Mkoa wa Qinghai uko kwenye uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet, kaskazini magharibi mwa China. Ingawa mkoani humo kuna maliasili nyingi, lakini kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watu, na kutokuwa na hali nzuri ya mawasiliano, ukilinganishwa na sehemu zilizoendelea za mashariki mwa China, mkoa huo ni sehemu ambayo bado haijaendelea kiuchumi, na idadi ya watu maskini mkoani humo bado ni kubwa. Baada ya juhudi za miaka mingi, mkoa wa Qinghai umetafuta njia mpya ya kuwasaidia watu maskini kuendeleza shughuli za utengenezaji wa mazao ya kilimo, ili kuondokana na umaskini.
Baada ya China kuanza kutekeleza sera za mageuzi na ufunguaji mlango mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, kilimo na uchumi wa vijiji wa mkoa wa Qinghai ulipata maendeleo makubwa, maisha ya wakulima na wafugaji yaliboreshwa kidhahiri, na hali ya umaskini iliboreshwa kwa kiasi kikubwa. Lakini kutokana na kuwepo kwa hali mbaya ya mazingira ya kimaumbile, hali duni ya miundo mbinu, na aina moja tu ya muundo wa uchumi, tatizo la umaskini kwa wakulima na wafugaji bado linaonekana kidhahiri katika baadhi ya sehemu mkoani Qinghai. Mpaka sasa mkoani Qinghai kuna vijiji maskini zaidi ya 2,400, na kuna watu masikini zaidi ya milioni 1.19.
Naibu mkurugenzi wa ofisi ya kuwasaidia watu maskini na kujiendeleza ya mkoa wa Qinghai Bw. Song Weizhen Alipozungumzia suala la umaskini mkoani Qinghai alisema,
"Sehemu maskini ziko mbali na miji na hazina maendeleo ya kiuchumi, kuna vijiji vingi maskini, hivyo kuna kazi nyingi sana za kutoa misaada, na watu maskini wengi ni wa makabila madogomadogo."
Vijiji maskini na familia maskini vimeenea kote mkoani Qinghai. Vijiji hivyo vingi viko milimani, na mawasiliano ya vijiji hivyo si rahisi, hivyo kwa muda mrefu, wanavijiji wanaishi kwa kutegemea kilimo cha jadi.
Siku chache zilizopita, mwandishi wetu wa habari alikwenda kwenye kijiji cha Fanshen, karibu na mji wa Xining, mji mkuu wa mkoa wa Qinghai kufanya mahojiano. Wanavijiji wa huko walimwambia mwandishi wa habari kuwa, mimea inayopandwa kijijini kwao ni rape, ngano, viazi na kadhalika, na wakulima wanaishi kwa kuuza mazao ya mimea hiyo. Kama mavuno sio mazuri kutokana na maafa ya kimaumbile huwa hawapati mapato. Ili kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha, vijana na watu wenye nguvu kijijini wanafanya kazi nje ya kijiji, na wazee na watoto wanabaki kijijini.
Ofisa husika wa ofisi ya kuwasaidia watu maskini kujiendeleza ya wilaya ya Pin'an Bw. Jia Yongchun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa,
"Wilaya yetu ina vijiji 111, kati ya hivyo vina vijiji maskini 73, miongoni mwa vijiji hivyo, vijiji 60 ni vijiji vyenye mapato kidogo, na vijiji 13 ni vijiji maskini kabisa."
Alijulisha kwamba, kwa kuwa mapato ya mwaka kwa mtu hayajafikia Yuan za RMB 625, hivyo kijiji cha Fanshen kinachukuliwa kuwa ni kijiji maskini kabisa nchini China. Hivi sasa bado kuna vijiji zaidi ya 1,400 kama hicho mkoani Qinghai.
Zamani serikali ya huko ilitoa msaada kwa watu maskini tu, ingawa hatua hii iliwawezesha wanakijiji watatue tatizo la njaa, lakini haikuweza kuondoa tatizo la umaskini kihalisi. Katika miaka ya karibuni, mkoa wa Qinghai ulibadilisha mawazo ya zamani ya kuondoa umaskini, na kuendeleza shughuli za kilimo zenye umaalum za huko, ili kutoa fursa ya kazi na chanzo cha mapato kwa watu maskini. Mwandishi wa habari alifahamishwa kuwa, hivi sasa kufanya kazi katika vituo vya utengenezaji wa mazao ya kilimo ni moja ya vyanzo muhimu vya wakulima wa mkoa huo kupata fedha. Vituo hivyo vimeundwa mahsusi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuondoa umaskini, kila wanapokuwa na nafasi, wakulima wanakwenda huko kufanya kazi ili kupata pesa.
Katika kijiji cha Wanzi ambacho kiko karibu na kijiji cha Fanshen, mwandishi wa habari aliona kituo cha kufuma mablanketi yenye mtindo wa kitibet. Mhusika wa kituo hicho Bw. Wei Zhanyun alimwambia mwandishi wa habari kuwa, wafumaji wa huko wengi ni wanawake wenyeji wa kijiji hicho.
"Hivi sasa kituo hicho kina wafumaji 40, na mishahara yao kwa kawaida kila mwaka inafikia Yuan za RMB 3,000 hadi 4,000."
Kituo hicho ni kituo cha kiwanda cha ufumaji wa mablanketi katika kijiji cha Wanzi. Vina vituo vingi kama hicho mkoani Qinghai, ambavyo vinahusu sekta za ufumaji na usindikaji wa maziwa na nyinginezo. Serikali katika ngazi mbalimbali mkoani humo zinahimiza viwanda vya kutengeneza mazao ya kilimo kuanzisha vituo vya utengenezaji katika sehemu maskini, na kuwaajiri wakulima maskini kuwa nguvu kazi, ili kuwasaidia kuongeza mapato. Sasa mkoa wa Qinghai umeunda mfumo wa uzalishaji ili kuwasaidia wakulima maskini kuondoa umaskini, na bidhaa zinazotengenezwa na vituo hivyo sio tu zinauzwa nchini China, bali pia zinauzwa katika nchi za nje. Mablanketi yenye mtindo wa kitibet ni moja ya bidhaa zinazouzwa katika nchi za nje, kila mablanketi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 1 yakiuzwa watu 1600 wanaweza kusaidiwa kupata ajira.
Ili kuinua ufanisi wa utengenezaji, viwanda vya utengenezaji wa mazao ya kilimo vya huko pia vinatoa mafunzo kwa wakulima wa vituo hivyo. Tie Yuchun mwenye umri wa miaka 18 ni msichana kutoka kijijini, baada ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari, alikuwa anakaa nyumbani tu kutokana na kutokuwa na ajira. Hivi karibuni alipewa mafunzo ya kufuma mablanketi na kupata kazi anayoridhika nayo.
"Baada ya miezi mitatu ya mafunzo, tutatumwa katika vituo 16 vya ufumaji na kuwa wafanyakazi mafundi."
Viwanda vya utengenezaji wa mazao ya kilimo vinafanya kazi kubwa siku hadi siku mkoani Qinghai, ambavyo sio tu vinawasaidia watu kuongeza mapato yao, bali pia ni daraja la mawasiliano kati ya wakulima na masoko. Naibu mkuu wa taasisi ya sayansi ya jamii ya mkoa wa Qinghai Bw. Sun Faping alisema,
"Kuendeleza sekta za utengenezaji wa mazao ya kilimo na ufugaji, ni sehemu ya kuboresha kilimo na ufugaji wa jadi kwa kutumia dhana za uzalishaji na uendeshaji wa kisasa, ili kilimo na ufugaji viweze kupata nafasi nzuri zaidi kwenye masoko."
Bw. Sun Faping alisema, mkoa wa Qinghai una raslimali za nguvu kazi na maliasili ya kipekee, tatizo lililopo ni kupata masoko. Iwapo mkoa huo utakuwa na mawasiliano na masoko, wakulima na wafugaji maskini wataweza kutimiza maendeleo makubwa na kuondoa umaskini. Katika miaka ya hivi karibuni, kwa kupitia kazi ya kuwasaidia watu maskini kujiendeleza chini ya uongozi kwa mpango, mkoa wa Qinghai unatimiza mabadiliko makubwa ya kuwasaidia watu kuendeleza shughuli mbalimbali badala ya kuwapa msaada tu.
Imefahamika kuwa hivi sasa wakulima na wafugaji maskini laki 3 wameweza kuongeza mapato yao kutokana na uendelezaji wa sekta za mazao ya kilimo, na mapato yao yalifikia Yuan za RMB milioni 270, ambayo kila mkulima na mfugaji alipata ongezeko la Yuan za RMB 900.
Idhaa ya kiswahili 2007-03-13
|