Miezi kadhaa iliyopita, filamu ya China iitwayo "Korti Kwenye Mgongo wa Farasi" ilipata tuzo katika Tamasha la Filamu la Venice. Mwongoza filamu hiyo anaitwa Liu Jie, kabla ya hapo hakutegemea kama filamu hiyo ingepata tuzo katika tamasha hilo, kwani ni mara ya kwanza kuongoza kwake upigaji wa filamu .
Bw. Liu Jie ana umri wa miaka 38. Hapo awali alikuwa na tumaini la kuwa mchoraji. Alipokuwa mwanafunzi wa sekondari, kwa bahati alitazama filamu moja iliyoonesha hali ya maisha ya watu wa kaskazini magharibi mwa China. Mandhari nzuri ya kimaumbile na desturi ya maisha ya wenyeji wa huko ilimvutia sana, kwa hiyo alibadilisha nia yake ya awali na kutaka kuwa mpiga picha, na kweli baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Filamu cha Beijing na kujifunza upigaji picha.
Mwanzoni mwa karne iliyopita, wahitimu wa vyuo vikuu nchini China walikuwa wanapangiwa kazi na serikali, lakini Liu Jie hakupangiwa kazi katika studio ya filamu kama alivyotarajia, hata hivyo hakuacha nia yake, aliamua kuwa mpiga picha za filamu binafsi kwa kushirikiana na wengine. Wakati huo, kazi ya kupiga picha za filamu binafsi ilikuwa ni kazi ambayo haikuwepo kabla katika sekta ya filamu nchini China. Bw. Liu Jie alisema,
"Elimu niliyosomea katika chuo kikuu ni upigaji filamu, lakini kazi niliyopewa ilikuwa haina uhusiano wowote na elimu yangu, nilifadhaika, mwishowe niliamua kuwa mpiga filamu binafsi. Wakati huo kwa bahati nilimkuta mwongoza filamu mmoja aitwaye Wang Xiaoshuai ambaye aliacha kazi yake ya studio ya filamu, tulianza na kuendelea kushirikiana kupiga filamu binafsi kwa muda wa miaka zaidi ya kumi."
Bw. Liu Jie na mshirika wake Wang Xiaoshuai walipata umaarufu katika nyanja ya filamu kutokana na filamu iliyopigwa chini ya uongozi wao kuvutia watu kutokana na kueleza mambo ya watu wa kawaida kabisa.
Bw. Liu Jie alibahatika tu kuanza kuongoza filamu peke yake katika mwaka 2003 wakati ambapo alisafiri kikazi kwenda kwenye wilaya moja mkoani Yunnan. Wilaya hiyo ina milima na wenyeji walikuwa maskini. Ili kuwapunguzia gharama za shughuli za mashitaka na kwa ajili ya kueneza elimu ya sheria miongoni mwa wenyeji, mahakimu walikwenda huko kushughulika na kesi badala ya kusubiri mahakamani. Mahakimu hao wakiwa na nembo ya taifa mgongoni na farasi, walipita mlima hadi mlima, walisikiliza kesi pia walieneza elimu ya sheria kwa wenyeji. Hali hiyo iligusa sana hisia za Bw. Liu Jie, alikwenda huko hata mara sita ili kufahamu zaidi hali ilivyo ya maisha ya wenyeji, na kuamua kuonesha hali hiyo kwa njia ya filamu. Alisema,
"Naona ni fursa yangu nzuri ya kuonesha matatizo ya sheria yaliyopo kwenye ngazi ya chini katika jamii. Naamini kuwa filamu hiyo itasababisha watu watafakari. Hali niliyoonesha katika filamu yangu si kama tu ilitokea katika sehemu fulani, bali ni hali ya kawaida kote vijijini nchini China. Hivi sasa utekelezaji wa sheria ni mgumu. Hapo kabla kulikuwa hakuna mtu aliyeonesha hali hiyo."
Filamu ya "Korti Kwenye Mgongo wa Farasi" inaonesha hadithi ya mahakimu kadhaa kutekeleza kazi na kueneza sheria katika sehemu za milima. Kutokana na mada hiyo nzito wawekezaji hawakuwa na nia ya kuwekeza. Kutokana na uhaba wa fedha, alitoa fedha zake zote alizolimbikiza kwa ajili ya ndoa yake. Filamu ilipooneshwa ilivutia wasomi wengi, serikali na watu wa vyombo vya sheria, na ilipata tuzo katika Tamasha la Filamu la Venice. Bw. Liu Jie alisema,
"Pengine baadhi ya watazamaji wanaona mada ya filamu hiyo iko mbali nao, lakini wanasheria wanaofanya kazi katika sehemu hizo wanaielewa filamu hiyo kwa kina. Hali hiyo mbaya ya utekelezaji wa sheria ni lazima iondolewe wakati China inapojitahidi kujenga mfumo wa sheria na demokrasia."
Bw. Liu Jie alisema, filamu yake iliposhiriki kwenye Tamasha la Filamu la Venice hakuwa na matumaini makubwa kama filamu hiyo itashinda. Lakini waamuzi waliisifu sana na hadithi yenyewe iliwavutia na kuwafanya watafakari muundo wa jamii usio wa kawaida nchini China na kudadisi ni jinsi gani watu wa ngazi tofauti wanaweza kuishi pamoja katika jamii moja. Waamuzi walielewa fika mada ya filamu hiyo aliyokusudia.
Kutoka mpigaji picha hadi mwongoza filamu, Bw. Liu Jie ana moyo wa kawaida mbele ya mafanikio yake. Anaona kuwa hivi sasa filamu zinazoonesha hali ilivyo ya jamii ni chache sana, anatumai kuwa atatengeneza filamu nyingi kuhusu hali ya maisha ya watu wa kawaida na kuonesha utamu na uchungu wa Wachina wanapokuwa katika mabadiliko ya kihistoria.
Idhaa ya kiswahili 2007-03-05
|