Mkutano wa taifa kuhusu teknolojia na sayansi uliofanyika kwa siku mbili, ulifungwa tarehe 30 mwezi Januari hapa Beijing. Habari kutoka kwenye mkutano zimesema, serikali ya China imeweka kipaumbele katika miradi 16 muhimu ya teknolojia na sayansi ukiwemo utafiti wa ndege kubwa, utafiti na matumizi ya raslimali za baharini na teknolojia ya nishati endelevu, na itatoa uungaji mkono mkubwa kwa utafiti wa miradi hiyo muhimu. Waziri wa sayansi na teknolojia wa China Bw. Xu Guanhua alisema, mwaka jana serikali ya China ilitenga fedha nyingi zaidi kuliko miaka ya nyuma katika utafiti na majaribio ya miradi ya sayansi na teknolojia, na maendeleo ya sayansi na teknolojia yamehimiza maendeleo ya uchumi na jamii ya China. Alisema,
"Takwimu ya mwanzo zinaonesha kuwa, fedha za utafiti na majaribio ya miradi ya sayansi na teknolojia zilizotolewa katika mwaka 2006 zilifikia Yuan bilioni 300 ikiwa ni ongezeko la 22% kuliko mwaka uliotangulia na zilichukua 1.4% ya pato la nchini la China. Kati ya fedha hizo, zile zilizotengwa katika bajeti ya taifa zilifikia Yuan bilioni 71.6. Baada ya jitihada za miaka mingi, sekta ya sayansi na teknolojia ya China ilipata maendeleo makubwa na imepunguza pengo lililopo kati ya China na nchi zilizoendelea."
Bw. Xu Guanhua alisema, pamoja na kuongezeka kwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya utafiti wa sayansi na teknolojia, utafiti wa kimsingi wa nchini China umepata maendeleo makubwa, na ubora wake umeinuka kwa kiwango kikubwa, yakiwa ni pamoja na mafanikio ya utafiti wa teknolojia muhimu za safari za chombo kinachobeba binadamu kwenye anga ya juu na kampuni za hali ya juu. Hivi sasa, maendeleo ya sayansi na teknolojia yameingia kwenye kipindi chenye mafanikio mengi. Kutokana na hali hiyo, serikali ya China imethibitisha mkazo unaowekwa katika utafiti wa sayansi na teknolojia wa mwaka 2007. Bw. Xu alisema, miradi muhimu 16 iliyothibitishwa katika mpango wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya China wa kipindi kirefu na cha wastani ukiwemo utafiti wa ndege kubwa, itapata maendeleo makubwa katika mwaka 2007.
Habari zinasema katika mpango wa maendeleo ya sayansi na teknolojia wa kipindi kirefu na cha wastani uliotolewa mwaka jana, serikali ya China imethibitisha miradi mikubwa ya sayansi na teknolojia inayotarajiwa kupata mafanikio makubwa katika miaka 15 ijayo, ikiwa ni pamoja na ya ndege kubwa, CMOS chip na software za utafiti za kiwango cha juu, utafutaji wa mafuta na utoaji wa gesi kwenye migodi ya makaa ya mawe, uoteshaji wa mbegu mpya za viumbe zinazoongezewa kwa gene za viumbe vingine, udhibiti wa maambukizi ya ukimwi na virusi vya ugonjwa wa maini, usafiri wa chombo cha anga kinachobeba binadamu na binadamu kutua na kufanya utafiti kwenye mwezi.
Bw. Xu Guanhua alisema, miradi muhimu ya taifa inayoendelezwa kwa kutumia teknolojia kubwa za kisasa na raslimali za taifa na kutakiwa kukamilishwa katika muda maalumu ili kuiwezesha China kutimiza malengo ya taifa. Utekelezaji wa miradi mikubwa ya taifa tangu China iasisiwe, ukiwemo mradi wa mpunga wa chotara, ilifanya kazi muhimu kwa uinuaji wa nguvu za taifa. Kwa hiyo, mwaka huu idara za sayansi na teknolojia za China zitaendeleza shughuli zake kwa kuzingatia miradi hiyo 16 mikubwa.
"Mkazo wa kazi za mwaka huu utawekwa katika uthibitishaji na maandalizi ya miradi hiyo mikubwa ili baadhi ya miradi hiyo iweze kuanzishwa ndani ya mwaka huu."
Aidha, mwaka huu, China itajenga maabra 10 za ngazi ya taifa na vituo vya utafiti vya ushirikiano wa kimataifa.
|