Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-09 15:15:28    
Mwongozaji wa filamu wa China Chen Daming

cri

Bw. Chen Daming aliyekuwa mwigizaji wa filamu nchini Marekani kwa miaka mingi, amerudi nyumbani China ili kutimiza ndoto yake ya kuwa mwongozaji wa filamu. Mwaka 2006 filamu ya "Mahangaiko ya Kutafuta Maisha" aliyoongoza upigaji wake, ilitingisha nyanja ya filamu.

Bw. Chen Daming alihitimu masomo yake mwaka 1988 katika Chuo Kikuu cha Filamu cha Beijing na alibaki chuoni hapo kuwa Mwalimu, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 24. Baada ya miaka miwili, aliona ni bora aendelee zaidi na masomo yake ingawa wakati huo alikuwa na fursa nyingi za kuigiza kwenye filamu. Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita aliacha kazi ya ualimu na kuweda Hollywood nchini Marekani akiwa anasoma na huku akijaribu kutafuta nafasi ya kuigiza kwenye filamu. Alikataliwa mara nyingi lakini mwishowe alipata nafasi ndogo katika filamu moja, mwanzo huo ulimpa moyo wa kujiamini. Alisema, kipindi alichokuwa Hollywood, kilimnufaisha sana katika maisha yake

"Huko Hollywood ushindani ulikuwa mkali, ambao ulinilazimisha nifanye kazi kikamilifu bila kukosea. Usipokuwa na nafasi ya kuigiza kwenye filamu unapaswa kwenda darasani, hivyo ndivyo iliyo Marekani kwa waigizaji wote, isipokuwa kama wewe ni mwigizaji nyota mkubwa kama Tom Cruise, kwa waigizaji wa kawaida ni lazima waende kutafuta tafuta nafasi za uigizaji, na ukipata nafasi hiyo ni lazima uigize vizuri. Hii ndio hali iliyonikuta nilipokuwa Hollywood, yaani ukifanya jambo, ni lazima ulikamilishe vizuri."

Bw. Chen Daming aliishi nchini Marekani na kuigiza kwenye filamu kwa miaka minane. Katika muda huo kutokana na juhudi zake alipata nafasi nyingi za kuigiza kadri muda ulivyopita na uigizaji wake ulikubalika. Aliwahi kuigiza filamu "Genhis Khan" aliyotengenezwa na Hollywood. Katika filamu hiyo alifanikiwa kuigiza kama shujaa Genhis Khan wa kabila la Mongolia la China aliyekuwa katika karne ya 12. Filamu hiyo iliwavutia sana watazamaji.

Lakini wakati huo ambapo Chen Daming alikuwa akielekea kwenye mafanikio ya uigizaji, alianza kutafakari mustakabali wake. Katika Shirika la Filamu la Hollywood waigizaji wa filamu kutoka Asia waliofanikiwa walikuwa wachache sana, na cha muhimu zaidi ni kuwa Chen Daming alitaka kuwa mwongozaji wa filamu na sio mwigizaji, ili aoneshe fikra zake mwenyewe kupitia filamu.

Alisema, "Nilipokuwa na umri wa miaka 30 hivi nilifikiri, nini nilichotaka maishani mwangu? Niwe Mwigizaji daima? Kwa kweli huko Hollywood wakati huo nilikuwa miongoni mwa waigiaji kutoka China waliofanikiwa kwa kiasi fulani, lakini nia yangu ni kuwa mwongozaji wa filamu na sio mwigizaji."

Mwaka 1998 alipotengeneza filamu nchini China aliona mabadiliko makubwa yametokea, akaamua kutimiza ndoto yake ya kuwa mwongozaji wa filamu katika nchi yake China. Aliandika mwongozo wa Filamu na kuwa mwongozaji wa filamu hiyo. Jina la filamu hiyo inaitwa "Mwanamke Kamili"/ Filamu hiyo inaeleza, mfungwa mmoja aliyekuwa gerezani kwa miaka minane alitamani kkuwoa mchumba wake wa zamani, lakini alipotoka gerezani alimwona mtu aliyekuja kumpokea alikuwa amebadilika kabisa ambaye sio kabisa kama mchumba wake wa zamani aliyekuwa mpole. Filamu hiyo ilipata tuzo katika mashindano ya kimataifa ya filamu mara nyingi na kusifiwa na wataalamu wa filamu. Ufanisi huo ulimfurahisha sana Chen Daming.

Alisema, "Mimi niliandika mwongozo wa filamu hiyo na ni mimi mwenyewe niliuhariri. Nilipoandika mwongozo niliona uhuru kabisa wa kujiamulia namna ya kuandika, na nilipoandika kwenye sehemu ya msisimko niliona raha isiyo ya kawaida, na nilipokuwa naongoza upigaji wa filamu hiyo niliona furaha ya aina nyingine ya kushirikiana na wenzangu."

Mwaka 2006 Chen Daming alitengeneza filamu yake nyingine ya "Mahangaiko ya Kutafuta Maisha". Hii ni hadithi iliyotokea katika mji wa kaifeng nchini China ambao pia ni mji alikoishi na alikokulia, ikieleza wachezaji watatu wa opera ya Yu waliopongeza kazi jinsi walivyojitahidi kupata ajira na kusababisha vicheko vingi. Utengenezaji wa filamu hiyo haukutumia fedha nyingi, lakini inawavutia sana watazamaji. Vyombo vya habari viliisifu filamu hiyo kuwa ni nzuri yenye gharama ndogo. Filamu hiyo iliwahi kuoneshwa mara nyingi katika mashindano ya kimataifa ya filamu, na ilinunuliwa na Israel. Bw. Chen Daming alisema, filamu hiyo imewasilisha fikra zake kuhusu filamu.

"Napenda kutengeneza filamu ya kuchekesha, kwani maisha ya binadamu huwa na furaha na huzuni, kwa hiyo filamu yangu huwafnya watazamaji wawe na vicheko na machozi. Filamu ya "Mahangaiko ya Kutafuta Maisha" ni jaribio langu la filamu ya aina hiyo."

Bw. Chen Daming alipoulizwa maoni yake kuhusu haliya sasa na ya baadaye ya soko la filamu nchini China, hakujibu ila alitabasamu tu. Alisema amejifunza mengi katika kazi yake ikiwa ni pamoja na kuraha na ushirikiano. Alisema, ataendelea kutengeneza filamu, ili kuonesha maisha ya aina mbalimbali ya binadamu.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-09