Katika kijiji cha Husa, mkoani Yunnan kusini magharibi mwa China, kila asubuhi majira ya saa 12 zinasikika kelele za kutengeneza visu.
Kijiji hicho kina wakazi mamia kadhaa, ambao ni watu wa kabila la Waachang. Miongoni mwa wanakijiji hao, familia zaidi ya mia moja zinafahamu ufundi wa kutengeneza visu. Kati ya mafundi hao, Bw. Xiang Laosai anajulikana kama "bingwa wa kutengeneza visu". Bw. Xiang mwenye umri wa miaka 45 anaonekana na tabasamu siku zote, alitwaa ubingwa katika mashindano ya kutengeneza visu kwa sababu visu alivyotengeneza ni vizuri na imara.
Bwana huyo alikumbusha akisema "Shindano moja lilikuwa kukata msumari. Visu kadhaa vilishindwa kukata msumari, badala yake visu vyenyewe viliharibika. Katika shindano lingine baadhi ya visu vilishindwa kuvunja kipande cha mbao. Nilijaribu kwa kisu nilichotengeneza kwenye vitu mbalimbali, kipande cha mbao kilikatika mara moja, na taulo pia likachanika. Mafundi wengine wa kutengeneza visu katika kijiji chetu cha Husa walikubali ushindi wangu."
Miaka mia 6 iliyopita watu wa kabila la Waachang walioishi kwenye kijiji cha Husa walijifunza ufundi wa kutengeneza silaha kutoka kwa watu wa kabila la Wahan, wakavumbua ufundi maalumu wa kutengeneza visu. Visu hivyo vilipewa jina la kijiji hicho vikiitwa visu vya Husa. Waachang kizazi baada ya kizazi walipokezana ufundi huo katika karne kadhaa zilizopita.
Bingwa wa kutengeneza visu Bw. Xiang Laosai alipokuwa na umri wa miaka 14 alirithi shughuli za kutengeneza visu kutoka kwa baba yake, alikuwa mrithi wa kizazi cha tano cha familia hiyo iliyotegemea shughuli za kutengeneza visu. Ingawa Bw. Xiang Laosai hakupata elimu ya shule na hajui kusoma wala kuandika, lakini yeye ni mchapa kazi na hodari katika kujifunza. Ilimchukua kipindi kifupi tu kupata ufundi kamili wa kutengeneza visu. Alipokuwa na umri wa miaka 27 Bw. Xiang Laosai alianzisha duka moja la kutengeneza visu na kuendelea na juhudi katika shughuli hizo. Visu alivyotengeneza vina sifa nzuri zaidi na vina mtindo unaoambatana na mahitaji ya soko, kwa hiyo vinawavutia sana watu. Baada ya kushinda taji la bingwa wa kutengeneza visu, watu wengi zaidi walianza kununua visu vyake.
Bw. Xiang alisema "Mimi natengeneza visu kwa moyo wote. Ukifanya uzembe unashindwa kutengeneza visu bora. Wateja wakinunua visu, wanalipa fedha, iwapo visu vyenyewe si bora, ni aibu kwangu kuwauzia wateja. Kama visu vinavyotengenezwa na fundi fulani vinafanya kazi vizuri, basi ni kwa sababu fundi anavitengeneza kwa bidii bila uzembe."
Visu vina hadhi muhimu katika utamaduni wa China na historia yake. Katika zana za kale, Wachina walivitumia visu katika uwindaji na kilimo. Katika mapigano kati ya makabila mbalimbali, visu vilitumika kama silaha. Hivi sasa hakuna vita, watu wanavitumia visu kama mapambo ya nyumbani badala ya silaha, pia kuna watu wanaopenda kukusanya visu vya aina mbalimbali. Bw. Xiang Laosai anatengeneza aina zaidi ya 10 ya visu vya Husa, kama vile visu vinavyotumika katika maisha na visu vinavyotumika na wawindaji ili kujilinda. Kutokana na kuwa na sifa nzuri, visu vyake vinawavutia wateja wengi wanaoishi karibu na kijiji hicho, wakiwemo watu wa makabila mengine ya Wahan, Wadai, Wajingpo, Walisu na Watibet. Zaidi ya hayo visu anavyotengeneza vinauzwa nje ya China, katika nchi za Japan, Norway na nchi nyingine mbalimbali.
Bw. Xiang Laosai ana watoto watatu, anataka watoto wake warithi ufundi wake. Watoto wake pia wanavutiwa na ufundi wa kutengeneza visu. Mtoto wake mkubwa Xiang Changming amekuwa akijifunza kutoka kwa baba yake. Kijana huyo amepata msingi wa ufundi huo. Alisema "Natengeneza visu ndani ya nyumba, hata kama mvua kubwa ikinyesha, lakini niko nyumbani. Zamani nilikuwa nafanya shughuli za kilimo shambani, ilinibidi nivumilie jua kali. Sasa nafanya kazi nyumbani, ni rahisi zaidi."
Xiang Changfu ni mtoto wa pili wa Bw. Xiang, yeye anapenda kutafiti ufundi wa kutengeneza visu. Amemchukulia baba yeke kuwa ni mfano, na kutaka kueneza zaidi sifa ya visu vya Husa. Alisema "Huwezi kupita maisha yote hivi hivi tu, ni lazima upate ushindi. Lengo langu ni kutwaa taji la bingwa wa kutengeneza visu katika miaka 10 ijayo."
Idhaa ya kiswahili 2007-02-01
|