Hivi karibuni serikali ya China ilitangaza rasmi kuanzisha mradi wa miaka mitano wa kuchunguza na kuweka orodha ya vitabu vya kale kote nchini ili kupata idadi halisi, kupima thamani ya vitabu hivyo na kufahamu mazingira ya kuhifadhi vitabu hivyo, kuchapisha orodha ya vitabu hivyo na kuandaa wataalamu wa kukarabati vitabu hivyo.
China ina historia ya miaka elfu tano ambayo ipo kwenye kumbukumbu ya maadishi. Katika China ya kale, licha ya kuandikwa kwenye karatasi, vitabu pia vilikuwa vinaandikwa kwenye vipande vya mianzi na vitambaa vya hariri. Kwa kawaida tunaposema vitabu vya kale, tuna maana vile vitabu vilivyoandikwa kwenye karatasi. Vitabu vitakavyochunguzwa na kuorodheshwa ni vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kichina kabla ya mwaka 1912 na vingine vilivyoandikwa kwa lugha nyingine za makabila madogo ya China. Vitabu hivyo vingi zaidi vimehifadhiwa katika majumba ya makumbusho na maktaba, lakini pia vipo miongoni mwa raia. Kwa makadirio ya wataalamu, idadi ya vitabu hivyo ni zaidi ya milioni 30. Katika historia ndefu vitabu hivyo viliharibika kwa kiasi fulani kutokana na vurugu za vita, kuliwa na wadudu, kugandiana kwa karatasi na hali mbaya ya matunzo. Kazi ya kuboresha mazingira ya kutunza vitabu hivyo haitakiwi kuchelewa zaidi.
Katika mradi huo, vigezo kadhaa vimetolewa kuhusu mazingira ya majumba ya kuhifadhia vitabu hivyo na ufundi wa kukarabati. Ofisa anayeshughulikia maktaba katika Wizara ya Utamaduni Bi. Liu Xiaoqin alisema, vigezo vina lengo la kuboresha mazingira ya kutunza vitabu hivyo. Alisema,
"Hivi sasa mazingira ya kutunza vitabu hivyo yana tofauti kubwa katika sehemu tofauti nchini China. Mazingira mazuri yanatakiwa yawe na joto maalumu na kiasi cha unyevunyevu bila kuwa na wadudu wala mavumbi, lakini sasa kwa kawaida vitabu hivyo vingi vimeachwa kwenye rafu tu kama vitabu vya kawaida."
Bi. Liu Xiaoqin alisema baada ya kutathmini vitabu hivyo kwa ngazi, serikali kuu itatenga fedha kukarabati vitabu vya ngazi ya kwanza na ya pili ambavyo viko kwenye hali ya hatari ya kutoweka, na vitabu vingine pia vitahifadhiwa kwa mujibu wa hali vilivyo.
Mtaalamu wa ukarabati wa vitabu vya kale Bw. Du Wei alipozongumza na waandishi wa habari alisema, hifadhi ya vitabu vya kale ni kazi ya kudumu, vitabu vingi vilivyopo sasa vimekuwepo kwa karne kadhaa na hata miaka elfu moja, licha ya kuwa vitabu hivyo vimeharibika kimaumbile, hifadhi ya vitabu hivyo inakabiliwa na changamoto mpya yaani uchafuzi wa hewa. Alisema,
"Utunzaji wa vitabu vya kale unatakiwa kuwa wa kiwango cha juu, hatua za kuhifadhi na kukarabati vitabu hivyo ni lazima zisaidie kudumisha vitabu hivyo, na ukarabati pia ni lazima utumie mbinu za kisayansi, ili kuhifadhi kwa muda mrefu."
Hivi sasa kuna wataalamu wa ukarabati wa vitabu vya kale nchini China mia moja tu, na wengi wao hawajawahi kupata mafunzo ya kitaalamu. Ufundi wao unatokana na kuiga uzoefu wa wenzao wazee, na umekuwa duni. Zaidi ya hayo wataalamu wazee wanazidi kustaafu na kumetokea pengo kati ya wataalamu wazee na vijana, hali hiyo imeathiri vibaya ukarabati wa vitabu hivyo.
Kutokana na hali hiyo, maandalizi ya wataalamu wa ukarabati ni lazima yaende sambamba na uchunguzi. Kituo muhimu cha kuandaa wataalamu vijana ni maktaba ya taifa. Maktaba hiyo ni kituo kikubwa cha kuhifadhi vitabu vya kale nchini China. Katika miaka ya hivi karibuni kituo hicho kimepanga na kukarabati vitabu vingi adimu. Mkuu wa kikundi cha ukarabati katika maktaba hiyo Bw. Zhang Ping alisema, katika mradi huo kituo hicho kitabeba majukumu kadhaa muhimu. Alisema,
"Katika maandalizi ya wataalamu wa ukarabati tuna majukumu mawili, moja ni kutofautisha vitabu hivyo kwa ngazi tofauti kwa mujibu wa hali ya uharibifu, nyingine ni kuthibitisha kiwango cha utaalamu kwa wataalamu wa ukarabati, na vile vile tutawafundisha wataalamu vijana watakaoshughulikia kazi ya ukarabati."
Wataalamu katika maktaba ya taifa wametoa kanuni za ukarabati zikiwa ni pamoja na kanuni ya kukarabati vitabu vya kale ili kudumisha hali yake ya kale baada ya kukarabatiwa, na ukarabati wa sasa uwe rahisi kuondolewa na kukarabatiwa tena kwa ufundi utakaotokea baadaye ambao ni wa kisasa zaidi. Walisema, kutokana na utafiti wa miaka mingi utaalamu wa ukarabati umekuwa wa kisayansi, wataeneza utaalamu wao kupitia mradi huo.
Mkuu anayeshughulikia mambo ya maktaba katika Wizara ya Utamaduni Bi. Liu Xiaoqin aliwaambia waandishi wa habari akisema, lengo la kufanya uchunguzi kote nchini ni kwa ajili ya kuorodhesha vitabu vya kale, ili vitabu hivyo viwekwe katika mpango wa kutunzwa. Alisema,
"Lengo la uchunguzi wa vitabu vya kale kote nchini China ni kupata orodha ya vitabu vyote vinavyohifadhiwa kwenye maktaba za serikali au binafsi, au vinavyohifadhiwa na watu binafsi, na hata vile katika maktaba za serikali katika sehemu ya Macau, Hong Kong na Taiwan. Bi. Liu Xiaoqin alisema serikali inawahamasisha watu binafsi waandikishe vitabu vyao na itawasiliana na idara husika za nchi za nje kuandikisha vitabu vyao ili vitabu hivyo ambavyo ni hazina iliyoachwa na wahenga wa China irithishwe kizazi baada ya kizazi.
|