Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-07 16:24:00    
China yavumbua simu ya mkononi inayotumia maandishi ya lugha za makabila madogo

cri

China ina idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.3, licha ya kabila la Wa-Han ambalo linachukua asilimia zaidi ya 90 ya idadi ya jumla ya watu wa China, bado kuna makabila 55 madogo, na makabila mengi madogo yana maandishi ya lugha zake. Katika miaka ya hivi karibuni simu za mkononi zimekuwa zikitumika sana nchini China, lakini simu zote za mkononi zinasanifiwa tu kwa maandishi ya lugha ya Kichina. Ili kukidhi mahitaji ya watu wa makabila madogo madogo wasiofahamu vizuri lugha ya Kichina, kampuni ya utafiti wa teknolojia ya kitarakimu ya Wangdao Xintong ya Beijing imefanikiwa kuvumbua simu ya mkononi inayotumia maandishi ya lugha mbalimbali za makabila madogo madogo.

Baadhi ya watu wa kabila la Wa-Uygur ambao hawaelewi vizuri lugha ya Kichina, hivi sasa wanaweza kutumia simu za mkononi kutumiana ujumbe kwa maandishi ya lugha yao. Simu hiyo ya mkononi ilivumbuliwa na kutengenezwa na kampuni ya Wangdao Xintong ya Beijing. Hivi sasa kampuni hiyo pia imefanikiwa kuvumbua simu nyingine za mkononi zinazotumia maandishi ya lugha 9 za makabila madogo madogo ambayo ni pamoja na lugha ya Kimongolia, Kitibet, Kikorea na Kihazak. Muda mfupi baadaye watu wa makabila hayo wataweza kutumia simu ya mkononi kwa maandishi ya lugha zao. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bwana Zhang Yan alipojulisha umaalum wa simu hiyo ya mkononi alisema:

"Kwanza kioo cha simu ya mkononi kinaonesha maandishi ya lugha ya kikabila, simu hiyo pia inaweza kutuma na kupokea ujumbe kwa maandishi ya lugha ya kikabila. Zaidi ya hayo simu hiyo imehifadhi ujumbe kadha wa kadha maalumu kwa maandishi ya lugha ya kikabila."

Hivi sasa idadi ya watu wa makabila madogo madogo nchini China imezidi milioni 100, asilimia 70 ya watu hao wanatumia maandishi ya lugha zao. Watu wa makabila madogo madogo wa China wamesambaa katika sehemu mbalimbali, kwa mfano wafugaji wengi wa kabila la Wamongolia wanapaswa kuondoka nyumbani kwa muda mrefu kwenda kutafuta malisho, hivyo inawafaa sana kutumia simu za mkononi kuwasiliana na nyumbani. Na kutuma ujumbe kuna ufanisi mzuri zaidi kuliko kuongea katika sehemu zisizokuwa na mawasiliano mazuri na kuwa na upepo mkali. Hivyo meneja mkuu Zhang Yan alisema, simu ya mkononi inayotumia maandishi ya lugha ya kikabila itakuwa na soko kubwa nchini China.

Katika miaka mitatu iliyopita, kampuni ya Wangdao Xintong iliwahi kushirikiana na makampuni mengine mawili kuvumbua simu ya mkononi inayotumia maandishi ya lugha ya Kiuygur, ambayo inapendwa sana na watu wa kabila la Wa-Uygur. Msichana Ajargul wa kabila la Uygur anayetumia simu hiyo ya mkononi alisema, simu hiyo ya mkononi imempa urahisi kuwasiliana na marafiki na jamaa zake. Alisema:

"Siku za zamani tulipaswa kutumiana ujumbe kwa maandishi ya Kichina, lakini lugha yangu ya kwanza si Kichina, na mimi nasoma katika shule ya kikabila, hivyo ni vigumu kueleza vizuri ujumbe wangu. Ni jambo la furaha kutumia simu ya mkononi kwa maandishi ya lugha ninayofahamu vizuri."

Baada ya simu ya mkononi inayotumia maandishi ya Kiuygur kuvumbuliwa, kampuni ya Wangdao Xintong inaendelea kutumia teknolojia hiyo kuvumbua simu nyingine za mkononi zinazotumia maandishi ya lugha 9 za makabila madogo madogo. Jambo hilo limesifiwa sana na wataalamu wa shirika la mawasiliano ya habari ya Kichina, walisema katika zama hizi za mawasiliano ya upashanaji wa habari, kuhimiza matumizi ya maandishi ya lugha za makabila madogo madogo kwenye mawasiliano ya upashanaji wa habari kumekuwa jukumu kubwa la serikali katika ngazi mbalimbali. Baada ya kufanya utafiti kwa miaka 20, kazi hiyo imepata maendeleo fulani. Mtaalamu wa shirika la mawasiliano ya upashanaji habari la Kichina Bwana Hua Shaohe alisema:

"China imepiga hatua kubwa katika kutumia software ya kompyuta iliyosanifiwa kutumia maandishi ya lugha ya makabila madogo madogo. Hivi sasa maandishi ya lugha nyingi za makabila madogo madogo ya China yanaweza kuandikwa kwenye kompyuta. Lakini hii ni mara ya kwanza kwa simu ya mkononi kutumia maandishi ya lugha za makabila madogo madogo."

Bwana Hua Shaohe anaona kuwa, kutumiana ujumbe kwa simu ya mkononi kwa maandishi ya lugha za makabila madogo madogo kutainua uwezo wa watu wa makabila madogo madogo kutumia maandishi ya lugha zao, kuhimiza urithi na maendeleo ya maandishi ya lugha za makabila madogo madogo.

Hivi sasa kampuni ya Wangdao Xintong iliyofanikiwa kuvumbua simu ya mkononi inayotumia maandishi ya lugha za makabila madogo madogo imeanza kushirikiana na makampuni kadhaa ya China yanayotengeneza simu za mkononi, huenda mwaka huu simu za mkononi zinazotumia maandishi ya lugha 9 za makabila madogo madogo zitapatikana kwenye soko la nchini China. Inasemekana kuwa kampuni ya TCL ambayo ni maarufu katika kutengeneza mitambo ya elektroniki ya nyumbani nchini China, imeanza kutengeneza simu za mkononi zinazotumia maandishi ya Kitibet, na zinatazamiwa kupatikana sokoni baada ya muda mfupi. Msichana wa kabila la Wahazak Janar alisema:

"Natumai kuwa simu ya mkononi inayotumia maandishi ya lugha ya kabila langu itapatikana haraka sokoni, na nitanunua simu moja ya namna hii."

Naye msichana wa kabila la Wamongolia Sharna alisema:

"Naona watu wengi wa kabila la Wamongolia watanunua simu ya mkononi inayotumia maandishi ya Kimongolia."

Imefahamika kuwa, hivi sasa maandishi ya lugha 19 za makabila madogo madogo yanatumiwa rasmi nchini China. Mkuu wa kampuni ya Wangdao Xintong alisema, katika siku zijazo kampuni hiyo itaendelea kuvumbua simu za mkononi zinazotumia maandishi ya lugha nyingine za makabila madogo.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-07