Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-19 19:40:35    
Sikukuu ya Spring ya China

cri

Tarehe 18 Februari ni sikukuu ya Spring ya China yaani sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China. Siku hiyo ni sikukuu kubwa kabisa kwa Wachina katika mwaka mzima ambayo ni kama siku ya Krismasi katika nchi za Magharibi. Ingawa namna ya kusherehekea sikukuu hiyo inabadilika kufuatana na jinsi jamii inavyoendelea, lakini nafasi muhimu ya sikukuu hiyo katika maisha ya Wachina haibadiliki.

Inasemekana kwamba hadi sasa Sikukuu ya Spring imekuwa ikisherehekewa kwa miaka elfu nne nchini China, lakini mwanzoni sikukuu hiyo haikuitwa sikukuu ya Spring na wala haikuwa na tarehe yake maalumu. Hadi miaka elfu mbili na mia moja iliyopita wahenga wa China walihesabu mwaka kwa mzunguko kamili wa sayari ya Jupita, sikukuu hiyo iliitwa sikukuu ya Jupita, na ilipofika miaka elfu moja iliyopita ndipo Wachina walipoanza kuita siku hiyo kwa "Sikukuu ya Spring".

Kutokana na mila na desturi ya Wachina sikukuu hiyo inaanzia tarehe 23 mwezi wa 12 kwa kalenda ya Kichina hadi tarehe 15 mwezi Januari yaani "sikukuu ya taa", jumla ni wiki tatu. Katika siku hizo za mwaka mpya, siku ya mwisho yaani tarehe 30 ya mkesha wa sikukuu na siku ya kwanza ya mwaka mpya ni siku za sherehe, au kwa maneno mengine siku hizi mbili ni kilele cha sikukuu ya Spring.

Ili kusherehekea sikukuu ya Spring, kuanzia mijini hadi vijijini watu huwa na pilikapilika za maadalizi. Huko vijijini wakulima hufanya usafi wa nyumba, na kutayarisha mahitaji ya mwaka mpya kwa kununua keki, peremende, nyama, vinywaji na matunda ili kutumia nyumbani na kukaribisha wageni. Katika miji maandalizi ya mwaka mpya yanaanza mapema zaidi, maduka na masoko ya kujihudumia hutayarisha vitu tele.

"Kukesha usiku" wa mkesha wa sikukuu ya Spring ni mila ya Wachina, kwa kawaida katika usiku huo jamaa hukusanyika na kula chakula pamoja, hali ambayo inaonekana kote nchini China. Jamaa hula chakula kwa pamoja na kuburudika hadi mapambazuko. Hapo kabla katika usiku huo watu walikuwa wanawasha fataki kusherehekea siku ya mwaka mpya. Kuwasha fataki kunatokana na mila na desturi zamani kwa maana ya kuwafukuza mashetani, lakini kutokana na usalama na uchafuzi wa mazingira desturi hiyo imepigwa marufuku katikati ya miji mikubwa, lakini vijijini kuwasha fataki ni sherehe ya lazima iliyokosekana. Wakati wa sikukuu halisi yaani siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza watu huvalia rasmi wakisubiri kutembelewa na wageni au kutoka kwenda kuwatembelea jamaa na marafiki. Katika siku za sikukuu ya Spring magulio hufanyika katika miji na vijijini, na kwenye magulio huwa kunakuwa na sherehe za aina mbalimbali za maonesho ya michezo.

Wakati wa sikukuu ya Spring, idara za utamaduni hushirikisha michezo ya sanaa. Kwa mfano, usiku wa kuamkia siku ya kwanza ya mwaka mpya vituo vya televisheni huonyesha michezo ya sherehe toka saa mbili za usiku hadi saa saba za usiku. Licha ya shamrashamra zinazofanyika kwenye magulio, katika miaka ya karibuni, kutokana na hali ya maisha ya Wachina kuinuka, watu wameanza kuisherehekea sikukuu hiyo kwa kutalii katika nchi za nje.

China ni nchi yenye makabila mengi, licha ya kabila la Wahan, kuna makabila mengine 55. Ingawa watu wa makabila tofauti wanaongea lugha tofauti na wanaishi na mila na desturi tofauti, lakini wote wanaichukulia sikukuu ya Spring kuwa ni sikukuu kubwa ya kabila lao.

Kutokana na mabadiliko ya maisha, watu wameanza kutumia simu za kawaida, simu za mkononi na hata mtandao wa internet kutumiana salaam za mwaka mpya wa Kichina.

Idhaa ya Kiswahili 2007-02-19