Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-20 16:54:55    
China inafanya juhudi kupunguza tofauti ya mapato na kujenga jamii yenye masikilizano

cri

Kutokana na maendeleo ya uchumi wa China, mapato ya Wachina yamekuwa yakiongezeka haraka. Lakini wakati huohuo, tofauti ya mapato pia imekuwa ikiongezeka. Katika miaka ya hivi karibuni, suala hilo limekuwa linafuatiliwa na watu mbalimbali wa China, na limekuwa suala muhimu la kijamii ambalo linashughulikiwa na serikali ya China kwa makini. Katika kipindi cha leo, tutawaeleza zaidi hatua zinazochukuliwa na serikali ya China ambazo zinalenga kupunguza tofauti ya mapato.

Tangu mwishoni mwa miaka ya 70, kigezo cha Gini, ambacho kinaonesha tofauti ya mapato nchini China kimekuwa kinaongezeka. Takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia zinaonesha kuwa, katika miaka 30 iliyopita kigezo cha Gini nchini China kilikuwa 0.16, lakini mwaka 2005 kigezo hicho kilifikia karibu 0.47 kiwango ambacho kimepita mstari wa tahadhari. Miaka hiyo 30 ilikuwa ni kipindi ambacho uchumi wa China ulipata maendeleo ya kasi. Hii imeonesha kuwa tofauti ya mapato ilitokea wakati ambapo uchumi ulipata maendeleo makubwa na maisha ya wananchi yaliboreshwa.

Taasisi ya sayansi ya jamii inakadiria kuwa, mapato ya asilimia 2 ya watu wenye mapato makubwa ni mara 18 ya mapato ya watu wenye mapato madogo zaidi. Serikali ya China imetambua tatizo hilo, na inafanya juhudi kutafuta ufumbuzi. Tofauti ya mapato si kama tu ni tatizo la kiuchumi, bali pia ni suala la haki kwenye jamii, ambalo litaathiri mgawanyo wa mali na maendeleo endelevu ya uchumi.

Nchini China mapato ya wakulima ni madogo kuliko mapato ya wakazi wa mijini, hilo ni jambo la kawaida kabisa. Ili kupunguza tofauti kati ya mapato ya watu wanaoishi vijijini na mijini, kuanzia mwaka wa 2004 serikali ya China imekuwa inatumia fedha nyingi katika sehemu ya vijijini, na kuwasaidia wakulima kununua mbegu na mashine za kilimo za kisasa, ili kuwasaidia kuongeza mapato yao. Hatua hiyo imepata mafanikio. Mkulima wa kijiji cha Caiping cha mkoa wa Sichuan Bw. Zhou Ming alimwambia mwandishi wa habari kuwa, katika miaka ya hivi karibuni kutokana na msaada wa serikali, mapato ya wakulima wa kijiji hicho yanaongezeka mwaka hadi mwaka, na kiwango cha maisha ya watu kijijini hapo kimeinuliwa.

"Nina bwawa la hekta 0.13, naweza kupata Yuan elfu 5 kwa mwaka kutokana na ufugaji wa samaki, nina shamba lenye hekta 0.5, naweza kupata Yuan elfu 4 hadi elfu 5 kutokana na kilimo cha mpunga, aidha nafuga nguruwe wanne, naweza kupata Yuan elfu 3. Sasa naweza kununua pombe na sigara zenye sifa zaidi."

Kiwango cha maisha ya wakulima wengi kama Bw. Zhou Ming kinakaribia kiwango cha maisha ya watu wa mijini siku hadi siku. Katika sehemu kadhaa za vijijini, ongezeko la mapato ya wakulima ni kubwa kuliko hata wakazi wa mijini. Takwimu zilizotolewa na idara ya takwimu ya taifa ya China zinaonesha kuwa, mwaka 2006 wastani wa mapato ya kila mkulima kwa mwaka yalifikia Yuan 3,587, ambao uliongezeka kwa asilimia 10 kuliko mwaka 2005.

Aidha kuanzia mwaka huu serikali imefuta kero na ada za masomo isipokuwa ada za vitabu kwa wanafunzi wa elimu ya lazima wanaoishi vijijini, na kueneza utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano nchini kote kwa miaka mitatu. Hatua hizo zitapunguza matumizi ya fedha za wakulima kwa kiasi kubwa, na kuwapatia faida zaidi. Licha ya kupunguza tofauti kati ya mapato ya wakulima na wakazi wa mijini, suala la tofauti kati ya mapato ya wakazi wa mijini haliwezi kupuuzwa. Watu wenye matatizo makubwa ya kiuchumi wanafuatiliwa sana na serikali.

Bw. Yao Rugeng mwenye umri wa miaka 60 ni mmoja wa wakazi wenye matatizo ya kiuchumi. Yeye ni mlemavu, zamani alikuwa anafanya kazi kiwandani, lakini miaka kadhaa iliyopita kiwanda hicho kilifungwa. Bw. Yao alimwambia mwandishi wa habari kuwa, anaweza kupata pensheni ya Yuan 200 inayotolewa na serikali kila mwezi, na pia anaweza kupata faida mbalimbali.

"Serikali inarudisha gharama zote za mfumo wa joto nyumbani, yaani Yuan 1600 kwa mwaka. Kodi ya nyumba ni Yuan 130 kwa mwezi, serikali pia inarudisha pesa kadhaa, hivyo nahitaji kulipa Yuan 30 tu. Hivi karibuni nimepata kadi ya matibabu, nikienda hospitali nitanufaika na kadi hiyo, pia ada nyingi zimefutwa."

Licha ya kuwasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi kuongeza mapato yao, serikali pia inatilia maanani kuratibu mgawanyo wa mapato. Mwaka jana China ilibadilisha kanuni za kutoza kodi ya mapato, na sasa inatoza kodi mshahara unaozidi kiasi cha Yuan 1600, ambayo zamani ilikuwa ni kuanzia kiasi cha Yuan 800. Serikali pia imeongeza usimamizi wa kuwatoza kodi watu wenye mapato makubwa ili kuratibu mgawanyo wa mapato. Naibu mkuu wa idara kuu ya kodi ya taifa ya China Bw. Wang Li alieleza kuwa,

"Mwaka 2006 China ilibadilisha kanuni za kutoza kodi ya mapato na kutoza kodi mshahara unaozidi Yuan 1600 ambayo zamani ilikuwa ni Yuan 800. Takwimu zisizokamilika zinaonesha kuwa, China imepunguza watu milioni 20 wanaohitaji kutozwa kodi za mapato. Hatua hiyo inasaidia kulinda haki kwenye jamii, na kusukuma mbele ujenzi wa jamii yenye masikilizano."

Aidha serikali ya China na idara za umma pia zinachukua hatua kudhibiti ongezeko kubwa la mapato ya watu wenye mapato mengi. Takwimu zilizotolewa na Idara ya takwimu ya taifa ya China zinaonesha kuwa, hivi sasa mishahara ya wafanyakazi wa makampuni ya umeme na upashanaji habari ni mara 2 hadi mara 3 ya mishahara ya wafanyakazi wa sekta nyingine. Na kutokana na mapato ya ziada na huduma za jamii, tofauti halisi ya mapato huenda itakuwa kubwa zaidi. Mwezi Mei mwaka jana, viwanda vingi vya umeme vimetoa uamuzi wa kudhibiti mishahara. Kwa mfano kampuni ya mfumo wa umeme wa China iliyataka matawi ya kampuni hiyo yasitoe pesa nyingine mbali na mishahara. Mkurugenzi wa ofisi ya utafiti wa matumizi ya taasisi ya utafiti wa uchumi ya kamati ya maendeleo na mageuzi ya China Bibi. Chen Xinnian amesema, hatua hizo ni juhudi za China za kupunguza tofauti ya mapato.

"Hii inaonesha kuwa tunachukua hatua kuwasaidia watu wenye mapato kidogo, na kusimamisha ugawaji wa mapato. Utaratibu mzuri wa ugawaji wa mapato si kama tu unahitaji usimamizi, bali pia unahitaji watu wajizuie."

Ingawa China inafanya juhudi kubwa katika kupunguza tofauti ya mapato, na imepata maendeleo kadhaa, lakini kutokana na maendeleo yasiyo na uwiano katika sehemu mbalimbali nchini China, bado kuna tofauti kubwa ya mapato kati ya wakazi wa mijini na wa vijijini, wa sehemu na wa sekta mbalimbali. Mkurugenzi wa kamati ya maendeleo ya mageuzi ya taifa ya China Bw. Ma Kai alisema, China itaendelea kuchukua hatua kupunguza tofauti ya mapato, ili kusukuma mbele ujenzi wa jamii yenye masikilizano.

"Katika siku za baadaye China itachukua hatua kadhaa zikiwemo hatua za kiuchumi na kisheria ili kushughulikia vizuri uratibu wa ugawaji wa mapato. China itakamilisha mfumo wa huduma za jamii na kuwasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi kutatua matatizo yao, hasa watu maskini mijini na vijijini."