Mwaka 1996 wakulima zaidi ya 80 wa kijiji cha Lujiazhuang cha mji wa Baoding, mkoani Hebei walikwenda nchini Zambia kushiriki kwenye ujenzi wa mradi wa boma la kuzuia maji kwenye mto Zambezi, ujenzi huo ulifanyika kwa miaka miwili. Katika kipindi hicho wakulima hao waliona kuwa Zambia ilikuwa na mashamba mengi yenye rutuba ambayo hayakulimwa, hivyo waliingiwa na wazo la kubaki huko na kulima mashamba hayo. Mwaka 1998 wakulima hao walirudi China kuwachukua wanafamilia, marafiki na jamaa zao kwenda Zambia na kufanya makazi yao huko, hivyo "Kijiji cha kwanza cha Baoding" kilijengwa nchini Zambia, na mji wa Baoding unasifiwa kuwa ni "Kijiji cha Afrika".
Mtu aliyewaongoza wakulima hao kujenga "Kijiji cha Baoding" na kujiendeleza barani Afrika ni Bwana Liu Jianjun mwenye umri wa miaka 60, hivi sasa yeye ni mkuu wa tawi la Baoding la shirikisho la biashara kati ya China na Afrika. Alisema baada ya wakulima wa "kijiji cha Baoding" nchini Zambia kutajirika kwa kulima mashamba, wakulima wengi zaidi wa Baoding walivutiwa kwenda kwenye nchi za Afrika kulima mboga na mazao ya nafaka, baadhi yao pia wanajishughulisha na biashara, elimu, matibabu na usindikaji wa mazao ya kilimo. Hadi sasa vijiji 48 vya Baoding vimeanzishwa katika nchi zaidi ya 20 za Afrika na Asia, wakulima zaidi ya 7000 wanajiendeleza katika nchi za Afrika. Kwa kuwa wakulima wengi wa China waishio barani Afrika wanaweza kujenga nyumba, kutengeneza matofali na samani, wanasifiwa kuwa ni "wataalamu".
Wakulima wa Baoding wanakaribishwa na kupendwa na wenyeji wa nchi za Afrika, picha za video zimeonesha kuwa, katika baadhi ya nchi za Afrika magharibi wakulima wa Baoding walikaribishwa na wenyeji kwa shangwe, hata walialikwa kutembelea nyumbani kwa waziri wa ulinzi wa Cote d'Ivoire.
Bwana Peng Yijun mwenye umri wa miaka 48 ni mkuu wa "Kijiji cha Baoding" nchini Kenya. Mwaka 2000 alipofika nchini Kenya alikodi shamba la kulima mboga, nyanya, matango na maharagwe. Alisema kutokana na udongo wa huko kuwa na rutuba na hali nzuri ya hewa, mboga zinakua haraka hata hakuna haja ya kununua mbolea na dawa za kuua wadudu. Kwenye soko la Kenya nyanya zinauzwa kwa Shilingi 400 za Kenya kwa kilo moja, matango na kabichi ya kichina zinauzwa kwa shilingi 200 za Kenya kwa kilo, bei hiyo ni kubwa mara kadhaa kuliko ile ya chini China." Kutokana na kupanuka kwa shamba lake la mboga, Bw. Peng Yijun amewaajiri watu wenyeji wengi, na kuwafundisha namna ya kulima mboga.
Ilipofika mwaka 2003, Bwana Peng Yijun aliacha kulima mboga, na kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mishumaa. Hivi sasa kiwanda chake kina uwezo wa kutengeneza tani milioni 8 za mishumaa kwa mwaka, idadi ambayo imechukua nusu ya mishumaa inayouzwa nchini Kenya. Baada ya kuishi nchini Kenya kwa miaka kadhaa, Bw. Peng amefahamu namna ya kuishi kwa masikilizano na wenyeji na wazungu waishio humo, amefanikiwa katika biashara yake, na pia anajua kuongeza na wenyeji kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili."
Bw. Liu Jianjun alisema, uhusiano kati ya "Kijiji cha Baoding" na nchi za Afrika ni wa kunufaishana, licha ya kujiendeleza, "kijiji cha Baoding" pia kimeleta faida kubwa kwa nchi kinakoanzishwa, kama vile kuwafundisha wenyeji teknolojia ya kilimo, kutoa nafasi za ajira, mazao ya kilimo yaliyozalishwa na kijiji cha Baoding yametajirisha maisha ya wenyeji.
Bwana Liu Jianjun alisema ili kuhakikisha usalama, matibabu na elimu kwa watoto wa wanavijiji, shirikisho la biashara kati ya China na Afrika limesaini mkataba na vijiji vyote vya Baoding vilivyoko nchi za nje, yaani kila mwaka vijiji vya Baoding vinapaswa kutenga asilimia 10 ya faida zao kwa mfuko wa vijiji hivyo. Pia limetunga mkataba wa wanavijiji wa Baoding na utaratibu wa usimamizi wa vijiji vya Baoding vya nchi za nje ili kulinda haki na maslahi halali ya wanavijiji.
Hivi sasa wakazi wengi zaidi wa mji wa Baoding na wa sehemu nyingine nchini China wanatarajia Bw. Liu Jianjun atawatafutia fursa za kibiashara katika nchi za Afrika. Alisema nchi za Afrika zina fursa nyingi za uwekezaji, pendekezo lake kwa wachina wanaotarajia kuwekeza barani Afrika ni kwamba, kama akitaka kuwekeza Yuan laki mbili hadi laki tano, ni vizuri aendeshe mkahawa wa kichina, pia wanaweza kufungua duka la kuuzia bidhaa zinazotengenezwa nchini China, au kulima mazao ya kibiashara, kama akitaka kuwekeza Yuan milioni moja, basi anaweza kuanzisha kiwanda chenye kiwango kidogo cha kutengeneza matofali au kushona nguo. Bw. Liu Jianjun amesema, "kijiji cha Baoding" kina uhusiano mzuri na serikali za nchi za Afrika, hivyo ni rahisi kuyaunganisha makampuni ya China na serikali za nchi za Afrika.
Mbali na hayo kutokana na kuimarishwa kwa mawasiliano ya kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika, benki ya maendeleo ya China imeanzisha ofisi katika sehemu mbalimbali za Afrika mashariki, Afrika magharibi, kusini mwa Afrika na Afrika kaskazini, jambo hilo limewafanya wachina waishio barani Afrika kuomba mikopo kwa urahisi, na "kijiji cha Baoding" kinaweza kuyasaidia makampuni ya China kuomba mikopo.
|