Shirika la bima ya maisha la China, ambalo linachukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa miongoni mwa mashirika ya bima ya maisha nchini China, tarehe 9 mwezi Januari lilianza kuuza hisa zake kwenye soko la bima nchini China. Hii ni mara ya kwanza kwa shirika hilo kuuza hisa zake nchini China baada ya kuuza hisa zake kwenye masoko ya hisa ya Hong Kong na Marekani. Katika siku ya kwanza ya hisa kwa shirika hilo kuuza hisa zake, bei ya hisa za bima ya maisha ilipanda moja kwa moja na kuwa mara dufu mnamo saa za kufunga soko la hisa kwa siku hiyo. Hali hiyo inaonesha kuwa, wawekezaji wa China wanashauku kubwa kuhusu shirika hilo la bima kurudi nchini China kutoka kwenye masoko ya fedha ya nchi za nje.
"Saa 3 asubuhi ya tarehe 9 mwezi Januari, hisa za shirika la bima ya maisha la China zilianza kuuzwa rasmi kwenye soko la hisa la China lililoko mashariki mwa China. Shirika hilo ni shirika kubwa zaidi la bima ya maisha nchini China, ambalo ninachukua 40% ya bima ya maisha nchini China. Mwaka 2003, hisa za bima ya maisha ya shirika hilo la China zilianza kuuzwa kwa nyakati tofauti kwenye masoko ya hisa ya Hong Kong na Marekani, hivi sasa jumla ya thamani ya hisa za shirika hilo zilizouzwa kwenye masoko ya hisa inachukua nafasi ya kwanza duniani.
Safari hii shirika la bima ya maisha nchini China limenuia kuuza hisa bilioni 1.5 nchini China, ambapo jumla ya fedha zitakazokusanywa zitakuwa zaidi ya Yuan bilioni 28. Katika siku ya kuanza kuuzwa kwa hisa za shirika la bima ya maisha la China, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la bima Bw. Yang Chao alipohijiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, baada ya hisa za shirika la bima ya maisha la China kuuzwa nchini China, wawekezaji watanufaika sana. Alisema,
"Nafikiri hii ni nafasi moja nzuri sana kwa wawekezaji wa nchini. Baada ya hisa za shirika letu kufanikiwa kuuzwa kwenye soko, watu wengi wanaonunua hisa zetu, watakuwa wateja wetu, tena ninaamini kuwa wateja waliokata bima ya maisha kwenye shirika letu, watakuwa na hisa za shirika letu, ili kutimiza lengo la kuhimizana, kusaidiana na kunufaishana kwa pamoja."
Katika siku hiyo ya kuanza kuuzwa kwa hisa za bima ya maisha za shirika hilo, hisa za shirika hilo zilipendwa sana na wawekezaji, na zilifikia bei ya Yuan 38.9 wakati wa kufunga soko siku hiyo, ikilinganishwa na Bei ya Yuan 18.88 wakati wa asubuhi hisa za bima za shirika hilo zilipoanza kuuzwa, na kiasi cha upandaji bei kilifikia 106.2%.
Kiasi kikubwa cha kupanda kwa bei ya hisa za bima ya maisha ya shirika hilo la China kinaonesha imani kubwa ya wawekezaji kuhusu mustakabali mzuri wa soko kubwa la bima za maisha la nchini China. Kutokana na mpango wa maendeleo ya miaka mitano uliotolewa mwezi Oktoba mwaka jana, kamati ya usimamizi ya sekta bima ya China, pato la sekta ya bima ya China litafikia Yuan trilioni 1 ifikapo mwaka 2010, kiasi ambacho ni ongezeko la zaidi ya mara mbili kuliko lile la mwaka 2005.
Naibu mkurugenzi wa taasisi ya mambo ya fedha ya chuo kikuu cha umma cha China Bw. Zhao Xijun alisema, mbali na uwezo mkubwa wa soko la bima nchini China katika siku za baadaye, moja ya vyanzo vinavyowavutia wawekezaji ni hadhi bora ya shirika la bima ya maisha la China kwenye soko la bima nchini China. Alisema,
"Shirika la bima ya maisha la China likiwa ni uti wa mgongo wa sekta ya bima nchini China, watu wana matarajio makubwa na shirika hilo, shirika hilo limeonesha mafanikio na nafasi za maendeleo ya sekta ya bima ya China katika siku za baadaye."
Habari zinasema hisa za shirika la bima ya maisha la China ni hisa za kwanza za bima kwenye soko la hisa la nchini China. Si hivyo tu, kuuzwa kwa hisa zake kuna maana nyingine muhimu. Katika nusu ya pili ya mwaka jana, baadhi ya mashirika makubwa ya serikali ya China yakiwemo Benki ya China na Shirika la ndege la China, yalianza kuuza hisa zake kwenye soko la hisa la nchini China, vitendo ambavyo viliinua wimbi la mashirika ya China yaliyouza hisa zake kwenye masoko ya nchi za nje, yarudi kuuza hisa zake kwenye soko la hisa la nchini China. Kuuza hisa zake kwa shirika la bima ya maisha la China kwenye soko la hisa la Shanghai kumechangia kuinuka upya kwa wimbi hilo.
Hapo zamani, kutokana na udogo wa soko la hisa la nchini China na kuwa mfumo kimasoko wa uuzaji wa hisa ulikuwa bado uko katika kiwango cha chini, baadhi ya mashirika makubwa ya China yaliachangua kuuza hisa zake kwenye masoko ya fedha ya Hong Kong na Marekani, hali ambayo iliwaletea faida kubwa wawekezaji wa nchi za nje. Kutokana na kuvutiwa na kuboreka kwa hali ya soko la hisa na kuweko kwa fedha nyingi kwenye soko la nchini, kuanzia mwaka jana baadhi ya mashirika makubwa yaliyouza hisa zake kwenye masoko ya nchi za nje, yalirudi kuuza hisa zake kwenye soko la hisa la nchini, hatua ambayo inaleta furaha kubwa kwa soko la hisa la China linaloanza kuingia hali nzuri.
Habari zinasema kutokana na kuingia kwenye soko la hisa kwa mashirika hayo makubwa ya serikali, wawekezaji wa nchini China wataweza kunufaika kutokana na ongezeko la uchumi na ongezeko la thamani ya fedha za Renminbi na kuchangia utulivu na maendeleo ya soko la hisa la China. Jambo muhimu zaidi ni kuinua ubora wa kampuni zinazouza hisa zake katika soko la hisa la China na kuimarisha imani ya wawekezaji kuhusu soko la hisa la China.
Naibu mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa mambo ya fedha ya Chuo Kikuu cha Wananchi cha China Bw. Zhao Xijun alisema, mashirika makubwa ya serikali kurudi kuuza hisa zake katika soko la hisa la China itahimiza kupata fedha nyingi zaidi za kuwekezwa kwenye soko la hisa, na kubadilisha hali ambayo viwanda na kampuni zinaendesha shughuli zake kwa kutegemea mikopo ya benki.
Hata hivyo kurudi na kuuza hisa zake katika soko la nchini kwa mashirika makubwa ya serikali kumeleta shinikizo kwa soko la hisa la nchini, kwani fedha zinazokusanywa na mashirika hayo makubwa ni Yuan bilioni kadhaa au Yuan zaidi ya bilioni kumi. Bw. Zhao Xijun alisema, ukusanyaji fedha kwenye soko la nchini China bado lina uwezo mkubwa utakaotumika katika siku za baadaye, endapo uchumi wa China utadumisha maendeleo mazuri, ukusanyaji fedha wa mashirika makubwa ya serikali kwa njia ya kuuza hisa hautakuwa na tatizo lolote. Habari zinasema, mwaka 2007 kwa soko la hisa la China, ni mwaka ambao wawekezaji wa nchini China wana matarajio makubwa.
Idhaa ya kiswahili 02-13
|