Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-07 16:03:56    
Bw. Guo Degang na mchezo wake wa ngonjera ya kuchekesha

cri

Ngonjera ya kuchekesha iliwahi kuwa ni aina moja ya michezo ya sanaa inayowavutia sana Wachina, lakini katika miaka ya karibuni mchezo wa aina hiyo umekuwa katika hali ya kudidimia, baadhi ya watu walitoa kauli wakisema, "Tuokoe mchezo wa ngonjera ya kuchekesha!" Lakini kwa bahati nzuri, mwaka huu ameibuka mchezaji mmoja ambaye kwa ghafla amejulikana kote mijini Beijing na Tianjin, watu wengi wanasimama foleni kukata tikti za kusikiza mchezo wake, na amewahi kurudia maonesho ya mchezo wake jukwaani hata mara 20 kwa sababu ya kupendwa sana na wasikilizaji!

Guo Degang ana umri wa miaka 33, ana kimo cha wastani, mnene na kichwa cha mviringo. Anapoonesha mchezo wake huvaa nguo ndefu kama joho, vazi ambalo zamani lilikuwa linavaliwa na wasanii wa ngonjera.

Guo Degang alizaliwa mjini Tianjin ambapo wakazi wa huko wanapenda zaidi sanaa ya ngonjera ya kuchekesha. Tokea alipokuwa mtoto alipenda sana kusikiliza opera na ngonjera ya kuchekesha. Alipokuwa na miaka minane alianza kujifunza kwa mwalimu wa ngonjera, na baadaye aliwahi kujifunza na kuonesha michezo akiwa katika makundi mengi ya michezo ya sanaa tofauti mjini Tianjin.

Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, wakati ambapo hali ya mchezo wa ngonjera ya kuchekesha ulikuwa imedidimia vibaya, kulikuwa na watu wacheche tu ambao walikwenda kusikiliza mchezo huo na ilikuwa ni nadra kwa michezo ya ngonjera kuoneshwa kwenye televisheni. Ili kutafuta maisha Guo Degang aliwahi kufanya kazi za utingo na biashara ndogo, maisha yalimwia magumu sana. Lakini hata hivyo, hakuwahi kuacha hamu kupenda sanaa ya ngonjera ya kuchekesha.

Mwaka 1996 Guo Degang aliunda kikundi cha mchezo wa kuchekesha, na kuonesha michezo yao katika mikahawa midogo ya chai. Alipojikumbusha kuhusu siku hizo, Guo Degang alisema, "Sasa wasikilizaji wamejaa kwenye jumba na watu zaidi ya 200 wanasubiri nje ya jumba hili. Lakini mwanzoni hali ilikuwa ya kusikitisha sana, siku moja kulikuwa na msikilizaji mmoja tu, nilimwambia kwa utani 'leo unabahatika sana, tunaonesha mchezo kwa ajili ya peke yako, lazima usikilize kwa makini, ukitaka kwenda kujisaidia tuambie.' Sasa jambo hili limekuwa la kuchekesha, lakini wakati huo liliniumiza sana roho yangu."

Hivi sasa, baada ya miaka karibu kumi kupita, hali imebadilika kabisa, kwamba Guo Degang na wenzake wanavuma sana katika miji ya Beijing na Tianjin. Vyombo vya habari vinatoa habari nyingi kuhusu mchezo wao. Kila siku asubuhi mapema, zaidi ya watu mia moja husimama foleni kununua tikti za michezo yao na baadhi yao wanatoka mbali.

Lakini, kwa nini michezo ya Guo Degang inawavutia wasikilizaji namna hii? Sababu ni tatu zifuatazo:

Kwanza, msingi unaotakiwa katika mchezo wa ngonjera ya kuchekesha ni imara, msingi huo ni uhodari wa kuongea, kuiga, kuchekesha na kuimba. Kati ya michezo anayoonesha, baadhi ni ya jadi na baadhi ni michezo aliyotunga mwenyewe ambayo ameingiza vichekesho alivyopata kutoka kwenye maisha halisi ya sasa. Kwa hiyo licha ya kuwa anaendelea kuwa na wasikilizaji wa zamani, pia amewavutia wasikilizaji vijana.

Pili, uhai wa mchezo wa ngonjera ya kuchekesha ni vichekesho na dhihaka. Guo Degang anathubutu kukosoa hali mbaya ya jamii kwa vichekesho, aliwahi kudhihaki hata baadhi ya waongozaji wa filamu na waigizaji nyota filamu. Hii ni moja ya sababu za kuwavutia wasikilizaji vijana.

Tatu, Guo Degang hataki kuonesha michezo yake kwenye televisheni kama wachezaji wengine wanavyofanya, bali anafanya maonesho mbele ya wasikilizaji uso kwa uso katika majumba madogo, na kuwafanya wacheke hata matumbo yawaume.

Kwa kifupi, ngonjera ni burudani ya kuchekesha tu wala sio mahubiri ya mambo ya siasa. Bw. Guo Degang alisema, "Watu wanakata tikti na kusikiliza mchezo wangu sio kwa ajili ya kufundishwa mambo ya siasa bali kwa ajili ya kufurahishwa."

Profesa Wu Wenke wa taasisi ya michezo ya sanaa alisema kuibuka kwa akina Guo Degang ni matokeo ya mazingira bora ya uhuru wa aina tofauti za utamaduni. Alisema, "Hali hii inaonesha kuwa katika mazingira ya soko huria nchini China, mchezo wa ngonjera ya kuchekesha umeanza kuwa na maonesho ya aina mbili, moja ni ya televisheni na nyingine ni ya kwenye majumba, na vijana wanapenda zaidi mchezo wa aina ya Guo Degang, mchezo unaoneshwa mbele ya wasikilizaji uso kwa uso."

Profesa aliongeza kuwa, hali ya kupendwa kwa mchezo wa Guo Degang haimaanishi kuwa hali iliyodidimia ya mchezo wa aina hiyo imetoweka. Ustawi wa ngonjera unataka wachezaji wa mchezo huo kama akina Guo Degang wawe wengi zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2007-05-07