Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-28 15:50:01    
Mtaa wa Beijing wanakoishi wakazi wengi wa makabila madogo madogo

cri

Katika mtaa wa Hepingli Jiaotong ulioko kwenye sehemu ya mashariki ya Beijing, wanaishi wakazi wa makabila madogo madogo 29 wakiwemo kabila la Wa-mongolia, Wa-tibet, Wa-hui, Wa-zhuang na Wa-yi. Kamati ya usimamizi ya mtaa huo inaandaa shughuli moto moto za kusherehekea sikukuu za makabila yote madogo, na kila sikukuu ya kabila moja inaposherehekewa, wakazi wa makabila mengine hualikwa kushiriki ili wajiburudishe pamoja na kupata nafasi ya kufahamiana.

Mwaka 2001 baada ya jengo la makazi la shirika la uchapishaji wa habari la kamati ya China inayoshughulikia mambo ya makabila madogo madogo kukamilika, wafanyakazi wengi wa makabila madogo madogo wa kamati hiyo wamehamia kuishi kwenye mtaa huo. Ili kuimarisha mawasiliano kati ya wakazi wa mtaa huo, kamati ya usimamizi ya mtaa huo iliwahi kufanya shughuli za aina nyingi. Mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa mtaa huo Bwana Zhang Jian alisema:

"Mwanzoni tulifanya shughuli za burudani kama vile kucheza ngoma, kuimba nyimbo, kucheza chesi na karata. Lakini shughuli hizo haziwezi kuwavutia watu wengi. Hivyo shirika la wazee na kamati ya usimamizi ya mtaa ziliamua kufanya shughuli za kusherehekea sikukuu kwa wakazi wa makabila madogo madogo. Sikukuu ya kwanza iliyosherehekewa ni mwaka mpya wa kalenda ya kitibet, jambo hilo liliwafurahisha sana wakazi wa kabila la Wa-tibet na wakazi wa makabila mengine madogo madogo."

Katika sherehe hiyo wakazi wa kabila la Wa-tibet walitengeneza vyakula vya kitibet kwa ajili ya wakazi wengine wa mtaa huo walioshiriki nao, pia waliwapatia vitambaa vya Hada. Kuanzia hapo mtaa huo umekuwa na mazoea ya kusherehekea sikukuu ya kikabila kwa wakazi wa makabila madogo madogo. Mama Naren wa kabila la Wa-mongolia anashughulikia mambo ya kikabila kwenye shirika la wazee, alisema:

"Kuanzia mwaka 2003 tunafanya shughuli za kusherehekea sikukuu za kikabila kama vile mwaka mpya wa kabila la Watibet, sikukuu ya Nadamu ya kabila la Wa-mongolia, sikukuu ya Idi, na sikukuu ya Corban. Kwenye sherehe hizo wakazi wa mtaa huo wanawasiliana na kufahamiana, wanafanya mazungumzo, huku wakicheza ngoma na kuimba nyimbo, uhusiano kati ya wakazi umekuwa mzuri siku hadi siku."

Mkazi Shalima ni wa kabila la Wa-hazak, kabla ya kustaafu alikuwa anafanya kazi ya uhariri katika ofisi ya lugha ya Kihazak ya shirika la uchapishaji. Ameishi mjini Beijing kwa miongo kadhaa, alisema zamani familia yake ilisherehekea sikukuu ya Natrium ya kabila la Wa-hazak kwa kula chakula nyumbani tu, lakini tangu kamati ya usimamizi wa mtaa huo ianze utaratibu wa kusherehekea sikukuu za kikabila, maisha yao wakati wa sikukuu yamekuwa mazuri zaidi. Alisema:

"Sikukuu kuu ya kabila la Wa-hazak ni Natrium, kila mara sisi tunawaalika wakazi wa makabila mengine washerehekee sikukuu hiyo pamoja nasi. Tunavaa mavazi maridadi ya kikabila, tunawafahamisha wakazi wengine maana ya sikukuu yetu, halafu tunaanza kula chakula cha kikabila, kucheza ngoma na kuimba nyimbo."

Baada ya Bi Shalima kusema hivyo alianza kuimba wimbo wa kienyeji wa kabila la Wa-hazak uitwao "Macho makubwa ya kupendeza".

Katika shughuli za kusherehekea sikukuu za makabila madogo madogo, wakazi wa makabila madogo madogo waishio kwenye mtaa huo si kama tu wanaimba nyimbo, kucheza ngoma na kula vyakula vitamu kwa pamoja, bali pia wanaona wenyewe utamaduni na mila za makabila tofauti. Zaidi ya hayo mtaa huo pia unaandaa mihadhara mbalimbali kuhusu mambo ya makabila madogo madogo. Kwa kufanya hivyo wakazi wa makabila madogo madogo waishio mtaani humo wanafahamiana zaidi, na kuishi pamoja kwa masikilizano zaidi. Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa mtaa huo Bi. Zhang Yurong ni wa kabila la Wa-Han, mume wake ni wa kabila la Wa-Korea. Alijifunza ustadi wa kutengeneza mboga ya kimchi ambayo ni mboga ya jadi ya kabila la Korea. Kila akitengeneza mboga ya kimchi huwapatia majirani zake, na kusifia kuwa ni mboga ya urafiki. Alisema:

"Nafurahi kuishi pamoja na wakazi wa makabila madogo madogo mengine, kati ya familia 131 za jengo ninaloishi, familia 83 ni za makabila madogo madogo. Baada ya kuhamia kwenye jengo hilo, tulikuwa tumejifunza mambo mengi kuhusu desturi na mila za makabila mbalimbali. "

Sikukuu za makabila madogo madogo ya wahazak, wamongolia, watibet, wakorea, na wahui zinasherehekewa kila mwaka, na wakati wa kuwadia kwa sikukuu za kawaida kama vile siku ya walimu, siku ya wazee na sikukuu ya Spring, wakazi wa makabila mbalimbali waishio mtaani humo pia wanakusanyika pamoja na kusherehekea pamoja, hivi sasa wakazi wa mtaani humo wanaishi pamoja kama familia moja kubwa."

Idhaa ya kiswahili 2007-03-28