Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-08 18:36:35    
"Mama wa upendo" Reyhan Kasim

cri

Bi. Reyhan Kasim ni Profesa mdogo wa chuo kikuu cha mafuta cha mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur. Mwaka 1995 Bi. Reyhan Kasim aliyestaafu aliwakuta watoto wawili waliokamatwa kwa kuiba pesa kwenye soko la mboga, badala ya kuwalaumu watoto hao kama watu wengine walivyofanya, Bi. Reyhan aliwachukua kurudi nyumbani kwake, akawapatia nguo safi na chakula kitamu. Alipoambiwa kuwa watoto hao wawili walipaswa kuacha shule kutokana na familia zao zenye hali ya umaskini na waliiba pesa kwa ajili ya kujikimu, hisia zake ziliguswa sana. Alisema:

"Usiku huo mimi sikulala vizuri. Watoto hao ni lazima wapelekwe shuleni ili wapate mafunzo kama watoto wengine wa rika lao. Nadhani kuna watoto wengi wanaolazimika kuacha shule kutokana na sababu mbalimbali na kurandaranda mitaani, wanakosa upendo na kufanya shughuli haramu, mimi ni mama wa watoto, nawajibika kuwapatia watoto hao upendo wa mama."

Hivyo Bi. Reyhan aliamua kuwafundisha watoto hao wawili nyumbani kwake. Jambo lililomfurahisha ni kwamba watoto hao walizoea maisha mapya haraka na kuwa na hamu kubwa ya kusoma. Kuanzia hapo yeye aliwasaidia watoto wengi walioacha shule. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1995 hadi 1997, aliwapokea watoto 27 walioacha shule, aliwapatia chakula na malazi, hata kuwarudisha shuleni kwa kuwalipia karo. Kutokana na msaada wake, watoto hao si kama tu wameacha tabia mbaya, bali pia sasa wanapenda kusoma. Alifurahishwa na maendeleo ya watoto hao, alisema:

"Nataka kumpa kila mtoto upendo wangu, mimi ni mwalimu, hivyo nawajibika kuwafundisha watoto, kuwaelimisha na kuwaelekeza kutoka pande zote. "

Vitendo vya Bi. Reyhan Kasim vimewaathiri kina mama wengine, na idadi ya "mama wenye moyo wa upendo" wanaojitolea kuwasaidia watoto maskini imeongezeka siku hadi siku, na watoto wengi zaidi wenye matatizo ya kwenda shule wamesaidiwa.

Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2006, Bi. Rehyah na akina mama wengine wenye moyo wa upendo kwa ujumla waliwasaidia watoto zaidi ya 1000 kutoka familia maskini kuendelea na masomo kwa njia ya kuwasaidia karo ya shule na gharama za kimaisha.

Uzalnur ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya chini, baba yake alifariki dunia mapema, mama yake hana ajira, familia yake inaishi maisha magumu, kumgharamia yeye na dada zake wawili kwenda shule ni mzigo mkubwa kwa mama yake. Bi. Reyhan na akina mama wenye moyo wa upendo walipojua hali hiyo waliwapatia karo na vitu vya matumizi ya kila siku. Uzalnur alisema:

"Akina mama hao wenye moyo wa upendo walipojua matatizo ya familia yangu, walitupa karo ya shule, na kutusaidia kimaisha. Wakati wa kusherehekea mwaka mpya na sikukuu, wanatuletea nguo, mchele, unga wa ngano na mafuta. Mimi nawashukuru sana, sina la kufanya ila tu kusoma kwa bidii na kupata maendeleo kwenye elimu."

Licha ya watoto walioacha shule, wanafunzi wengi waliougua magonjwa makubwa pia walimwandikia Bi. Reyhan Kasim barua za kuomba msaada. Kutokana na takwimu zisizokamilika, Bi. Reyhan kwa nyakati tofauti aliwasaidia watoto 18 waliougua magonjwa makubwa kuchangisha gharama za matibabu.

Shughuli za Bi. Reyhan na mama wengine wenye moyo wa upendo wa kuwasaidia wanafunzi maskini zinajulikana na kufuatiliwa na jamii. Mwaka 2005, mfuko wa akina mama wenye moyo wa upendo ulianzishwa chini ya uungaji mkono wa shirikisho la ufadhili la mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur, watu wa fani mbalimbali walichangisha Yuan zaidi ya laki 3 kwa ajili ya mfuko huo.

Bi. Reyhan Kasim alisema, amefahamu thamani halisi ya maisha wakati wa kuwasaidia watoto maskini. Ni matumaini yake makubwa kuwa, watoto wote wenye matatizo ya kiuchumi watapata upendo wa mama. Alisema yeye amezeeka, lakini shughuli za kuwasaidia watoto wenye matatizo ya kiuchumi zitaendelea, anatumaini kuwa watu watapokezana moyo wa kuwafuatilia wengine kizazi hadi kizazi.