Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-22 19:05:17    
Watu wa nchi za kigeni washuhudia maendeleo ya mji wa Shijiazhuang

cri

Shijiazhuang ni mji mkuu wa mkoa wa Hebei, katikati ya China. Mji huu ulianzishwa na kuendelezwa kutokana na ujenzi wa reli. Katika miaka ya hivi karibuni, mji huo umewavutia wageni wengi kwenda kusoma, kufanya kazi na hata kuishi huko.

Bw. Maike Livingston mwenye umri wa miaka 28 anatoka Canada, alifika Shijiazhuang miaka miwili iliyopita. Hivi sasa anafanya kazi katika chuo cha upashanaji habari cha Hebei. Katika miaka miwili iliyopita, alishuhudia maendeleo makubwa ya mji huo. Bw. Livingston alisema "Nilifika mjini Shijiazhuang mwaka 2004, wakati huo mji huo ulikuwa ukipandwa miti mingi na kujengwa barabara pana zaidi, ambapo maduka makubwa pia yalijengwa. Shijiazhuang imenipa picha ya mji unaoendelezwa kwa haraka."

Mji wa Shijiazhuang upo katikati ya mkoa wa Hebei, ni kituo muhimu cha makutano ya reli na barabara kuu nchini China. Basi je, mji huo una umaalumu gani? Bw. Livingston alieleza maoni yake akisema "Niliwahi kutembelea miji mingi ya China, kama vile Beijing, Xian, Shanghai, Guangzhou na Shenzhen, kila mji unatofautiana na mwingine. Shijiazhuang ni mji mwenye umaalumu wake, ambao hauna historia ndefu kama miji ya Beijing na Xian, huu ni mji mpya, hapo awali kulikuwa na kijiji kimoja tu, kwenye mji huo naweza kushuhudia jinsi China inavyokua."

Huko Shijiazhuang, Bw. Livingston amepata marafiki wengi. Kabla ya kwenda kununua vitu, mwenye nyumba anayoishi anamwelekeza maduka yalipo na jinsi ya kufika. Akikumbwa na matatizo, majirani zake wanamsaidia, na alipoumwa marafiki zake wa China walimpeleka hospitalini. Marafiki hao pia walimfundisha lugha ya Kichina na kumwalika nyumbani. Kijana huyo wa Canada na marafiki zake wa China walipata furaha na kujenga urafiki mkubwa.

Bw. Osso ni mtaalamu wa uchumi kutoka Chad, amefanya kazi ya ualimu katika chuo kikuu kimoja mjini Shijiazhuang kwa miaka mitatu. Yeye na familia yake ya watu wanne wanaishi huko Shijiazhuang. Bw. Osso alisema "Kwa nini nilichagua mji wa Shijiazhuang? Kwa sababu hapa kuna hali nzuri ya hewa, watu wakarimu wanaopenda kusaidiana. Mji huo upo karibu na Beijing. Lakini Beijing ni mji mkubwa sana, Shijiazhuang ni mdogo zaidi. Hata hivyo kuishi kwenye mji mdogo kuna manufaa yake, ambapo ni rahisi kutatua masuala mengi. Kwa hiyo nimeamua kubaki hapa."

Bw. Osso alikumbusha kuwa siku ya kwanza alipofika kwenye mji wa Shijiazhuang, alipata msaada kutoka kwa wakazi wa huko. Alisema "Siku ya kwanza nilipofika Shijiazhuang, katika kituo cha garimoshi nilishindwa kupata taxi, askari polisi mmoja alikuja kunisaidia kupata taxi. Wakati huo sikuomba msaada kwake, lakini alifanya hiari kunisaidia. Wakazi wa mji huo ni wakarimu sana."

Mbali na wageni waliokwenda mjini Shijiazhuang katika miaka ya hivi karibuni kama Bw. Livingston na Bw. Osso, pia kuna wageni ambao wameishi mjini humo kwa miaka mingi. Wao wamezoea kabisa maisha ya hapa, katika mji huo wana shughuli, familia na marafiki, pia wana hisia nzito kwa mji huo. Wao wanauchukulia mji wa Shijiazhuang kama ni maskani yao ya pili. Bibi Wilma Sullivan ni Mwingereza anayefundisha lugha ya Kiingereza katika shule ya lugha za kigeni ya Shijiazhuang, ameishi katika mji huo kwa miaka 11. Alisema ameshuhudia maendeleo ya mji huo. Alisema "Mwanzoni nilipofika, mji huu ulikuwa na sura ambayo ni tofauti kabisa na ile ya sasa. Kulikuwa hakuna bustani wala uwanja wa mchezo wa golf, kulikuwa na mashamba tu. Nimeishi hapa mjini kwa miaka 11, nimeshuhudia maendeleo ya mji huu, jinsi ulivyokua na kustawi."

Bibi Sullivan alieleza kuwa, mkazi mmoja wa Shijiazhuang ni rafiki yake mkubwa, na urafiki wao umedumu kwa miaka 11. Bibi Sullivan anakwenda kumtembelea rafiki huyo nyumbani kwake mara kwa mara. Wao wanafanya mazungumzo pamoja na kwenda madukani kwa pamoja. Kila alipozungumzia urafiki huo, Bibi Sullivan alikuwa na furaha.

Mwezi Septemba mwaka 2006, Bibi Sullivan alipata tuzo ya urafiki ambayo inatolewa kila mwaka kwa wataalamu wa kigeni hodari wanaofanya kazi nchini China. Walimu wenzake wanaotoka nchi za kigeni za Marekani na Italia walimpongeza. Bibi Sullivan mwenyewe pia alifurahi sana, alisema tuzo hiyo ya urafiki aliyopewa na China ni tuzo kubwa kwake.