Mji wa Chongqing uko kwenye eneo la kusini magharibi mwa China, mji huo unajulikana kwa sura yake pekee ya kijiografia, ambao unasifiwa na watu kuwa "mji wa mlimani" na unawavutia watalii wengi kutoka nchini na nje kutalii mjini humo. Mito miwili Changjiang na Jialin inapita kwenye mji huo, na kuugawanya kuwa na kando nne za mito. Katika miaka iliyopita kandoni mwa mito, zilijengwa nyumba nyingi za mbao ambazo zilining'inia kwenye nguzo za miti zikiegemea miamba ya mlima kandoni mwa mito. Hongyadong ni eneo moja la majengo mengi ya namna hii, eneo hili ni kama kisukuku cha "utamaduni wa gati". Mtalii kutoka Mkoa wa Guangdong Bi. Liu Dan alitembelea eneo hilo kwa mara ya kwanza, alisema:
Eneo la Hongyadong lilijengwa kwa kuegemea mlima, majengo ya kale na sura ya kisasa yanapatana na kupendekeza.
Majengo ya Hongyadong yalijengwa kwenye eneo la Chaotianmen mjini Chongqing ambapo ni sehemu inayopakana kwa maji ya Mito Changjiang na Jialinjing, majengo ya mbao yalijengwa kwenye kando za mito yakiegemea miamba mirefu, ambapo majengo yanatambaa kwa kufuata sura ya mlima, eneo hilo lina urefu wa mita 600, majengo yote yanapitapita kwenye ngazi 11 ambayo yote yanaegemeana kwa kufuata mwelekeo wa mlima, kuna pengo la kimo cha mita 75 kati ya majengo yaliyojengwa kwenye ngazi ya juu na yaliyojengwa kwenye ngazi ya chini kandoni mwa mito.
Na katikati ya majengo hayo yanayoning'inia kwenye nguzo za miti pia kuna njia mbili, moja iko umbali wa mita 30 kutoka chini ya ardhi, na nyingine iko umbali wa mita 47 kutoka chini ya ardhi. Ilisemekana kuwa, hivi sasa duniani hakuna majengo kama hayo yaliyojengwa kandoni mwa mito na kati yao kuna pengo la kimo la juu namna hii. Majengo hayo yalipambwa kwa michongo iliyopakwa rangi mbalimbali, ambayo inaonekana kama majengo yaliyoko peponi. Mkazi wa Chongqing Bwana Liu Xian alisema:
Majengo hayo yameonesha historia na utamaduni wa Chongqing. Historia na utamaduni wa mji huo unaenea kwa njia hiyo, kweli thamani yake kubwa inaonekana zaidi katika shughuli za utalii. Watalii wakifika huko wanaweza kutambua historia ya Chongqing, vilevile wanaweza kusikia harufu ya zama za hivi sasa. Eneo la Hongyadong ni kivutio cha utalii mjini Chongqing.
Watalii wakipanda lifti kutoka kwenye ukumbi wa sehemu ya utalii wanaweza kupanda mara moja kwenye roshani ya kuangalia sura ya mji kwenye ghorofa ya 11. Kwenye roshani hiyo yenye eneo la mita 7000 za mraba, watalii wanaweza kutazama mandhari nzuri ya mji wa Chongqing ulioko kandoni mwa mito na mlima, na kuona hali ya ustawi wa mji huo, ambapo mawimbi ya maji ya mito miwili inayopatana huko yanakwenda kwa kasi. Wakishuka chini kwa kufuata ngazi ya mawe mlimani wataona njia moja yenye vipengele iliyoko katikati ya majengo yanayoning'inia kwenye nguzo za miti na miamba mirefu ya mlima, watavutiwa na sura ya kipekee ya eneo la Hongyadong lenye vivutio.
Kwenye njia hiyo kuna maduka mbalimbali yanayouza bidhaa za aina tofauti kutoka Afrika ya kati, Uturuki, Australia, Japan na Korea ya kusini, ambapo watalii wanaweza kuvutiwa na utamaduni wa nchi mbalimbali duniani. Meneja mkuu wa Kampuni ya utalii ya Tianer Bwana Liu Jun alisema:
Kwa kuwa eneo la Hongyadong limegawanywa kwenye ngazi 11, hivyo watalii wanaweza kupata chakula, malazi, kutembelea sehemu zenye vivutio, kununua vitu na kufanya burudani, kweli eneo hilo lina mvuto kwa watalii.
Bwana Liu Jun alifahamisha kuwa, kwenye njia hiyo yenye vipengele vingi kuna mikahawa mingi, ambapo watalii wanaweza kupata vyakula vya mapishi tofauti ya nchi mbalimbali duniani, vikiwemo pamoja na bata wa kuokwa wa Beijing, vitoweo vya mapishi ya Shanghai, vyakula vya mapishi ya Hong Kong pamoja na vingine vya nchi mbalimbali za Asia na Ulaya. Mbali na mikahawa hiyo, pia kuna mikahawa ya chai ya aina mbalimbali, baada ya kula chakula katika mikahawa, watalii wanaweza kunywa chai katika mikahawa ya chai, wakipiga soga na kujiburudisha kwa raha mustarehe.
Watalii wakitembea kwenye njia mbili katikati ya majumba yanayoning'inia, pia wanaweza kutazama michezo ya sanaa na sarakasi inayooneshwa kwenye sehemu mbalimbali. Vilevile wanaweza kununua mazao mbalimbali maalum ya Chongqing na vitu vya kumbukumbu za utalii. Wakati wa usiku, mandhari ya huko ni tofauti na ile ya mchana, taa elfu 50 za rangi mbalimbali zinayapamba majumba yanayoning'inia ya Hongyadong kuwa kama peponi, ambapo mtaa wa baa kandoni mwa mto unawavutia zaidi watalii. Bwana Liao Changguang alisema:
Katika eneo la Hongyadong, wakati wa usiku ukiwadia, watalii wanaweza kushuhudia maisha ya jadi ya wakazi wa huko, kila saa mpiga kibao anapiga kibao kutangaza saa, wasanii wenyewe wa Chongqing wanakusanyika kwenye eneo la Hongyadong kufanya maonesho ya michezo ya sanaa, utamaduni wa aina mbalimbali wa Chongqing unaonekana kwenye eneo Hongyadong linaloegemea miamba ya mlima.
Idhaa ya kiswahili 2007-01-29
|