Karibuni katika kipindi hiki cha "safari nchini China". Kwenye mkoa wa Guizhou ulioko sehemu ya kusini magharibi mwa China, wanaishi watu wa makabila madogo 48. Serikali ya mkoa wa Guizhou ikizingatia umaalumu wa kuweko kwa makabila mengi madogo, ilijenga majumba manne ya makumbusho yasiyo na uzio, ambayo yanawafahamisha watalii wa nchini na wa nchi za nje kuhusu utamaduni maalumu na desturi na mila za wakazi wa makabila madogo.
Hivi sasa, mkoa wa Guizhou umekwishajenga majumba manne ya makumbusho ya ikolojia ya makabila. Makumbusho hayo ya ikolojia ya makabila ni kama hifadhi za ikolojia ya makabila. Kila moja ya makumbusho hayo ya ikolojia ni kijiji kimoja, ambacho wanaishi wakazi wa kabila moja dogo, ndani ya makumbusho hayo hakuna ukumbi wala vitu vya kuoneshwa, watalii wanaweza kutembelea moja kwa moja na kuangalia mila, utamaduni na majengo katika kijiji. Alipoeleza makumbusho hayo ya ikolojia ya makabila ya mkoa wa Guizhou, Bw. Wang Jun, ambaye amefanya kazi ya kuongoza watalii kwa zaidi ya miaka 10, alisema,
"Kwa jumla kuna makumbusho manne ya ikolojia. Ya kwanza yako katika sehemu ya magharibi mwa Guizhou, China na Norway zimeshirikiana kujenga makumbusho ya ikolojia kwenye sehemu hiyo wanayoishi watu wa kabila la wamiao wenye pembe ndefu, ya pili ni hifadhi ya kimaumbile ya kijiji cha kabila la wadong iliyojengwa kusini mashariki mwa Guizhou, katika kusini mwa Guizhou pia kilijengwa kijiji cha kabila la wabuyi, na makumbusho ya nne yako kwenye tarafa ya kale ya Longli kusini mashariki mwa mkoa wa Guizhou."
Jumba la makumbusho ya ikolojia ya Suoga lilijengwa kwa ushirikiano kati ya mkoa wa Guizhou na idara husika ya Norway mwaka 1998 katika kijiji wanachoishi watu wa kabila la wamio wenye pembe ndefu. Kijiji hicho kina eneo la kilomita za mraba 120 na chenye watu zaidi ya 4,000 ambao wamekuwa wakiendeleza utamaduni wa kale wa kabila lao. Watu wa kabila hilo wanaitwa kuwa wamiao wenye pembe ndefu ni kutokana na watu hao wanafunga nywele zao kama pembe ndefu za maksai. Huko kuna hadithi moja kuwa, watu wa kabila la wamio wanaoishi kwenye eneo la karibu kilomita 100 la tarafa la Suoga wana desturi ajabu ya kupamba vichwa kwa ajili ya kuwatisha wanyamapori, kwanza wanaweka ubao wenye umbo la pembe za maksai ndani ya nywele, halafu wanasuka nywele kwenye ubao na kuzifunga nywele kwa nyuzi za katani na sufu. "Mapambo ya kichwani" hayo yanaweza kufikia kilo mbili kwa yale makubwa zaidi, nywele zao zikifunguliwa zinaweza kufikia urefu wa mita 3, mapambo hayo ya kichwani yenye pembe ndefu yamekuwa kama alama maalumu ya tawi hilo la kabila la wamiao. Bw. Xu Meilin ni mkuu wa jumba hilo la makumbusho ya ikolojia, alisema,
"Jumba hilo ni jumba la kwanza la makumbusho la ikolojia nchini China hata katika bara la Asia, kimsingi, utamaduni wa jadi haujabadilika. Utamaduni wake ni pamoja na mitindo maalumu sana ya jadi ya uzalishaji mali na maisha, kuna sanaa ya kiwango cha juu ya kuweka rangi kwenye vitambaa kwa kutumia nta, muziki na michezo ya ngoma maalumu ya jadi hususan mavazi na mapambo ya kichwani ya kabila hilo, ni ya kipekee kabisa duniani."
Kuingia katika kijiji cha wamiao cha Suoga kwa kufuata njia iliyotengenezwa kwa vipande vya mawe, watu wanaweza kuona mimea ya kitani iliyoanikwa kwenye penu za nyumba. Kitani ni mali-ghafi muhimu ya kutengenezea nguo za wamiao wenye pembe ndefu. Watalii wanaweza kuangalia utengenezaji wa nguo za wamiao toka mwanzo hadi mwisho kwenye tarafa ya Suoga, ikiwa ni pamoja na ufumaji wa kitambaa, utiaji rangi, utarizi na ushonaji. Nguo za watu wa kabila la wamiao wenye pembe ndefu zinashonwa kwa mikono, nguo na suruali zinashonwa kwa miaka miwili au mitatu. Mbinu za kutarizi kwenye nguo za wamiao ni zaidi ya aina 10, njia ya utarizi inayotumika zaidi ni kutumia uzi mwembamba wa nyuzi zaidi ya kumi zilizofunguliwa kutoka kwenye uzi wa kutarizi. Ustadi wa kiwango cha juu wa kutarizi unawashangaza sana watu. Licha ya kushuhudia makazi, nguo, ala za muziki na hali ya uzalishaji na maisha ya watu wa kabila la wamiao wenye pembe ndefu, watalii wanaweza kurekodi urithi huo wa kiutamaduni wenye thamani kubwa kwa zana za audio na video.
Jumba la makumbusho ya ikolojia ya kabila la wadong wa kijiji cha Tangan ni moja ya makumbusho manne ya mkoani Guizhou. Kijiji hicho kimekuwa na historia ya miaka zaidi ya 700. Nyuma ya kijiji cha Tangan ni msitu wa asili wenye maliasili nyingi. Jengo la kuwekea ngoma kubwa na daraja linalojulikana kwa daraja la upepo na mvua ni kama majengo ya vielelezo yaliyojengwa kwa ufundi mkubwa ya watu wa kabila la wadong. Kijiji cha Tangan kiko kwenye miteremko ya mlima, karibu wakazi wote wanaishi katika nyumba, ambayo pembe nne za paa la nyumba zinainuka kwa juu. Njia zote za kijijini zilitengenezwa kwa vipande vya mawe. Kuhusu umaalumu wa majengo ya kijiji cha kabila la wadong cha Dangan, mfanyakazi anayeongoza watalii Bw. Wang Jun alisema,
"Jengo lililojengwa katikati ya kijiji kwa kufuata mila ya kabila la wadong, ni jengo la kuwekea ngoma kubwa na lenye mtindo wa kipekee wa kabila la wadong. Jengo hilo lilitumika katika kupambana na mashambulizi wa maadui wa sehemu ya nje. Sasa limebadilika na kuwa sehemu ya burudani ya umma, ambapo wazee wanacheza bao na vijana wanachumbiana au kuimba nyimbo."
Baada ya kutoka katika kijiji cha Tangan, watu wanaweza kuona mashamba ya matuta yaliyotengenezwa kwenye miteremko ya milima, mfano wa mfululizo wa ngazi pana. Katika majira ya Spring, mashamba ya matuta yaliyojaa maji ya chemchem yanaonekana kama vioo vikubwa vinavyoangaza macho chini ya mwangaza wa jua; katika majira ya joto, miche ya mpunga inafanya miteremko ya milima kuwa ya rangi ya kijani na ya kupendeza sana; katika majira ya kupukutika majani, kitu wanachoona zaidi ni mpunga uliokomaa wenye rangi ya dhahabu. Kwa ufupi, katika majira yoyote yale, mashamba makubwa ya matuta ya kijiji cha Tangan yanafanya watu wasitake kuondoka. Ofisa wa serikali ya mkoa wa Guizhou bibi Long Chaoyun alisema,
"Sasa wanakijiji wa huko wameweza kuongea na watalii kwa lugha za kigeni."
Idhaa ya kiswahili 2007-04-30
|