China ni nchi yenye idadi ya watu bilioni 1.3. Kuanzia miaka ya 70 ya karne iliyopita, China ilianza kutekeleza sera ya uzazi wa mpango, kwa ajili ya kupunguza ongezeko kubwa la idadi ya watu. Ili kuhakikisha sera hiyo inatekelezwa vizuri kwa kuambatana na maisha ya wananchi, katika miaka ya karibuni, China ilifanya majaribio ya kuzipatia familia zinazofuata sera hiyo msaada wa pesa, na kuwaelekeza wananchi kutekeleza sera hiyo kwa hiari. Majaribio hayo yamepata mafanikio.
Bibi. Luo Cuian mwenye umri wa miaka 69 ambaye ni mzee wa kabila dogo mkoani Yunnan ana binti mmoja. Hivi sasa licha ya kupata pensheni pia anaweza kupata yuan 700 kwa mwaka, hivyo ana furaha kubwa.
"Hii ni sera nzuri, kila mwaka serikali inanipa yuan 700, na nimepata fedha hizo kwa miaka miwili."
Bibi. Luo anapata fedha hizo kutokana na China kutekeleza sera ya kuwapatia watu wanaofuata sera ya uzazi wa mpango msaada wa pesa katika baadhi ya sehemu za vijijini kuanzia mwaka 2004. Kwa mujibu wa sera hiyo, wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 ambao wana mtoto mmoja au mabinti wawili wanaweza kupata msaada wa fedha zisizopungua yuan 600 kwa mwaka.
Katika sehemu za vijijini, kutokana na kutokamilika kwa utaratibu wa huduma za jamii, maisha ya wazee yanategemea kimsingi watoto wao, hivyo wanavijiji wa China wanapenda kuzaa watoto wengi. Sera ya kuwapatia watu wanaofuata sera ya uzazi wa mpango msaada wa pesa imeondoa kwa kiasi fulani wasiwasi huo wa wananvijiji, na kuwasaidia kubadilisha wazo lao kuhusu uzazi.
Licha ya sera hiyo, China pia imeanzisha mradi wa "kuzaa watoto wachache ili kujitajirisha haraka" katika sehemu za magharibi. Mradi huo unazipatia familia zinazofuata kwa hiari sera ya uzazi wa mpango msaada mkubwa zaidi wa pesa. Wakati huo huo, serikali zinawasaidia watu watumie pesa hizo kufanya uzalishaji mali ukiwemo ufugaji wa ng'ombe na mbuzi ili kuwasaidia waboreshe maisha yao.
Sera ya kuwapatia watu wanaofuata sera ya uzazi wa mpango msaada wa fedha na mradi wa "kuzaa watoto wachache ili kujitajirisha haraka" vimepata mafanikio makubwa. Mkurugenzi wa kamati ya idadi ya watu na uzazi wa mpango wa China Bw. Zhang Weiqing alisema,
"Baada ya sera hizo kuanza kutekelezwa katika sehemu kadhaa, kwa ujumla wazee milioni 1.35 wenye umri zaidi ya miaka 60 ambao wanafuata sera ya uzazi wa mpango wamepata msaada wa fedha zisizopungua yua n600 kwa mwaka. Na katika sehemu za magharibi, familia laki 3 zimepata msaada wa fedha wa mradi wa 'kuzaa watoto wachache ili kujitajirisha haraka'."
Bw. Zhang pia amedokeza kuwa, wakulima wanafurahia sera hizo, na wanafuata sera hizo kwa hiari, katika sehemu kadhaa uzazi wa watu umepungua.
Kwa mujibu wa mpango, mwaka huu mradi wa "kuzaa watoto wachache ili kujitajirisha haraka" utaanza kutekelezwa katika sehemu zote za magharibi, na sera ya kuwapatia watu wanaofuata sera ya uzazi wa mpango pia itakamilika na kuanza kutekelezwa katika sehemu nyingi zaidi, fedha za kutekeleza sera hizo zimetolewa na idara za fedha.
Wataalamu wengi wa suala la idadi ya watu wanakubaliana na sera hizo mpya, na kuona kuwa sera hizo zinatoa mchango mkubwa. Sera hizo zinamaanisha kuwa njia ya kutekeleza sera ya uzazi wa mpango imebadilika. Naibu mkuu wa taasisi ya idadi ya watu katika chuo kikuu cha ualimu cha Yunan Prof. Luo Huasong alisema,
"Utekelezaji wa sera hizo umepunguza uzazi wa watu, ambapo ongezeko la idadi ya watu limedhibitiwa kwa ufanisi. Utaratibu wa kutekeleza sera hizo umebadilika, zamani China iliwalazimisha wananchi wafuate sera ya uzazi wa mpango, sasa watu wanafuata sera hizo kwa hiari."
Zamani China iliwalazimisha wananchi watekeleze sera ya uzazi wa mpango kwa kuwatoza faini watu wasiofuata sera hiyo, hivyo kazi ya kutekeleza sera hiyo ilikabiliwa na matatizo kadhaa. Baada ya China kuchukua hatua ya kuwapatia msaada wa fedha watu wanaofuata sera ya uzazi wa mpango msaada wa fedha, sera ya uzazi wa mpango inatekelezwa kwa njia mbili yaani kuwatoza faini watu wasiofuata sera hiyo na kuwapatia msaada watu wanaofuata sera hiyo, hivyo kazi hiyo inafuatilia zaidi maisha ya wananchi.
Licha ya sera hizo mbili, China pia itatekeleza kwa pamoja sera za uzazi wa mpango, huduma za jamii, elimu na msaada kwa watu wenye matatizo, na kuzinufaisha kwanza familia zinazofuata sera ya uzazi wa mpango. Pia China itachukua hatua kuhakikisha uwiano wa kijinsia, kulinda maslahi ya uzazi ya watu wanahamahama, na kuongoza uhamiaji wa watu.
Mkurugenzi wa kamati ya idadi ya watu na uzazi wa mpango ya China Bw. Zhang Weiqing anaona kuwa kutoa sera husika kwa kuelekeza utekelezaji wa sera ya uzazi wa mpango ni muhimu sana, alisema,
"Kuanzisha na kukamilisha sera ya uzazi wa mpango inayoongozwa na serikali kwa mujibu wa hali ya jamii ni njia muafaka ya kuwahimiza wakulima wafuate sera ya uzazi wa mpango kwa hiari, kudhibiti ongezeko kubwa la idadi ya watu vijijini; kutatua matatizo ya familia zinazofuata sera hiyo na kuondoa wasiwasi wao, pia ni hatua nzuri inayolinda usawa na haki katika jamii ya China."
Idhaa ya Kiswahili 2007-02-14
|