkubwa wa viwanda na biashara kuliko miji mingine ya China, kwa nini Lu Jie alirudi Huanjiang? Kijana huyo alijibu akisema "Niliona maskani yangu kuna umaskini, mimi mwenye nilitoka kwenye sehemu ya milimani iliyoko mbali na mji, kwa hiyo nilipokwenda nje kusoma chuo kikuu na kupata ujuzi, nilitaka kurudi kwenye maskani yangu na kutoa mchango katika ujenzi ili maendeleo yapatikane kwa haraka. Wakati huo mbali na mimi, wanafunzi wenzangu waliosoma huko Beijing na Tianjin pia walifikiri kama mimi."

Tokea mwaka 2001, kila mwaka vijana 400 au 500 hivi kutoka kabila la Wamaonan walikuwa wanaandikishwa na vyuo vikuu mbalimbali, ambao wengi wakihitimu walirudi nyumbani. Bw. Lu Jie alisema  "Katika miaka 10 iliyopita tangu nianze kufanya kazi, nilishuhudia maendeleo makubwa ya maskani yangu. Awali niliporudi nyumbani kutoka chuo kikuu, kulikuwa na simu moja tu katika wilaya nzima, hivi sasa wakulima karibu wote wanatumia simu za mkononi. Hata mimi sikuweza kutabiri kama sehemu hii ingeendelezwa namna gani baada ya miaka 20."

Idhaa ya kiswahili 07-01-25