Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-08 15:31:04    
Mlinzi wa mpaka wa kabila la Wakyrgiz

cri

China na Kyrgizistan ni nchi jirani. Zaidi ya kilomita 100 za mpaka kati ya nchi hizo mbili zipo katika wilaya ya Tugumaiti ya mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Wauygur, kaskazini magharibi mwa China. Katika wilaya hiyo, mbali na wanajeshi wa China, watu wa kabila la Wakyrgiz pia wanashiriki kwenye shughuli za kulinda mpaka.

Bw. Wusiman ni mkazi wa kijiji cha Idaliang cha wilaya hiyo. Wakazi 9 wa kijiji hicho ni wanamgambo wanaolinda mpaka, Bw. Wusiman mwenye umri wa miaka zaidi ya 50 ni mkubwa zaidi kuliko wanamgambo wengine. Kazi yake ni kuwasaidia askari polisi kukagua eneo la mpaka ili kuzuia watu na mifugo isivuke mpaka. Bw. Wusiman alisema  "Tangu baba yangu, watu wa vizazi vitatu wa familia yangu ni walinzi wa mpaka. Hivi sasa ninamfundisha mtoto wangu kulinda mpaka."

Familia ya Bw. Wusiman imekuwa inajishughulisha na kulinda mpaka tokea miaka zaidi ya 50 iliyopita. Katika mpaka unaopita kwenye wilaya wanakoishi, kuna mabonde 22 na hali yenye utatanishi ya kijiografia. Kwa hiyo kuna desturi ambayo wanajeshi na wakazi wa huko kushirikiana katika ulinzi wa mpaka.

Bw. Wusiman alianza kuambatana na baba yake katika shughuli za kulinda mpaka alipokuwa na umri wa miaka 16. Alifanya doria katika bonde la Butmunaq lenye mwinuko wa mita karibu elfu 5 kutoka usawa wa bahari na hali mbaya ya mazingira. Hata katika majira ya siku za joto, halijoto ya huko ni nyuzi 20 chini ya sifuri. Bw. Wusiman amelinda bonde hilo kwa miaka 26.

Siku moja miaka 19 iliyopita, Wusiman na jamaa zake walipofanya doria mlimani, theluji kubwa ilianguka bila matarajio, watu 7 wa familia hiyo walipoteza njia na kuzungukwa na theluji. Baada ya siku ya tano walipokuwa wameshakata tamaa, walisikia sauti ya ndege. Mke wa Bw. Wusiman mama Wuer Ruqin alikumbusha akisema "Hatukutarajia kama serikali ingetuma helikopta ambayo ilituletea chakula pamoja na chakula cha mifugo. Tukanusurika."

Helikopita hiyo ilitumwa na jeshi kwa ajili ya kuwaokoa Wusiman na jamaa zake. Wusiman alisema baada ya tukio hilo alikuwa na nia imara zaidi ya kujishughulisha na kulinda mpaka. Alisema  "Naishukuru sana serikali. Kwa kutoa shukrani zangu ni lazima nifanye vizuri kazi ya kulinda mpaka hadi siku yangu ya mwisho."

Katika miezi ya Juni na Julai kila mwaka, Bw. Wusiman anakuwa na pilika pilika nyingi. Kwa sababu watu wengi wanakwenda kuchunga mifugo yao katika bonde analolinda, na ni rahisi kwa mifugo kuvuka mpaka. Bw. Wusiman anatumia mbinu mbalimbali ili kuwafanya wafugaji wafuate sheria kwa hiari.

Bonde la Butmunaq lina hali ya kijiografia yenye utatanishi na hali gumu ya mazingira, ni vigumu kwa binadamu kutembea huko. Kwa hiyo baadhi ya watu wanataka kuvuka mpaka kupitia bonde hilo. Adhuhuri ya siku moja, mwezi Mei mwaka 2005, Bw. Wusiman alikutana na wageni wawili alipokuwa njiani kurudi nyumbani. Kutokana na uzoefu wake, alitambua kuwa watu hao walitaka kuvuka mpaka. Wusiman alipanda farasi kwenda kwenye kituo cha polisi kutoa ripoti. Askari polisi walikwenda hadi kwenye bonde hilo na kufanikiwa kuwakamata watu hao waliojaribu kuvuka mpaka. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na ushirikiano kati ya Wusiman na askari polisi, wamefanikiwa kuwakamata watu 35.

Bw. Wusiman na askari polisi wamejenga urafiki mkubwa katika kazi. Askari polisi Bw. Yalikun alisema  "Kila tunapokumbwa na shida, mlinzi wetu wa mpaka Bw. Wusiman anatusaidia, tunaguswa sana hisia zetu."

Bw. Yalikun alikumbusha kuwa, siku moja alipokuwa kwenye doria alipata maumivu tumboni kiasi kwamba alitaka kuanguka kutoka kwa farasi. Bw. Wusiman na mlinzi mwingine wa mpaka walitembea kwa siku moja kumpeleka hospitali. Daktari alisema Yalikun alipaswa kufanyiwa upasuaji mara moja, kama asingepelekwa hospitali kwa wakati angekufa. Yalikun alisema maisha yake yaliokolewa na Wusiman.

Bw. Wusiman ana watoto watano. Mtoto wake mdogo hivi sasa pia anafanya kazi ya kulinda mpaka. Mtoto huyo alianza kufuatana na baba yake kufanya doria alipokuwa na umri wa miaka 6. Nchini China kabila la Wakyrgiz linajulikana kuwa ni kabila la walinzi wa mpaka. Wakyrgiz wanaona mlima ni baba na mto ni mama. Kwa hiyo wana hisia nzito kwa milima, mito, miti na maua ya taifa.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-08