Kutokana na maendeleo ya kasi ya utandawazi wa viwanda na miji nchini China, wakulima wengi wanakwenda mijini kufanya kazi za vibarua. Imefahamika kuwa, hivi sasa kati ya wakulima wapatao milioni 800 nchini China, wakulima karibu milioni 200 wanafanya kazi za vibarua mijini. Serikali ya China na jamii ya China zinawafuatilia sana wakulima hao, na zinafanya juhudi za kuhakikisha haki na maslahi yao halali yanalindwa.
Kwenye mahala pa ujenzi wa handaki la reli ya kasi mkoani Zhejiang, mashariki mwa China, mkulima Chen Qi anayefanya kazi ya kibarua huko alimwonesha mwandishi wa habari kadi yake ya mshahara. Alisema analipwa mshahara kwa mwezi kupitia benki kwenye akunti inayoambatana na kadi hiyo, sasa haitatokea tena kwa wasimamizi wa kandarasi kuwalipa wafanyakazi sehemu ya mshahara tu au kutowalipa kabisa. Pamoja na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanalipwa mshahara wanaostahili kwa wakati, kwa kutumia kadi hiyo pia ni rahisi kwa jamaa za wafanyakazi kutumia fedha hizo. Bw. Chen Qi alifahamisha kuwa "Mimi nachukua kadi na ninaacha kijitabu cha akiba nyumbani, kwa hiyo jamaa zangu wanaweza kutumia fedha hizo moja kwa moja."
Kusema kweli kadi hiyo ya mshahara imewasaidia wafanyakazi wa ujenzi ambao wengi ni wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini. Hapo awali kutokana na kukosa usimamizi wa lazima, baadhi ya watu waliopata kandarasi za ujenzi wakipata mishahara ya wafanyakazi walikuwa hawalipi wafanyakazi, hali hiyo iliwafanya wakulima wengi vibarua washindwe kupata pesa baada ya kuchapa kazi kwa mwaka mzima. Katika miaka miwili iliyopita, kutokana na uingiliaji kati wa serikali ya China, tatizo hilo limetatuliwa vizuri. Kampuni nyingi za ujenzi zilianza kutoa kadi za mishahara kwa wakulima wanaofanya kazi za ujenzi mijini, sasa wakulima hao wanalipwa moja kwa moja kwenye kadi hizo, hatua hiyo inawahakikishia wanalipwa mishahara wanazostahili kwa wakati.
Katika utatuzi wa tatizo hilo, mahakama za sehemu mbalimbali za China zimetilia mkazo kusikiliza kesi husika. Huko Shenyang, mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China, kilianzishwa kituo cha kwanza cha kulinda haki na maslahi ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini, kituo hicho kiliundwa na idara tisa za serikali zikiwemo mahakama na idara ya ajira na huduma za jamii. Katika kituo hicho kuna korti ya kutoa maamuzi kwa haraka, ambapo kesi zinazohusiana na haki na maslahi ya wakulima wanaofanya kazi mijini zinasikilizwa na kuamuliwa kwa haraka.
Hakimu mkuu wa korti hiyo Bw. Wei Xiaodong alifafanua lengo la kuanzishwa kwa korti hiyo kuwa ni kurahisisha utaratibu wa kusikiliza kesi, ili wakulima wapate mishahara wanayodai kwa haraka iwezekanavyo.
Hakimu Wei Xiaodong alisema "Tunajitahidi ili wakulima wanaofanya kazi mijini wapate mishahara wanayodai kabla ya kuondoka kutoka kwenye kituo chetu."
Kwa mujibu wa maamuzi ya serikali ya China, wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini ni watu wanaopewa kipaumbele kupata msaada wa kisheria. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2006 wakulima zaidi ya laki 1.2 wanaofanya kazi za vibarua mijini walipata huduma za msaada wa kisheria zilizotolewa na vyombo mbalimbali vya utoaji wa msaada wa kisheria nchini China, idadi hiyo iliongezeka kwa asilimia 65 kuliko mwaka 2005.
Mbali na hayo katika sehemu mbalimbali za China, unaanzishwa hatua kwa hatua mfumo wa kuhakikisha kuwa wakulima wanaofanya kazi mijini wanalipwa. Kutokana na mfumo huo, kampuni za ujenzi zinazofuatiliwa na zilizowahi kuchelewsha mishahara yao wafanyakazi zinapaswa kuweka dhamana ya fedha kwenye idara za ajira na huduma za jamii, kampuni hizo zikichelewa kuwalipa wafanyakazi wao, serikali itazitumia fedha hizo kulipa mishahara ya wafanyakazi.
Tatizo lingine linalowasumbua wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini nchini China ni huduma za jamii. Lakini hali ya kufurahisha ni kuwa, wakulima wengi zaidi wanalindwa na bima ya ajali kazini na bima ya matibabu. Bibi Li Dongmei ni mkulima anayefanya kazi za vibarua mjini Harbin, mkoani Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China. Miezi kadhaa iliyopita aliumia mkono wake wa kulia alipokuwa anafanya kazi kwenye mtambo. Mtoto wake bado anasoma na mama wa mume wake pia amelazwa hospitalini, Bibi Li alipaswa kulipa Yuan elfu 30 kwa upasuaji wa mkono wake, fedha hizo ni nyingi na alishindwa kumudu. Alisema "Wakati huo nilikuwa sijui la kufanya, kusema kweli kama nisingelindwa na bima ya ajali kazini, ningeshindwa kulipa gharama za matibabu."
Mwanamke huyo alieleza kuwa, kutokana na bima ya majeraha kazini, ajali hiyo haikuleta mzigo mkubwa kwa familia yake. Akipona ataendelea na kazi, hili ni jambo analotarajia kuliko mengine katika mwaka mpya.
Wakulima wanaofanya kazi mijini nchini China wana nguvu na moyo wa kuchapa kazi, lakini kutokana na kuwa na elimu ndogo, hawajui ufundi wa kikazi na ujuzi wa usalama kazini, kwa hiyo baadhi ya wakati wanakumbwa na ajali ambazo zingeepukika. Ili kukabiliana na hali hiyo, katika sehemu nyingi nchini China mafunzo kwa wafanyakazi hao yameongezwa.
Kutokana na mafunzo hayo, baadhi ya wakulima sasa ni mafundi hodari. Kijana Li Dongsheng kutoka mkoa wa Shandong ni mfano mzuri. Mwaka 2005 aliajiriwa na kampuni ya ujenzi ya Xintai kama fundi umeme. Baada ya kushiriki kwenye mafunzo ya ufundi wa kazi yaliyotolewa na kampuni hiyo, kijana huyo alipata hati ya kufanya kazi ya fundi umeme, na katika kipindi cha miaka miwili aliteuliwa kuwa mkuu wa mafundi umeme. Kijana huyo alisema "Sasa nina hati hiyo ya fundi umeme, pia naweza kupata ajira kwenye kampuni nyingine, hati hiyo ni sawa na uhakikisho wa kazi. Bila hati hiyo, waajiri hawawezi kuwa na imani kuhusu uwezo wangu, na sasa mimi mwenyewe pia ninajiamini zaidi."
Zaidi ya hayo kuna sera mbalimbali zinazowanufaisha wakulima wanaofanya kazi mijini nchini China. Kwa mfano awali watoto wa wakulima hao wakisoma kwenye shule za mijini, walipaswa kulipa ada za nyongeza, hivi sasa ada hizo zimefutwa. Idara za huduma za jamii za China pia zinajitahidi kutafuta bima ya uzee inayowafaa wakulima wanaofanya kazi mijini.
Wataalamu husika wanasema mbali na hatua hizo zilizotajwa, inapaswa kutunga sheria husika ili kutimiza lengo la kuhakikisha kuwa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini na wakazi wa mijini wanapata haki sawa.
Idhaa ya kiswahili 2007-03-15
|