Mzee Fang Cheng mwenye umri wa miaka 89, ni mchoraji mashuhuri wa picha za katuni nchini China, ameshughulika na utafiti wa uchoraji wa picha za katumi kwa miaka mingi. Picha alizochora zinawachekesha sana watu hata kuwavunja mbavu, na huku zinawafanya watu watafakari. Licha ya kuchora picha, ameandika vitabu vingi vya nadharia ya uchoraji wa picha za katuni.
Si rahisi hata kidogo kuonana na mzee Fang Cheng, kwani wakati wake karibu wote anautumia kuandika makala zake, isipokuwa tu mara moja moja anapokutana na marafiki zake wachache. Ingawa amekuwa na umri wa miaka karibu 90 lakini ni mtu mchangamfu na mwenye akili sana. Mzee huyo anakumbuka mambo mengi aliyopitia.
Mzee Fang Cheng alituambia kuwa ilikuwa ni bahati tu kwa yeye kuanza kazi ya uchoraji wa katuni maishani mwake. Katika miaka ya 30 ya karne iliyopita Fang Cheng alipohitimu shule ya sekondari ulikuwa ni wakati ambapo China ilikuwa inakabiliwa na mashambulizi ya Japan, wanafunzi walikuwa wanafanya maandamano na shule zilihitaji watu kuchora picha za katuni kuwahamasisha watu kupinga mashambulizi ya Japan, na Fang Chen alianza kuchora picha hizo. Baada ya miaka kadhaa, picha alizochora zilikuwa zinajulikana katika jamii. Mwaka 1946 Fang Cheng alikwenda mjini Shanghai kutafuta maisha. Kutokana na uhodari wake wa kuchora picha za katuni, bila ya shida alikubaliwa kuwa mchoraji katika kampuni ya matangazo ya biashara.
"Bahati nzuri wakati huo kampuni ya matangazo ya biashara ilihitaji mchoraji mmoja. Mwaka 1946 China ilikuwa imeshinda vita dhidi ya mashambulizi ya Japan, kutokana na kuwa watu wengi hawakuwa na ajira, msururu wa kuomba ajira ulikuwa mrefu sana, mimi nilijihimu na kukimbia haraka nikawa mtu wa kwanza kwenye msururu nikitamani sana kupata ajira, kwa sababu nilikuwa sina pa kulala wala pesa za kununulia chakula. Mtu aliyeshughulika na ajira alikuwa Mmarekani, alinitaka nichore picha moja kama mtihani, sikuwa na uwezo wa kuchora picha za aina nyingine ila za katuni, alipoona picha niliyochora mara akasema 'sawa sawa, umekubaliwa.' "
Licha ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, Fang Cheng alitumia wakati wa mapunziko kuchora picha akijaribu zichapishwe katika magazeti makubwa mjini Shanghai, baadaye picha alizochora kwenye magazeti zilimvutia mhariri mmoja wa gazeti moja na hata baadaye alikuwa mhariri mkuu wa ukurasa wa picha za katuni katika gazeti hilo.
Katika miaka ya nyuma Fang Cheng aliwahi kufanya kazi katika Hong Kong, mwaka 1950 alihamia Beijing na kuwa mchoraji katika gazeti la Ren Min Ri Bao mpaka alipostaafu. Mwanzoni alipokuwa katika gazeti hilo alichora zaidi picha za mambo ya kisiasa ulimwenguni, na kila siku alichora picha moja. Katika miaka hiyo ambapo shughuli za kidiplomasia zilikuwa chache nchini China, picha alizochora ziliwasaidia sana wasomaji kufahamu mambo ya nje. Alipokumbuka jinsi alivyofanya kazi wakati huo alisema,
"Kila siku nilikuwa nashika zamu ya usiku, kiasi cha saa tatu hivi makala za kuchapishwa gazetini zilipowasilishwa tulifanya mkutano wa kuamua makala gani zichapishwe katika gazeti la siku ya pili, na mimi nilianza kuchora picha na kumaliza kabla ya saa sita za usiku ili kuwahi kutengeneza pleti, vivyo hivyo kila siku niliandaa picha moja."
Mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, Fang Cheng alichora picha za katuni zaidi ya 100. Picha hizo, baadhi zinadhihaki hali mbaya katika jamii, na baadhi zinakosoa uzembe wa kazi. Moja kati ya picha hizo ni "Mwenye Duka Wu Dalang". Bw. Wu Dalang alikuwa mbilikimo katika fasihi ya kale ya China, katika picha hiyo watumishi walioajiriwa wote walikuwa ni wafupi zaidi kuliko Wu Dalang, ikimaanisha kuwa baadhi ya viongozi wanadhalilisha watu hodari kwa hofu ya kuzidiwa. Wakati huo alifanya maonesho ya picha alizochora kwa mzunguko katika miji kadhaa na kusababisha kishindo kikubwa. Alisema,
"Wakati huo maonesho yalipofanywa katika mji mmoja, mji mwingine ulikuwa unasubiri kwa hamu, kwenye maonesho watazamaji walisongamana, na baadhi walitoka mbali. Maonesho yalipomalizika katika mji mmoja mara yalisafirishwa kwenda mji mwingine kwa masanduku. Maonesho hayo yalifanywa kwa mzunguko katika miji zaidi ya kumi."
Bw. Fang Cheng alipotunga picha alizochora pia alikuwa anafanya utafiti kuhusu nadharia ya uchekeshaji. Mpaka sasa amekwisha chapisha vitabu vya nadharia ya uchekeshaji zaidi ya kumi na atachapisha vitabu vingine vitatu hivi karibuni. Alisema, uchekeshaji ni sanaa ya lugha, ni akili ya binadamu, lengo lake ni kuwachekesha watu na kuwafanya watafakari maana ya undani. Aliwahi kutoa mihadhara nchini Marekani na anatumai kutoa mihadhara katika nchi nyingine. Alisema,
"Nafahamu kwamba uchekeshaji unatokana na lugha, na namna ya kuchora picha ni ufundi. Nilipotoa mihadhara huko Marekani nilikuwa naeleza kwa kutumia picha nilizochora."
Mzee Fang Cheng ni mtu mwenye urafiki na mwenye lugha ya kuchekesha. Alisema hataki kuwa mzee asiyefaa kwa lolote, anataka kufanya mambo mengi zaidi. Alijichorea picha moja akiwa anapanda baiskeli, mwenye nywele chache lakini mwenye tabasamu. Kuendesha baiskeli ni mchezo anaoupenda, akienda posta au kwenye soko la mboga huwa anapanda baiskeli. Hivi sasa anaendelea kuwa na hamu ya kujifunza, anaweza kutumia kompyuta na kusoma hadithi za picha ambazo huwa zinapendwa na vijana, ili apate msukumo wa kutunga picha.
Idhaa ya kiswahili 2007-04-23
|