Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-29 11:48:12    
Mwigizaji mashuhuri wa filamu Bi. Gong Li

cri

Katika siku za karibuni filamu inayoitwa "Askari Wenye Deraya Kote Mjini" ambayo iliongozwa na Zhang Yimou na kuigizwa na Bi. Gong Li inaoneshwa katika majumba yote ya filamu mjini Beijing. Huu ni ushirikiano wa pili katika uigizaji wa filamu kati ya mwongoza filamu Zhang Yimou na mwigiza filamu Gong Li katika muda wa miaka kumi iliyopita.

Mwaka 1986 Gong Li alipokuwa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Uigizaji cha Beijing alipata fursa iliyobadilisha maisha yake, kutokana na kuchaguliwa na mwongoza filamu Zhang Yimou kuwa mwigizaji mkuu katika filamu ya "Mtama Mwekundu". Filamu hiyo ilipata mafanikio makubwa nchini China na nchi za nje na ilipata tuzo ya Tamasha la Kimataifa la 38 la Filamu mjini Berlin. Katika tamasha hilo Zhang Yimou na Gong Li walijulikana kutokana na usanii mkubwa wa filamu yao. Tokea hapo, Gong Li aliigiza filamu kadhaa mfululizo zilizoongozwa na Zhang Yimou, na zote zilipata mafanikio makubwa. Katika filamu hizo Gong Li alionesha mitindo tofauti ya wanawake wa China. Kutokana na uhodari wake mkubwa wa uigizaji alipata tuzo ya mwigizaji bora kabisa katika tamasha la kimataifa la filamu la 49 la Venice. Hii ni tuzo ya ngazi ya juu kabisa miongoni mwa waigizaji wa filamu wa kike nchini China. Mwaka 1996 alijiunga na Hollywood, lakini mwanzoni hakupata nafasi aliyopenda kuigiza. Alisema,

"Kama hakuna filamu na nafasi ninayopenda kuigiza naona ni heri nipumzike kuliko kuigiza, na ninapopumzika ni wakati wangu mzuri wa kuimarisha uwezo wangu, nawatembelea marafiki zangu na kuburudika na maisha yangu ya kawaida. Sitaki kuwa ua kama pambo tu katika filamu."

Ingawa Gong Li hakupata fursa aliyoipenda katika muda wa miaka kadhaa, lakini hakutoweka katika nyanja ya filamu, bali kutokana na uhodari wake wa uigizaji wa mtindo wa Kichina alijulikana sana katika nyanja ya filamu ya kimataifa. Mwaka 1997 Gong Li alichaguliwa kuwa mwamuzi katika kamati ya uamuzi wa kutathmini filamu katika tamasha la kimataifa la filamu la Canne, na kuanzia mwaka 2000 katika nyakati tofauti alikuwa mwenyekiti wa kamati ya kutathmini filamu katika matamasha ya filamu ya Berlin, Venice na Tokyo, alikuwa kama mwakilishi wa sanaa ya filamu ya China katika nyanja ya kimataifa ya filamu. Kuhusu kuwa mwenyekiti wa kamati ya upimaji katika matamasha ya filamu ya kimataifa, Gong Li alieleza,

"Kwa kuwa mwenyekiti, nina wajibu wa kuwaongoza waamuzi kumi wa kamati hiyo ambao wanatoka nchi mbalimbali na wote ni watu hodari na wana mawazo yao wenyewe kuhusu filamu zilizoshiriki kwenye matamasha, namna ya kuwaongoza na kufanya uamuzi wa mwisho kwa haki bila kuwa na migongano nao ni kazi ngumu, na maoni ya upimaji wako yakiwa ya haki, waamuzi wanaona wewe ni mtu mwadilifu na wanakuheshimu, na wao pia wanaacha upendeleo na kukubali uamuzi wa haki."

Baada ya kuwa kimya kwa miaka kadhaa, mwaka 2005 Gong Li alishiriki tena kwenye uigizaji wa filamu ya Hollywood iitwayo "Kumbukumbu za maisha ya mburudishaji wa kike" na "Machafuko ya Miami". Katika filamu ya "Machafuko ya Miami" Gong Li aliigiza kama hawara wa kiongozi wa genge la watu wabaya. Ili aweze kuiga vizuri, Gong Li alitumia miezi mitatu kujifunza kutumia bunduki, na kuendesha mataboti, alisema nafasi hiyo inamvutia.

"Uigizaji wa nafasi hiyo kwangu ni mara ya kwanza, na maishani mwangu sikuwahi na ilikuwa haiwezekani kuwasiliana na watu wabaya kama hao, kweli nimejifunza mengi wakati filamu hiyo ilipopigwa."

Na vile vile kutokana na kuigiza nafasi ya aina mpya katika filamu, baada ya filamu ya "Machafuko ya Miami" alishiriki kwenye filamu ya "Askari Wenye Deraya Kote Mjini" iliyoongozwa na Zhang Yimou. Katika filamu hiyo Gong Li aliigiza kama malkia mmoja wa China ya kale aliyekuwa na utatanishi wa kimawazo. Mwongoza filamu hiyo Bw. Zhang Yimou alisema, ni Gong Li tu ndiye anayeweza kuigiza vizuri kwenye nafasi hiyo ya malkia.

Akiwa mwigizaji anayejulikana duniani kwa miaka mingi, Gong Li hakupokea maombi mengi ya kucheza filamu, bali wakati mwingi alikuwa anasubiri tu nafasi nzuri na filamu nzuri ambazo anaona zinamfaa. Gong Li ambaye sasa amekuwa mtu wa makamo anaelewa zaidi uhusiano kati ya sanaa na maisha ya mwigizaji. Alisema, kutokana na umri unavyoongezeka mwigiza filamu ana mambo mengi ya kufanya. Alisema,

"Kuwa na umri mkubwa si vibaya kwa mwigiza filamu, kuishi kwingi ni kuona mengi, unaweza kuigiza nafasi yako kwa kina zaidi. Wakati ulipokuwa kijana unaigiza kijuu juu tu bila kufahamu maisha yenyewe, lakini ukiwa na umri mkubwa unaweza kuigiza kwa kina zaidi."

Siku zilizopita Gong Li alikuwa Hong Kong kufanya uenezi wa filamu aliyoigiza "Askari Wenye Deraya Kote Mjini". Watazamaji waliowahi kuona filamu zake za zamani wameona uigizaji wake wa aina mpya kabisa katika filamu hiyo.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-29