Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-09 20:06:57    
Usalama kwenye mtandao wa Internet kuwa suala linalofuatiliwa nchini China

cri

Mtandao wa Internet unaleta mabadiliko katika maisha ya kila mtu. Nchini China, asilimia 10 ya idadi ya jumla ya watu, yaani watu milioni 130 wanatumia mtandao wa Internet. Teknolojia hiyo inapoleta urahisi kwa kazi na maisha ya watu, pia imeleta usumbufu kadha wa kadha. Kirusi kilichotokea hivi karibuni kinachoitwa "Xiongmaoshaoxiang" (Panda awasha udi) kiliwahangaisha watumiaji wengi wa kompyuta na makampuni ya software zinazojishughulisha na kazi za virusi nchini China. Kwa hivyo tunapaswa kufanya nini ili kulinda usalama kwenye mtandao wa Internet?

Gazeti moja la teknolojia ya mawasiliano lililotolewa hivi karibuni linaona kuwa, kusambazwa kwa kirusi hicho ni moja ya matukio mabaya zaidi yaliyotokea kwenye mtandao wa Internet nchini China katika mwaka 2006.

Kompyuta ikiambukizwa kirusi hicho, nyaraka zote kwenye kompyuta hiyo zitaonesha picha ya panda mmoja akiabudu, na kompyuta itaweza kujizima na kujiwasha mara kwa mara, hata hard disk yake itaweza kuharibika. Mbali na hayo, kirusi hicho pia kinaweza kuenezwa kwenye mtandao wa Intranet na kuziambukiza kompyuta zote zilizounganishwa kwenye mtandao huo, hatimaye mtandao mzima utaharibika. Mpaka wakati kirusi hicho kinagunduliwa, mamilioni ya kompyuta binafsi, na mitandao ya Intranet ya makampuni ilikuwa imeambukizwa na kuharibika. Bw. Dong ni mhandisi wa software, kazi yake haiwezi kuepukana na kompyuta, lakini aliwahi kusumbuliwa sana na kirusi hicho. Bw. Dong alisema,

"kazi yangu ni kusanifu program, kuna miradi mingi ya software kwenye kompyuta yangu. Baada ya kuambukizwa kirusi hicho, watumiaji wengine wakitumia software hizo kwenye tovuti, kompyuta zao pia zitaambukizwa pia."

Naibu maneja wa kituo cha utafiti cha kampuni ya teknolojia ya Rising ya Beijing Bw. Ma Jie alipoeleza njia ya kuenea kwa kirusi hicho alisema, kompyuta za watengeneza tovuti au wasimamizi wa tovuti fulani zikiambukizwa kirusi hicho, kirusi kitajipenyeza kwenye nyaraka za tovuti zilizopo kwenye kompyuta hizo, lakini kwa kuwa kirusi hicho ni programu ndogo sana, ni vigumu kugunduliwa. Na kama watengeneza tovuti wakiweka nyaraka hizo kwenye tovuti, basi tovuti nzima itaambukizwa kirusi hicho. Bw. Ma Jie alisema,

"ufumbuzi mmoja uliotolewa na kampuni ya Rising ni kufanya usimamizi wa jumla kwenye server za Intranet, ili kupunguza uwekezano kwa makampuni kuambukizwa kirusi hicho."

Kutokana na takwimu zisizokamilika, hivi sasa duniani kuna virusi vya kompyuta zaidi ya elfu 80, na kila mwaka idadi hiyo inaongezeka kwa elfu 20. Watu wanaoshambulia mtandao wa Internet kwa kutumia virusi wanaitwa 'Hackers' kwa Kiingereza. Baadhi yao wanafanya hivyo kwa ajili ya faida za kiuchumi, baadhi hayo wanalipiza kisasi kwa jamii, wengine wanataka kuonesha tu uwezo wao. Hivyo ni vipi watumiaji wa kawaida wa internet wanaweza kugundua virusi na kuepuka data za kompyuta zisiharibike?

Bw. Ma Jie alisema suala hilo linaweza kutatuliwa kwa kutumia teknolojia ya Virtualization, yaani kutumia software kuumba nakala ya mfumo wa kompyuta ambayo ina uwezo sawa na mfumo wa asili, kwa hivyo virusi vitadanganywa na kushambulia nakala hiyo.

Meneja mkuu wa kituo cha usalama wa uhandisi wa ujuzi cha Beijing (Beijing Knowledge Security Engeering Center, PKSEC) Bw. Wang Xinjie anaona kuwa, kutatuliwa kwa suala la usalama kwenye mtandao wa internet kunahitaji kujenga mfumo kamili wa usimamizi wa usalama wa mtandao wa internet, utaratibu wa hivi sasa hauwezi kutatua kimsingi suala hilo. Mtandao pia unahitaji mfumo kamili wa kinga kama binadamu. Bw. Wang Xiejie alisema:

"ya kwanza ni kuzuia matatizo yasitokee, ya pili ni kuzingatia hali ya jumla, na kuchambua hatua gani zinaweza kukidhi mahitaji hayo."

Ili kukamilisha zaidi mfumo wa usalama wa mtandao, mkakati wa maendeleo ya sekta ya mtandao wa Internet nchini China kwa mwaka 2006 hadi 2020 uliotungwa hivi karibuni, unaagiza kujenga utaratibu wa uhakikisho wa usalama kwenye mtandao wa Internet nchini China na kuinua uwezo wa China kuzuia na kukabiliana na matukio ya usalama kwenye mtandao wa internet.

Mfanyakazi wa kituo cha kuratibu na kushughulikia matukio ya dharura ya mtandao wa kompyuta wa taifa Bi. Ji Yuchun alieleza, matukio ya kawaida ya usalama kwenye mtandao wa internet ni pamoja na maambukizi ya virusi vya Worm na Trojan Horse na virusi vya kubadilisha kurasa za tovuti. Utaratibu wa uhakikisho wa usalama wa mtandao wa Internet unalenga kukabiliana na matukio kama hayo, na hatua mbalimbali za kiteknolojia zitachukuliwa ili kupunguza harasa na athari kwa watumiaji wa Internet. Bi. Ji Yuchun alisema:

"kwa mfano, utaratibu huo ni kama kikosi cha zimamoto, wakati maafa ya moto yakitokea, utakwenda kwenye sehemu zilizotokea maafa, kuchunguza hali halisi ya maafa, halafu utaweka mpango na hatimaye kuzima moto."

Mwanachama wa taasisi ya uhandisi ya China Bw. Fang Bingxing alisema, kutokana na kuwa washambulizi kwenye mtandao hutafuta shabaha mpya, hivyo kufuatilia matukio ya mashambulizi hayo, na kuchunguza umaalum wake na kubuni bidhaa au mbinu za kukabiliana na matukio hayo, ni kazi za muda mrefu.