Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-27 10:14:11    
Ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta za uchumi na biashara wapata mafanikio makubwa

cri

Katika miaka kadhaa iliyopita, ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta za uchumi na biashara uliimarishwa siku hadi siku. Hasa kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika hapa Beijing mwaka jana, kulifungua ukurasa mpya wa ushirikiano huo. Katika mkutano wa mwaka wa benki ya dunia na shirika la kifedha la kimataifa (IMF) uliofanyika mjini Washington hivi karibuni, mawaziri wa fedha wa nchi nyingi za Afrika walieleza kuwa, China ni mwenzi wa ushirikiano wa nchi za Afrika, na ushirikiano kati yao katika sekta za uchumi na biashara unanufaisha maendeleo ya pande hizo mbili.

Waziri wa fedha na mipango ya taifa wa Zambia Bw. Ng'andu Magande alisema, uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Zambia unajengwa kwa msingi wa kunufaishana ulio wa muda mrefu. Alisema nchi za Afrika hazina wasiwasi na China, China na nchi za Afrika zinafanya ushirikiano kwa ajili ya maendeleo yao, na China ni rafiki na mwenzi wa ushirikiano wa nchi za Afrika.

Serikali ya China siku zote inaunga mkono kampuni zake kuwekeza barani Afrika, ili kuhimiza kampuni za China ziwekeze barani Afrika, serikali ya China ilianzisha mfuko wa maendeleo wa China na Afrika wenye thamani ya jumla ya dola za kimarekani bilioni 5. Katika miaka kadhaa iliyopita, thamani ya uwekezaji barani Afrika kutoka China ilifikia dola za kimarekani bilioni 6.27, na China iliwekeza barani Afrika katika sekta za biashara, uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa, maliasili, mawasiliano ya simu pamoja na kazi ya kilimo. Mwezi Septemba mwaka jana, wajumbe 1,500 wa China na Afrika walihudhuria mkutano wa wawekezaji wa China na Afrika uliofanyika hapa Beijing, na walisaini makubaliano ya ushirikiano yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.9.

Mwezi Aprili mwaka huu China na Afrika ya Kusini zilisaini makubaliano manane yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 143. Kutokana makubaliano hayo, China itanunua mvinyo, sufu na shaba kutoka Afrika ya Kusini. Kabla ya kusaini makubaliano hayo, kampuni ya China na kampuni ya Namibia zilisaini makubaliano ya biashara yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 20. Mwezi Machi mwaka huu, sehemu ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Zambia ilifunguliwa rasmi, hii ni sehemu ya kwanza ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara iliyoanzishwa na China barani Afrika. Kuanzishwa kwa sehemu hiyo pia kulionesha kuwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika uliingia kwenye kipindi kipya cha maendeleo.

Waziri wa fedha wa Liberia Bw. Antoinette M. Sayeh alisema, katika miongo kadhaa iliyopita, China imepata mafanikio makubwa kuliko nchi nyingine katika kupunguza umaskini, na nchi za Afrika zinapaswa kuiga uzoefu wa China.

Suala la usalama wa chakula ni tatizo linalokabili nchi nyingi za Afrika. Ili kuzisaidia nchi za Afrika kutatua suala hilo na kuinua uwezo wa kujiendeleza, China ilipeleka maarifa na ufundi wake barani Afrika. Katika miaka mitatu ijayo, China itaanzisha sehemu 3 au 5 za ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara barani Afrika, na kutuma wataalamu 100 wa kilimo barani Afrika, na kuanzisha vituo 10 vya vielezo vya ufundi wa kilimo vyenye umaalumu barani Afrika.

Maofisa wa nchi za Afrika waliona kuwa hadhi ya China katika biashara ya kimataifa inayozidi kuongezeka siku hadi siku itahimiza biashara ya kimataifa. Naibu waziri mkuu wa Mauritania ambaye pia ni waziri wa fedha na maendeleo ya uchumi Bw. Shitanan alisema, katika historia, mfumo muhimu wa biashara ya kimataifa ni biashara kati ya Kusini na Kaskazini, lakini nchi za Afrika zinaona kuwa biashara kati ya Mashariki na Magharibi, na biashara kati ya Kusini na Kusini zitanufaisha biashara kati ya Kusini na Kaskazini.

Katika miaka kadhaa iliyopita, biashara kati ya China na Afrika iliongezeka haraka sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya biashara ya China, thamani ya biashara kati ya China na Afrika ya mwaka jana ilifikia dola za kimarekani bilioni 55.5, na kuongezeka kwa asilimia 40 kuliko ile ya mwaka 2005, thamani hiyo imeongezeka kwa asilimia zaidi ya 30 kwa miaka mitano ya mfululizo.

Biashara kati ya China na Afrika pia ilitoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa Afrika. Watu husika wa Afrika walieleza kuwa, maendeleo ya uchumi wa China yanahimiza ongezeko la zaidi ya asilimia 5 la uchumi wa Afrika mwaka 2005. Waziri mkuu wa zamani wa Mali Bw. Soumana Sako alisema, Afrika inanufaishwa kutokana na uhusiano wa kiwenzi na ushirikiano kati yake na China. Vitega uchumi vya wachina barani Afrika vimeleta nafasi nyingi za ajira, na China imeletea bidhaa nzuri zenye bei nafuu kwenye nchi za Afrika, nchi za Afrika zinaweza kununua bidhaa mbalimbali kutokana na uwezo wa ununuzi wa wananchi wake.

Vyombo vya habari vinaona kuwa kadiri ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya uwekezaji unavyozidi kufanyika, mustakabali wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili kwenye sekta za uchumi na biashara utakuwa mzuri zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-27