Mji wa Hangzhou uliopo mashariki mwa China unasifiwa kuwa ni mji ulio kama peponi. Mji huo ni mji wa kale, ambapo Ziwa Xihu lililoko katikati ya mji huo linaufanya mji huo uonekane kuwa na utulivu zaidi. Ndiyo maana, watu wanaoishi katika mji huo wanaona burudani za utulivu zaidi.
Niliwahi kwenda Hangzhou mara kadhaa, kila mara vivutio vya mji huo hugusa hisia zangu na kunivutia sana. Wakazi wa mji huo uliopo pwani ya mashariki ya China wanajivunia na kuona fahari kwa mji wao. Bwana Wang Guoping alisema:
Hangzhou ni moja kati ya miji mikuu iliyokuwa maarufu katika enzi za kale za China. Mji huo una historia ndefu sana na utamaduni unaong'ara. Mji huo ni mji wa utalii unaojulikana duniani, vivutio vyake zaidi ya 100 vimetapakaa katika sehemu ya Ziwa Xihu. Katika miaka ya hivi karibuni, mji huo ulipewa tuzo ya "sehemu mwafaka zaidi kwa maisha ya binadamu" iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, na kusifiwa na jumuiya husika ya kimataifa kuwa ni mji wa bustani duniani.
Ukienda mjini Hangzhou utaona kuwa popote unapokwenda unakuwa kama umezungukwa na Ziwa Xihu lililoko katikati ya mji huo, ziwa hilo ni kama roho ya mji huo. Eneo la ziwa hilo ni kilomita 6 za mraba, ambapo kuna kumbukumbu nyingi za kale zinazoonesha historia na utamaduni wa mji huo. Pamoja na mandhari yake nzuri kumbukumbu hizo zinawavutia watalii wengi kung'ang'ania huko. Mwongozaji wa watalii Bibi Zhang Qing kila mara anapowasimulia watalii hali ya Ziwa Xihu, anasema ziwa hilo haliwezekani kusimuliwa ipasavyo kwa maneno.
Ziwa Xihu la Hangzhou lina historia ndefu ya zaidi ya miaka 2000. Kwenye ziwa hilo kuna visiwa vitatu, pamoja na makingo matatu ya Suti, Baiti na Yanggongti. Suti lilipewa jina la kingo la wapenzi, kwani kingo la Suti ni refu zaidi kuliko mengine mawili, urefu wake ni kilomita 2.8. Kwenye kingo la Suti kuna madaraja 6, mandhari ya huko ni nzuri sana, na maumbile yake ya mimea yana mtindo pekee, maua ya aina mbalimbali tofauti na majani. Wachumba wawili wawili wa mji huo wanapenda sana kutembelea kwenye kingo hilo.
Watu wengine wengi wanapenda kupanda meli kutembea kwenye ziwa, na wengi wanapenda kupanda kisiwa cha Santanyinyue kujiburudisha na mazingira ya maumbile ya huko.
Kisiwa cha Santanyinyue kiko kwenye ncha ya kusini ya Ziwa Xihu, ambapo kuna minara mitatu ya mawe yanayoelea kwenye ziwa, kisiwa hicho kimekuwa na historia ya zaidi ya miaka 400. Kila mnara una urefu wa mita mbili, ncha ya mnara inaonekana kama kibuyu, mnara mwenyewe unaonekana kama ni mpira, juu yake kuna matundu matano madogo, na michoro ya nakshi. Kila ifikapo usiku wa mbalamwezi, watu wakiwasha mshumaa ndani ya mnara, na kufunika matundu juu ya mnara kwa karatasi nyepesi, ambapo vivuli vya mnara, mawingu na mwezi vinaweza kupatana na kuonekana mwanga murua wa mshumaa, maji ya ziwa na mwanga wa mbalamwezi, kisiwa cha Santanyinyue kinajulikana sana.
Mbali na vivutio vya utalii, mjini humo kuna maduka mengi, mikahawa, baa za bia, chai na kahawa. Mji wa Hangzhou ni mji mwafaka kwa maisha ya watu, wakazi wa mji huo wamezoea maisha ya utulivu ya mji huo, na wengi wao hawapendi kuondoka mji huo daima.
Idhaa ya Kiswahili 2007-05-07
|