Karibuni katika kipindi cha elimu na afya. Katika miaka ya hivi karibuni, matatizo ya kupata matibabu na gharama kubwa za matibabu yamekuwa moja ya masuala yanayowasumbua wananchi wa China. Matatizo hayo yanaonekana wazi zaidi kwenye sehemu za vijijini zilizo nyuma kiuchumi. Ili kuinua kiwango cha matibabu kwenye sehemu hizo, mwaka 2003, China ilianza kutekeleza kwa majaribio utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano kwenye sehemu kadhaa, na manufaa ya utaratibu huo yameanza kuonekana. Kwenye mkutano wa mwaka wa baraza la mashauriano ya kisiasa ya China uliofanyika hivi karibuni, suala hilo lilifuatiliwa sana mkutanoni.
Kwenye sehemu za vijijini zilizo nyuma kiuchumi nchini China, kupatwa magonjwa ni jambo la kutisha kwa kuwa watu wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu, na hata kama wana fedha za kutosha, pia hawezi kupata matibabu mwafaka na yenye ufanisi kutokana na kiwango cha chini cha matibabu cha huko. Mjumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa Bw. Shi Xinmin anayetoka mkoa wa Shanxi anafahamu matatizo ya matibabu yanayowakabili wakulima. Alisema:
"Natoka kwenye sehemu ya vijijini na kila mwezi ninarudi kwenye maskani yangu. Wakazi wengi wakipatwa na magonjwa makubwa hawapati matibabu kwa kuwa hawana uwezo wa kumudu gharama za juu. Hata kama wakiwa na magonjwa ya kawaida, hawapati matibabu. Kutokana na upungufu wa vifaa vya matibabu, upimaji mbalimbali wa kimatibabu haufanyiki. Wagonjwa wengi wanapoamua kwenda hospitali, magonjwa yanakuwa yamefikia kipindi cha mwisho. Hii ni hali ya kawaida kwenye sehemu za vijijini."
Bw. Shi Xinmin anaona kuwa, baada ya kutatuliwa kwa tatizo la chakula na mavazi, tatizo la kupata matibabu limekuwa tatizo halisi linalowakabili wakulima wa China. Lakini Bw. Shi Xinmin alisema, tatizo hilo limepunguzwa kiasi.
Hivi sasa njia ya kutekeleza utaratibu mpya wa ushirikiano wa matibabu nchini China ni kuwa, serikali kuu na serikali za mitaa zinatoa Yuan 20 kwa kila mkulima, na kila mkulima pia anachangia Yuan 10. Mfuko huo unatumiwa kutoa ruzuku kwa wakulima wanaopewa matibabu. Bw. Shi Xinmin ametambua kuwa, tangu mwaka jana utaratibu huo ulipoanza kutekelezwa kwa jaribio katika maskani yake, wakulima wengi zaidi wanakwenda kwenye hospitali za tarafa na za wilaya kupata matibabu. Bw. Shi Xinmin alisema:
"wakulima ninaowafahamu wote wanasema kuwa utaratibu wa ushirikiano wa matibabu ni mzuri."
Mjumbe mwengine wa baraza la mashauriano ya kisiasa Profesa Hou Shuxun ambaye ni daktari, anafuatilia sana utaratibu huo mpya. Alisema:
"kwenye sehemu za vijijini ambazo kiwango cha matibabu kiko nyuma, utaratibu huo unaweza kutoa uhakikisho wa kimsingi wa matibabu kwa wakulima walioshiriki kwenye utaratibu huo, na kuhakikisha kuwa wanapewa matibabu kwa wakati kama wakipatwa na magonjwa. Kama wakiwa na magonjwa sugu, utaratibu huo pia utasaidia kupunguza mzigo kwa familia yao. Hivi sasa uchumi wa sehemu za vijijini za China bado uko nyuma, katika hali hiyo, nadhani kwamba utaratibu huo ni ufumbuzi mzuri."
Imefahamika kuwa hadi kufikia mwezi Septemba mwaka 2006, nusu ya wilaya na miji ya China imeanza kutekeleza kwa majaribio utaratibu mpya ya matibabu ya ushirikiano, na watu zaidi ya milioni 400 wananufaika na utaratibu huo. Ripoti ya kazi ya serikali iliyotolewa na Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao kwenye mkutano wa mwaka wa bunge la umma la China inasema kuwa, mwaka huu China itapanua zaidi eneo la utekelezaji wa majaribio wa utaratibu huo. Bw. Wen Jiabao alisema:
"mwaka huu China itajitahidi kueneza utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano, na kupanua eneo la utekelezaji kwa majaribio kwenye asilimia 80 ya wilaya na miji kote nchini China. Serikali kuu itatenga Yuan bilioni 10.1, likiwa ni ongezeko la Yuan bilioni 5.8 kuliko mwaka jana."
Mjumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa Bw. Zhu Qingsheng aliwahi kuwa naibu waziri wa afya ya China, anaukubali uamuzi wa serikali kueneza utaratibu huo. Bw. Zhu Qingsheng alisema:
"waziri mkuu Bw. Wen Jiabao alipozungumzia utaratibu huo alisema, mwaka huu utekelezaji wa utaratibu huo utapanuliwa kwenye asilimia 80 ya wilaya na miji kote nchini China, yaani tumetimiza lengo la kueneza utaratibu huo kote nchini mwaka mmoja mapema kuliko mpango uliowekwa. Nadhani kuwa serikali imeongeza nguvu katika kazi ya kuondoa tatizo la kupata matibabu kwa wakulima."
Bw. Zhu Qingsheng alisema, wajumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa wanafuatilia sana hali ya matibabu kwenye sehemu za vijijini, walifanya uchunguzi mara nyingi kuhusu hali ya utekelezaji wa utaratibu huo mpya na walitoa mapendekezo mbalimbali. Bw. Zhu Qingsheng anaona kuwa, kauli ya Bw. Wen Jiabao kuhusu utaratibu huo si kama tu inaonesha kuwa serikali ya China inafuatilia hali ya maisha ya wananchi, bali pia imeonesha kuwa serikali inasifu mafanikio yaliyopatikana katika mashauriano ya kisiasa. Hali hiyo imewatia moyo zaidi wajumbe wa baraza hilo. Mbali na kusifu mafanikio ya utaratibu huo, wajumbe hao pia wanatoa mapendekezo mbalimbali ya kukamilisha utaratibu huo. Mjumbe Bw. Zhang Xuemei anayetoka mkoa wa Fujian alisema, anapenda utaratibu ukamilike zaidi katika shughuli za usimamizi wa fedha na kiwango cha matibabu, ili kuwahudumia wakulima vizuri zaidi. Bw. Zhang Xuemei alisema:
"serikali katika ngazi mbalimbali zinapaswa kuanzisha mfuko maalum na kuuweka kwenye bajeti ya fedha ya mwaka, vituo vya afya vya wilaya na tafara vinapaswa kuinua kiwango cha huduma na kupunguza gharama za matibabu; serikali zinapaswa kuanzisha idara maalum kusimamia matumizi ya fedha ili kuhimiza maendeleo ya utaratibu huo."
Aidha, suala la watumishi wa huduma za afya vijijini pia linafuatiliwa na wajumbe hao. Mjumbe Bw. Yan Hongcheng alipendekeza kuboresha mazingira ya kazi na maisha kwenye vituo vya afya vijijini, kuhakikisha maslahi na mishahara ya watumishi wa afya na kuwaandaa madaktari vijijini kwa njia mbalimbali. Hospitali kubwa au za mijini zinapaswa kutoa maelekezo na misaada kwa vituo vya matibabu vijijini ili kuinua uwezo wa watumishi wa afya vijijini.
|