Kwenye mkutano wa mwaka wa baraza la Asia la Boao uliofungwa hivi karibuni, usalama wa nishati kwa Asia ya mashariki ulikuwa ni suala lililofuatiliwa na watu waliohudhuria mkutano huo. Maofisa na wanaviwanda wa nchi nyingi za Asia ya mashariki waliona kuwa, hivi sasa malimbikizo ya nishati kwa Asia ya mashariki siyo mengi yasiyo na kikomo, lakini mahitaji ni makubwa. Hivyo nchi mbalimbali za Asia ya mashariki ni lazima ziimarishe ushirikiano wa nishati, ili kuhakikisha usalama wa nishati kwa sehemu hiyo.
Hivi sasa Asia ya mashariki ni moja ya sehemu inayotumia mafuta na gesi kwa wingi duniani, lakini malimbikizo ya nishati ya sehemu hiyo siyo mengi yasiyo na kikomo, hivyo inategemea sana nishati ya nje. Ripoti iliyotangazwa hivi karibuni na Deloitte & Touche, ambayo ni kampuni kubwa kabisa ya utoaji ushauri kuhusu mambo ya usimamizi duniani inaonesha kuwa, sehemu ya Asia ya mashariki inahitaji asilimia 30 ya nishati duniani, lakini inatoa asilimia 10 tu ya nishati duniani, kwa kuwa Asia ya mashariki ambayo uchumi wake unakua kwa kasi unakabiliwa na tishio la upungufu wa nishati, hivyo kuhakikisha usalama wa nishati kumekuwa ni suala muhimu linalokabili nchi mbalimbali za Asia ya mashariki.
Naibu mkurugenzi wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa ya China Bw. Chen Deming kwenye baraza hilo alitoa mwito kuwa, ni lazima nchi za Asia ya mashariki zianzishe utaratibu wenye ufanisi zaidi wa usalama wa nishati, ili kukabiliana kwa pamoja na suala la usalama wa nishati. Alisema
"Tunapaswa kuweka mfumo mpya wa usalama wa nishati wa kunufaishana, na China pia inapaswa kushiriki katika mfumo huo. Licha ya ushirikiano wa uendelezaji wa maliasili, pia tutachunguza pamoja namna ya kusafisha nishati na kuinua ufanisi wa nishati, na kusaini makubaliano ya pande mbili mbili au pande nyingi kati ya serikali na kufanya majadiliano."
Imefahamika kuwa, China ni nchi ya pili inayotumia mafuta kwa wingi duniani, pia ni nchi ya tatu inayoagiza mafuta kwa wingi. Baada ya mwaka 2001, katika hali ambayo bei ya mafuta duniani kuendelea kupanda juu na uchumi wa China kuongezeka kwa kasi, utoaji wa mafuta nchini China uko katika hali ya kubanwa kwa muda mrefu. Hivyo kuepusha kupungua kwa utoaji wa mafuta na athari mbaya zinazoletwa na kubadilika sana kwa bei ya mafuta kumekuwa lengo muhimu la usalama wa nishati wa China.
Bw. Chen Deming alisema, kufanana na nchi nyingi duniani, China itajenga malimbikizo ya kimkakati ya mafuta ili kukabiliana na hali ya dharura itakayoweza kutokea ghafla. Alidokeza kuwa hadi kufikia mwaka 2010, malimbikizo ya kimkakati ya mafuta ya China yatakuwa sawa na uagizaji wa mafuta ya siku 30 kutoka nchi za nje. Kiasi hiki ni cha chini sana ikilinganishwa na malimbikizo ya mafuta ya Japan na Korea ya Kusini ya hivi sasa, ambayo ni sawa na uagizaji wa mafuta wa siku 90 kutoka nje. Habari zinasema China imeunda ofisi ya malimbikizo ya mafuta, na kuanza kujenga vituo vinne vya kwanza vya kulimbikiza mafuta ya kimkakati.
Bw. Chen Deming alisema katika hali ya upungufu wa nishati, China inatumai kuimarisha ushirikiano kati yake na nchi mbalimbali za Asia ya mashariki. Kwa mfano, kutokana na mpango wa maendeleo ya kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia wa China, mwaka 2020 uwezo wake wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa nyuklia utafikia kilowati milioni 40, ambao ni mara 6 wa ule wa hivi sasa. Lakini China inakabiliwa na upungufu wa malighafi ya nyuklia, na ukosefu wa uzoefu wa kushughulikia takataka za nyuklia, hivyo inahitaji kuimarisha ushirikiano kati yake na nchi za Asia ya mashariki katika sekta hiyo.
Imefahamika pia kwamba katika miaka ya hivi karibuni, hali ya wasiwasi wa nishati duniani imesababisha ushindani mbaya wa nchi mbalimbali za Asia ya mashariki katika soko la nishati. Hali hii inazifanya nchi za Asia ya mashariki zenye upungufu wa nishati kuathirika mbaya zaidi katika hali isiyo na utulivu ya soko la nishati duniani.
Kuhusu hali hiyo, Profesa Kim Tai Yoo wa Chuo Kikuu cha taifa cha Seoul alisema, nchi za Asia ya mashariki lazima ziwe na msimamo wa pamoja na sauti moja katika sera ya nishati, ili kulinda utulivu wa bei ya nishati ya kikanda. Alisema:-
"Kwa kuwa hivi sasa hatuna mpango mzuri wa utatuzi wa matatizo, hali hii inatufanya tuwe na ushindani, na kusababisha bei kupanda siku hadi siku. Ushindani wa kikanda ni changamoto kubwa kabisa kwa ushirikiano wa usalama wa nishati duniani. Kama kuna utaratibu unaoweza kufanya nchi zinazotumia mafuta zishirikiane, ili kuepusha ushindani mbaya katika soko la nishati, basi utaratibu huo ni mzuri kuliko ule wa hivi sasa."
Pia alipendekeza kuwa, Asia ya mashariki lazima iunde umoja kama "mfuko wa kutuliza bei ya mafuta", ambao unatoa uungaji mkono wa fedha na teknolojia kwa miradi mikubwa ya nishati endelevu na kulinda nishati mbadala, hii itasaidia kupunguza hatari ya nchi moja kutumia fedha nyingi, na kuhimiza nchi nyingine za Asia kushiriki kwenye miradi hiyo, na kuhakikisha usalama wa nishati barani Asia.
Usalama wa nishati sio tu unahitaji ushirikiano wa nchi mbalimbali, bali pia unahitaji ushirikiano wa viwanda na makampuni. Meneja mkuu wa kampuni ya mafuta ya baharini ya China Bw. Fu Chengyu anaona kuwa, viwanda na makampuni ya nchi za Asia ya mashariki licha ya kuendeleza nishati kwa pamoja, bali pia yanapaswa kuimarisha ushirikiano katika kuinua ufanisi wa matumizi ya nishati, kupunguza matumizi ya nishati, kutafiti na kuendeleza nishati mpya.
"Tunapaswa kupanua ushirikiano kati ya nchi hadi ushirikiano kati ya viwanda na makampuni katika kutafiti teknolojia mpya na nishati mpya, na kupanua utafiti na kuongeza fedha katika nishati mpya, nishati mbadala na nishati endelevu. Uwekezaji wa leo unamaanisha utoaji mwingi zaidi wa kesho."
Hivi sasa ushirikiano wa nishati kati ya viwanda na makampuni ya China, Japan na Korea ya Kusini umeingia katika kipindi halisi. Viwanda na makampuni mengi ya Asia ya mashariki yatafanya kazi ya uendelezaji wa mafuta ya ng'ambo na gesi kwa pamoja, na kuimarisha ushirikiano katika nishati endelevu, usalama na hifadhi ya mazingira. Wataalam walioshiriki kwenye mkutano wa baraza la Asia la Boao waliona kuwa, kwa mtazamo wa muda mrefu, kuunda jukwaa la ushirikiano wa usalama wa nishati ni chaguo la lazima kwa nchi za Asia ya mashariki.
Idhaa ya kiswahili 2007-05-15
|