Soko la Xiushui lililopo kando ya barabara kuu ya Changan hapa mjini Beijing, ni maarufu kwa biashara ya nguo. Soko hilo linawavutia sana wageni kutokana na kuwa na nguo za hariri za mtindo wa Kichina. Zamani kwenye soko hilo, kulikuwa na wafanyabiashara waliokuwa wanauza nguo zilizokuwa zimewekwa chapa maarufu za bandia. Kutokana na juhudi za pamoja za idara ya usimamizi wa soko na wafanyabiashara wa soko hilo, sasa hali hiyo haipo tena, nguo zote zinazouzwa kwenye soko hilo zinatumia chapa zinazolindwa na hakimiliki ya ujuzi. Hivi karibuni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa hakimiliki ya ujuzi iliyo chini ya shirika la biashara la Ulaya Bw. Paul Ranjard alitembelea soko hilo, akiwapa wafanyabiashara 40 wa soko hilo tuzo ya maduka bora ya kulinda hakimiliki ya ujuzi.
Zamani soko la Xiushui lilikuwa ni soko la nguo lenye urefu wa mita 200 hadi 300 kandoni mwa barabara kuu ya Changan, mjini Beijing. Katika miaka ya 80 na 90 ya karne iliyopita, maduka ya soko hilo yalianza kujulikana kwa biashara ya nguo za hariri. Kwa kuwa ubalozi wa nchi mbalimbali na ofisi nyingi za mashirika ya kimataifa zipo karibu na soko la Xiushui, wageni wengi wakija Beijing wanapenda kutembelea soko hilo. Kulikuwa na kipindi ambacho wafanyabiashara wa soko hilo walikuwa wanajishughuisha na biashara ya nguo zilizotumia chapa maarufu za bandia, ili kukidhi mahitaji ya baadhi ya wateja wanaopenda kununua nguo zenye chapa maarufu. Nguo hizo zenye chapa bandia zilinunuliwa sana na wageni kutokana na kuuzwa kwa bei ya chini.
Ili kulinda haki na maslahi ya wenye chapa hizo na wateja, idara ya usimamizi ya soko la Xiushui ilichukua hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kuwaelimisha wafanyabiashara wa huko kwamba, kuuza nguo zinazotumia chapa ya bandia ni kitendo cha kukiuka hakimiliki ya ujuzi, na kulifanyia ukarabati soko hilo. Ukarabati huo ulianza miaka mitatu iliyopita, hivi sasa maduka zaidi ya elfu moja ya soko hilo yamehamia kwenye jengo jipya lenye ghorofa saba.
Bw. Hua Shijun amekuwa akifanya biashara kwenye soko la Xiushui kwa miaka mingi. Aliwahi kufanya biashara ya nguo zilizotumia chapa bandia, lakini hivi sasa ameacha kufanya biashara hiyo na kuuza nguo zenye chapa zinazolindwa na hakimiliki ya ujuzi, zaidi ya hayo bwana huyo anawahamasisha wateja wanunue nguo hizo zisizotumia chapa bandia. Alisema"Zamani nilikuwa nauza nguo zenye chapa bandia, lakini sasa nimeacha biashara hiyo. Sasa bado kuna wageni wengi wanaokuja soko la Xiushui ili kununua nguo zenye chapa bandia. Watu hao wakija wanatuuliza kuhusu nguo hizo, na sisi tunajitahidi kuwashawishi waache tabia hiyo."
Duka la Bw. Hua lina eneo la mita 150 za mraba, ambalo linauza nguo, kofia na viatu.
Katika soko hilo mwandishi wetu wa habari aliona mbali na Bw. Hua, wenye maduka wengine pia wameacha biashara za bidhaa zinazotumia chapa bandia. Zaidi ya hayo yalijitokeza maduka mbalimbali yanayouza vito na vitu vya mapambo vya mtindo wa jadi wa China. Soko la Xiushui lenye sura mpya sasa linawavutia watu wengi zaidi kutoka kila pembe ya dunia.
Bw. Jim Michael anatoka Canada, ana mpango wa kukaa mjini Beijing kwa siku 20. Hii ni mara yake ya pili kutembelea soko hilo. Alisema "Kununua vitu na kujadiliana bei kwenye soko hilo ni jambo la kufurahisha watu. Wenye maduka wa hapa ni watu wenye urafiki, na bidhaa wanazouza zina sifa nzuri. Mimi na mke wangu tulishanunua vitu vingi, pochi, makoti, sweta n.k.. Sasa naona sanduku langu ni dogo, ni afadhali ninunue sanduku lingine kubwa ili niweze kuweka vitu vyote tulivyonunua."
Kampuni kadhaa zenye chapa maarufu za jadi za China pia zilianzisha maduka kwenye soko hilo, kama vile duka la vitambaa, duka la viatu na duka la kofia, ambayo yanawavutia sana wageni. Duka liitwalo Ruifuxiang ni maarufu sana miongoni mwa maduka hayo. Duka hilo linauza vitambaa vya hariri na sufi, lina historia ya miaka zaidi ya 100. Tawi la duka la Ruifuxiang lililoanzishwa kwenye soko la Xiushui lina eneo la mita 160 za mraba, linauza vitambaa vya aina zaidi ya 100. Meneja mkuu wa duka hilo Bw. Zhou Guoping alieleza kuwa, duka hilo linauza vitambaa vya hariri vinavyotengenezwa huko Suzhou na Hangzhou, mahala panapojulikana kwa uzalishaji wa hariri nchini China.
Alisema "Vitambaa tunavyouza vinatoka kwenye duka kuu la kampuni yetu ambayo inapata bidhaa hizo kutoka Suzhou na Hangzhou. Ni lazima bidhaa hizo ziwe na sifa nzuri zinazolingana na vigezo vyetu, kwa mfano uzuri wa rangi na uimara wa rangi, tuna ripoti za upimaji juu ya bidhaa hizo, kwani tunapaswa kuwahakikishia wateja wananunua bidhaa zetu zenye sifa nzuri."
Kutokana na ubora wa hali ya juu wa bidhaa na uaminifu wa wateja, watu wengi wakija kwenye duka la Ruifuxiang wananunua vitu kabla ya kuondoka. Na wageni wengi wakinunua vitambaa, pia wanapenda kushonewa nguo kwa mtindo wa jadi wa China kwenye duka hilo, hata baadhi ya wateja wanataka kuvaa nguo mpya mara moja. Ili kukidhi mahitaji ya wateja hao, ambao wengi ni wageni wanaokuwepo hapa Beijing kwa muda mfupi, duka la Ruifuxiang limeanza kutoa huduma mpya ya kutengeneza nguo kwa haraka.
Meneja mkuu wa duka hilo Bw. Zhou alisema Tunaahidi kukamilisha utengenezaji wa nguo ndani ya saa 24 kwenye duka letu lililopo kwenye soko la Xiushui. Ili kutimiza ahadi hiyo, kampuni yetu imeandaa magari kadhaa yanayopeleka nguo na wafanyakazi wanabadilishana zamu kutwa kucha. Mteja akija na kukubaliana nasi kuhusu saa ya kuchukua nguo, kwa mfano saa fulani kwenye hoteli fulani, tutapeleka nguo bila kuchelewa, na mteja ataweza kuvaa nguo mpya papohapo. Kwa hiyo huduma hiyo inawafurahisha sana wateja wageni."
Mpaka hivi sasa maduka mengi ya soko la Xiushui yamepata idhini ya kuuza bidhaa zilizotolewa na kampeni zenye chapa wanazotumia. Maendeleo ya soko hilo ni sehemu ya mafanikio iliyopata China katika juhudi za kulinda hakimiliki ya ujuzi. Maendeleo hayo pia yalimvutia Bw. Paul Ranjard ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa hakimiliki ya ujuzi iliyo chini ya shirika la biashara la Ulaya. Hivi karibuni yeye mwenyewe alitembelea soko la Xiushui na kuwapa wenye maduka 40 tuzo ya maduka hodari katika ulinzi wa hakimiliki ya ujuzi. Bw. Ranjard alisema (sauti 8) "Tunafurahi kushuhudia jitihada zilizofanywa ili kuondoa matatizo hayo, jitihada hizo ni pamoja na kuweka mkakati wa kulinda hakimiliki ya ujuzi kwenye soko la Xiushui, kuanzisha mfuko wa ulinzi wa hakimiliki ya ujuzi na kuwapa tuzo wenye maduka hodari katika ulinzi wa hakimiliki ya ujuzi."
|