Kwenye mkutano wa mwaka wa bunge la umma la China uliofungwa hivi karibuni, sheria mpya ya kodi ya mapato ya viwanda na makampuni ilipitishwa kwa kura nyingi. Sheria hiyo imeweka kigezo cha namna moja kodi za mapato ya makampuni na viwanda vya mitaji ya kigeni na ya China, na kuweka kiwango kipya cha kodi kuwa asilimia 25. Hii inaondoa upendeleo wa kodi kwa makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni nchini China kwa kiasi fulani, na kuvipa viwanda na makampuni nchini China mazingira ya soko yenye usawa zaidi. Kuanzia mwaka kesho, sheria ya kodi ya mapato ya viwanda itaanza kutekelezwa rasmi, je makampuni na viwanda vya China na vya nchi za nje vina maoni gani kuhusu utaratibu huo mpya wa utozaji kodi?
Japan ni nchi ya pili iliyowekezwa kwa wingi nchini China. Hivi sasa thamani ya uwekezaji wa Japan nchini China kwa ujumla imekaribia dola za kimarekani bilioni 60, na kampuni nyingi za Japan zimeunda vituo vya uzalishaji mali nchini China. Kampuni ya Omron ikiwa ni kampuni maarufu duniani kwa uzalishaji wa mitambo inayojiendesha na zana za elektroniki, iliingia nchini China miaka ya 80 ya karne iliyopita, na mwaka 2002 ilianzisha rasmi tawi la China, na fedha ilizowekeza nchini China zimefikia dola za kimarekani milioni mia kadhaa.
Meneja mkuu wa tawi la China la kampuni ya Omron Bw. Yamashita Toshio alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, Omron imepata fununu kuhusu utekelezaji wa utaratibu mpya wa utozaji kodi, hivyo uendeshaji wa kampuni hautaathiriwa sana.
"Hivi sasa, sioni kama sheria hiyo italeta athari kwetu kuweka mitaji nchini China. Serikali ya China kupunguza na kuondoa tofauti kati ya makampuni na viwanda vya China na vya nchi za nje ni mwendo baada ya China kujiunga na WTO. Kwa kweli tuliweza kukadiria kuwa serikali ya China itapunguza hatua kwa hatua upendeleo kwa makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni siku China ilipojiunga na WTO. Lakini hali hiyo haitaathiri nia yetu ya kuwekeza mitaji nchini China."
Bw. Yamashita Toshio alisema kampuni ya Omron inatilia maanani soko la China, na thamani ya uwekezaji mitaji nchini China katika miaka mitatu iliyopita ilifikia Yuan za RMB bilioni 2; mwezi Aprili mwaka jana, kampuni ya Omron pia ilianzisha kituo cha kwanza cha utafiti wa bidhaa huko Shanghai, China, ambacho kimekuwa cha pili kwa kundi la Omron kuanzisha kituo cha utafiti nje ya Japan baada ya kuanzisha kituo huko silicon valley, Marekani. Alisema mwaka 2007, Omron inapanga kuuza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani zaidi ya bilioni 1.3 nchini China, ambayo itachukua asilimia 20 ya thamani ya jumla ya uuzaji bidhaa ya Omron.
Bw. Yamashita Toshio alisema lengo la China kutunga sheria ya kodi ya mapato ya viwanda ni kuweka mazingira ya soko yenye haki zaidi, hailengi makampuni na viwanda vilivyowekezwa na wageni.
"Baada ya China kujiunga na WTO, imekuwa inafungua zaidi soko lake, na kuambatana na hali ya kimataifa katika sekta nyingi, makampuni na viwanda vyote hodari duniani vinapenda kuja China kufanya ushindani. Tunapenda kuona makampuni na viwanda vyote vinashindana katika mazingira yenye usawa, na kutengeneza na kutafiti bidhaa zinazolingana na mahitaji ya soko la China ni msingi wa kupata mafanikio katika soko. Hivyo sioni kuwa kuweka kigezo cha namna moja kodi mbili kutatishia makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni."
Makampuni na viwanda vya Umoja wa Ulaya pia vinauelewa utaratibu huo mpya wa kodi. Ikiwa mwenzi mkubwa kabisa wa biashara wa China, thamani ya uwekezaji ya Umoja wa Ulaya nchini China imekuwa inaongezeka kwa kasi katika miaka ya karibuni. Mwaka jana, zaidi ya miradi 2,700 iliwekezwa na Umoja wa Ulaya nchini China, na thamani ya mkataba ilifikia dola za kimarekani zaidi ya bilioni 10. Uchunguzi mpya umeonesha kuwa, asilimia 92 ya makampuni na viwanda vya Ulaya vinafurahia maendeleo yao nchini China.
Mwakilishi wa kwanza wa shirikisho la kuhimiza biashara ya nje la Italia Bw. Antonino Laspina alisema, soko la China linavutia sana makampuni na viwanda vya Ulaya, alisema,
"Mvuto wa utaratibu wa uchumi wa China sio tu unatokana na utaratibu huo, bali pia kuna sababu nyingine, kwa mfano nguvu kazi, China ina wafanyakazi wenye sifa bora, na mishahara yao ni ya chini; licha ya hayo, China inaweza kuweka mazingira mazuri zaidi kuliko zamani, ikiwemo uchukuzi na miundo mbinu. Hivyo kwa upande wa viwanda, kuweka mitaji na kuanzisha viwanda nchini China ni chaguo linalolingana na soko, na jambo muhimu kabisa ni kwamba wanaweza kupata soko kubwa hapa China."
Ikilinganishwa na makampuni na viwanda vya nchi za nje, makampuni na viwanda vya China vinafurahia zaidi utaratibu huo mpya wa kodi. Kwa sababu kutokana na utaratibu wa sasa wa kodi nchini China, ingawa kiwango cha utozaji kodi kwa makampuni na viwanda vinavyowekezwa na China na nchi za nje kuwa ni asilimia 33, lakini kwa kuwa China inatekeleza utaratibu wa kutoa nafuu katika utozaji kodi kwa makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni katika baadhi ya sehemu, utozaji kodi wa makampuni na viwanda vya China unakuwa asilimia 10 zaidi kuliko ule wa makampuni na viwanda vya nchi za nje.
Imefahamika kuwa baada ya kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango mwishoni mwa miaka 70 ya karne ya 20, ili kuvutia mitaji ya nje na kukuza uchumi, China ilitekeleza sera tofauti ya utozaji kodi kwa makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni. Uzoefu pia umeonesha kuwa, kwa kupitia sera za kutoa nafuu kwa makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni, China inajifunza teknolojia ya kisasa kutoka kwenye makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni, na kupata uzoefu wa usimamizi wa kisasa wa makampuni na viwanda, pia inaongeza mapato ya fedha za kigeni.
Lakini kadiri China inavyoendelea, utaratibu wa utozaji kodi unaotekelezwa hivi sasa haulingani na matakwa ya hali mpya. Baada ya kujiunga na WTO, soko la China limefunguliwa zaidi, viwanda vyenye mitaji ya China pia vinajiunga hatua kwa hatua na mfumo wa uchumi duniani, na vinakabiliwa na shinikizo kubwa la ushindani. Hivyo sauti ya makampuni na viwanda vyenye mitaji ya China kuhusu kuondoa upendeleo wa utozaji kodi ilikuwa inaongezeka siku hadi siku.
Meneja mkuu wa kiwanda maarufu cha utengenezaji wa vyombo vya umeme vya nyumbani nchini China?TCL Bw. Li Dongsheng anaona kuwa, ni jambo la kuweka kigezo cha namna moja cha kodi kwa makampuni na vile vinavyowekezwa na wageni na viwanda vyenye mitaji ya China.
"Naona hivi sasa inafaa 'kuweka kigezo cha namna moja cha kodi'. Hivi sasa uchumi wa China umeendelezwa katika hali ya juu, baada ya kujiunga na WTO, tumeondoa vifungu vingi vinavyoweka vikwazo kwa uingizaji wa makampuni na viwanda vinavyowekezwa na wageni katika soko la China. Hivyo naona kuwa sasa kutoa utaratibu huo mpya ni mwafaka pia ni wenye usawa."
Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai baada ya kupitishwa kwa Sheria ya kodi ya mapato ya makampuni na viwanda alisema, zamani kutekeleza utaratibu tofauti wa utozaji kodi ilikuwa ni halali, kwa kuwa ilihimiza mitaji mingi ya kigeni kuingia katika soko la China; lakini sasa kuweka kigezo cha namna moja cha kodi pia ni halali, kwa kuwa itahimiza China kutumia mitaji ya kigeni vizuri zaidi. Alisema kutokana na sheria mpya ya kodi, makampuni na viwanda vyenye mitaji ya kigeni vilivyopewa nafuu zamani vitakuwa na muda wa miaka mitano wa utaratibu wa kupewa nafuu, na viwanda vyenye mitaji ya kigeni vinavyoweka mitaji katika teknolojia ya kisasa na hifadhi ya mazingira pia vitapewa nafuu ya kodi.
Mtaalam wa uchumi Bw. Lin Yifu alisema, kutokana na ukubwa wa soko la China na ubora wa nguvu kazi, utekelezaji wa sheria mpya ya kodi hautaathiri uwekezaji mitaji wa wafanyabiashara wa kigeni katika siku za usoni.
Sheria mpya ya kodi inaviweka viwanda na makampuni yanavyowekezwa na wageni na vile vyenye mitaji ya China katika mstari mmoja. Mageuzi hayo yanasaidia kuweka mazingira yenye usawa kwenye soko, na kuhimiza viwanda kufanya ushindani kwa utaratibu ili kuhimiza kuinua kiwango cha miundo ya sekta ya uzalishaji.
Idhaa ya kiswahili 2007-04-17
|