Siku chache zilizopita mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Tanzania Bi. Anna Abdallah na ujumbe wake wa watu sita walikuwepo nchini China kwa ziara ya mafunzo, ziara iliyoanza tarehe 19 hadi tarehe 29 mwezi march. Katika ziara hiyo Bi Anna Abdalah alipata nafasi ya kuongea na Radio China Kimataifa ambapo alieleza kuhusu uhusiano uliopo kati ya wanawake wa China na Tanzania.
Kuhusu uhusiano kati wanawake wa China na Tanzania Bi Anna alisema, "Ushirikiano kati ya wanawake wa China na Tanzania ulianza mara tu baada ya uhuru wa Tanzania na tangu wakati huo hadi hivi sasa tumeshafanya mambo mbalimbali" Zamani ushirikiano kati wanawake wa China na Tanzania ulitilia mkazo zaidi namna ya kuwasaidia kuwasomesha wasichana wa kitanzania hasa katika maeneo ambayo ilikuwa vigumu kwa wasichana wa kitanzania kupata nafasi ya kusomea, kwa mfano taaluma ya udaktari. Kwa kupitia ushirikiano wasichana wengi walipata nafasi ya kuja nchini China kwa masomo na walisaidiwa kujiandaa ili kuweza kushika madaraka mbalimbali nchini mwao. Wakati huo serikali ya China ilikuwa inatoa nafasi za masomo kwa Watanzania wake kwa waume lakini licha ya nafasi hizo umoja wa wanawake wenyewe ulipewa nafasi zake maalum kwa ajili ya wanawake.
Bi Anna amesema kuwa umoja wa wanawake wa china umekuwa ukiwasaidia sana wanawake wa Tanzania, kwa mfano waliwahi kuvisaidia vikundi vya wanawake vya ushonaji masaada wa vyerehani, wamewahi kusaidia uboreshaji wa shughuli za mikono ya kina mama.
Mwaka 2006 shirikisho la wanawake wa China lilituma ujumbe nchini Tanzania ambapo pia walituleta vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya ofisi kama computer na printer zake, mashine za kurudufu na baiskeli ambapo baiskeli ziligawiwa kwa makatibu wa umoja wa wanawake wa kila wilaya. Katika ziara hiyo tuliwatembeza katika matawi yetu ambapo waliona shughuli mbalimbali zinazofanywa na umoja wetu, na baada ya ziara waliona kuna umuhimu wa kuzidisha zaidi ushirikiano ambapo pia walitualika kuzuru nchini China.
Pia tuliwatembeza katika shule za chekechea zilizopo katika jamii za kimasai huko Arusha ambapo tuliwaonesha jinsi serikali inavyowahamasisha vijana kuanza shule ambapo katika jamii nyingi za kimasai za wafugaji, hili limekuwa tatizo gumu hasa kwa watoto wa kike. Na katika ziara yetu wametupa vifaa mbalimbali vya shule ya chekechea kama vile mipira, kalamu, vifutio na vifaa vya kutengenezea madawati, na vifaa hivyo watavisafirisha wenyewe.
Akieleza ni mambo gani ambayo wamejifunza katika ziara yao nchini China, Bi Anna Abdalah alisema kuwa, wamejifunza sana kuhusu wanawake wajasiriamali jinsi wanavyofanya shughuli zao, kwa sababu wanawake wajasiriamali wa Tanzania wanafanya shughuli ndogondogo tofauti na ilivyo China ingawa wapo wengine ambao wanafanya biashara za kati au za juu wakisafiri kuja China kununua bidhaa au kwenda Dubai. Na jambo la msingi kabisa walilojifunza ni jinsi ya kuwaunganisha wajasiriamali hao, ili wawe na umoja mkubwa, ili kama mtu anataka kuagiza bidhaa kutoka China isiwepo haja ya kuja China kununua bidhaa bali mjasiria mali anaweza kutumia mawasiliano ya internet au kuwasiliana na wajasiriamali wa china ili kuweza biashara nzuri kabisa.
Katika ziara hiyo ambapo pia walitembelea viwanda vya wanawake waliosaidiwa na shirikisho la wanawake wa China, waliomba msaada wa kuwasaidia wanawake wa Tanzania wanaotengeneza bidhaa ndogondogo ili ziwe na ubora utakaozifanya zipate masoko kwa urahisi.
Alimalizia kwa kusema, wanawake wajasiriamali wa China wameonesha nia ya kwenda kuwekeza nchini Tanzania ambapo wamewaomba kuwekeza katika shughuli zinazofanywa na wanawake.
|