Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-14 16:15:49    
Kabila la Wa-Tu wanavyosherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa jadi ya China

cri

Kijiji cha Wushi kiko katika wilaya inayojiendesha ya kabila la Wa-Tu ya mkoa wa Qinghai, kaskazini magharibi mwa China, kijiji hicho kina familia zaidi ya 160 ambazo ni za makabila matatu ya Wa-Tu, Wa-Han na Wa-Tibet, idadi kubwa ya watu wa kijiji hicho ni Wa-Tu. Katika miaka ya karibuni, kutokana na uongozi wa idara husika za serikali ya huko, kijiji cha Wushi kimepata mavuno makubwa ya kilimo cha mbegu za rapa, viazi na maharage aina ya broad bean, bidhaa zinazotengenezwa kutokana na mazao hayo zinasafirishwa hata nchi za nje. Maisha ya wanakijiji yamekuwa mazuri siku hadi siku, katika sikukuu ya mwaka mpya wa jadi, kijiji hicho huandaa shughuli za aina mbalimbali za kiutamaduni.

Sikukuu ya Spring na sikukuu ya Natrium ni sikukuu mbili kubwa kabisa kwa watu wa kabila la Wa-Tu, wanasherehekea sikukuu ya Spring kama watu wa kabila la Wa-Han. Kila inapowadia sikukuu ya Spring, Wa-Tu huimba nyimbo huku wakicheza ngoma, kwa watu wa kabila hilo kuimba nyimbo ni muhimu zaidi kuliko kula chakula, yaani kila siku ni lazima waimbe nyimbo, hata wakati wa kusherehekea sikukuu.

Kwenye ua wa jengo la kamati ya kijiji cha Wushi, wazee kadhaa walikusanyika pamoja, baadhi yao walipiga ala ya muziki aina ya Board Hu, wengine walipiga upatu huku wakipiga muziki wa kienyeji wa Qinghai. Katikati ya ua wanawake zaidi ya kumi wa kabila la Wa-Tu waliovalia mavazi maridadi ya kikabila walicheza ngoma ya jadi ya Yangge, huku watoto wakiwa wanarukaruka huku na huko kwa furaha.

Mama Wu Yuqin ana umri wa miaka 62, lakini anapocheza ngoma ya Yangge anaonekana kama ni mtu mwenye ukakamavu. Alisema:

"Hata katika siku za kawaida tunacheza ngoma ya Yangge na kuimba nyimbo, maisha yetu yamekuwa mazuri siku hadi siku, kucheza ngoma si kama tu kunatuburudisha sisi wenyewe, bali pia kunatusaidia kujenga afya."

Miongoni mwa wanawake waliocheza ngoma ya Yangge, kuna wasichana na wazee wenye umri wa miaka 60 hadi 70. Wachezaji hao walivaa vizibao vya rangi, kufunga utepe wenye rangi tano kiunoni, kuvaa viatu vinavyotariziwa kwa maua, na kushika vipepeo vyekundu mikononi, walicheza kwa nguvu wakifuata midondo ya muziki, kila mtu anaonekana na tabasamu ya furaha. Wanawake hao ni wa kikundi cha michezo ya sanaa cha kijiji cha Wushi, katika mkesha wa sikukuu ya Spring, walishiriki katika tamasha lililoandaliwa na serikali ya wilaya, kuanzia siku ya pili hadi siku ya 15 ya mwaka mpya wa jadi, wachezaji hao watafanya maonesho ya sanaa katika vijiji jirani kimoja baada ya kingine.

Mkuu wa kikundi cha michezo ya sanaa cha kijiji hicho anaitwa Liu Yinchun. Mzee Liu anajua mambo mengi kuhusu michezo ya sanaa ya jadi ya kienyeji, hasa anapenda kuimba opera ya kienyeji ya Qinghai aina ya Yuexuan, Yuexuan ni moja ya opera za kienyeji za Qinghai, mara nyingi huwa mchezaji mmoja anaimba na kuonesha wahusika kadhaa, opera aliyoimba mzee Liu huwa aliibuni mwenyewe. Alisema:

"Nawaongoza wanakijiji kuandaa shughuli za kiutamaduni kama vile kuiga muziki, kucheza ngoma na kuimba nyimbo. Watoto wangu wananitendea vizuri, hivyo naishi kwa furaha na napenda kuwashirikisha wazee wa kijijini kuimba nyimbo."

Familia ya mzee Liu ina watu 9, mtoto wake wa kwanza anafanya kazi katika kampuni ya ujenzi ya Xining, mji mkuu wa Qinghai, anarudi nyumbani mara mbili kwa mwezi. Mtoto wake wa pili Bwana Liu Xingui ni fundi seremala maarufu kijijini, ana ustadi mzuri wa kazi ya seremala, kila mwaka wakati wa mapumziko ya kilimo yeye hutoka nje pamoja na wanafunzi wake kufanya kazi ya useremala, na kurudi nyumbani na Yuan elfu kumi hivi. Bw. Liu XIngui alisema, kutokana na ongezeko la uchumi, hivi sasa maisha ya wanakijiji yamekuwa mazuri mwaka hadi mwaka. akisema:

"Hivi sasa tunaishi maisha mazuri, hata siku za kawaida tunaishi kama wakati wa kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya. Ni rahisi kununua pombe na sigara dukani, hivyo hatuna haja ya kufanya maandalizi mengi, wakija wageni sisi hununua vitu dukani."

Mzee Liu Yinchun alisema, watu wa kabila la Wa-Tu huanza kufanya usafi na kutenegneza chakula siku zaidi ya 20 kabla ya kuwadia kwa mwaka mpya. Katika mkesha wa mwaka mpya, watu wote wa familia hukusanyika pamoja, kubandika picha zenye michoro ya dragon, finiksi,, farasi na Yuanbao ya dhahabu kwenye madirisha na milango, pia kufanya sherehe ya "weisang", yaani kuelekea upande wa magharibi, kuchoma moto matawi ya mvinje, na udi tatu, kuomba baraka na kusahau huzuni au masikitiko yote ya mwaka uliopita. Mapema ya siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi, wanafamilia wote wanavaa mavazi mapya na kucheza mchezo wa kupiga kitu kama kimpira uani. Siku ya pili vijana huchukua jagi la pombe kuwatembelea wazee wa kila familia kuwapa salamu za mwaka mpya kwa pombe.

Mzee Liu Yinchun alisema, ingawa hivi sasa mila na desturi hizo za kusherehekea mwaka mpya wa jadi bado zinaendelea, lakini baadhi ya mila hizo zimebadilika kidogo. Kwa mfano hivi sasa kwenye siku ya kwanza ya mwaka mpya wanawake kwa wanaume, wazee kwa watoto wa kijijini hukusanyika pamoja katika ua wa kamati ya kijiji kufanya shughuli za kupeana salamu za mwaka mpya.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-14