Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-16 17:03:34    
Asilimia 85 ya watoto wanaohamahama waishio mjini Shanghai wapewa chanjo za kinga maradhi

cri

Tarehe 25 Aprili ilikuwa ni siku ya chanjo kwa watoto nchini China, habari zilizotolewa na idara husika za afya za mji wa Shanghai zinasema, mwaka huu asilimia 99 ya watoto waliozaliwa Shanghai wamepewa chanjo kutokana na mpango wa kukinga maradhi uliowekwa na serikali kuu ya China, na zaidi ya asilimia 85 ya watoto wanaohamahama wanaoishi mjini Shanghai walipewa chanjo hizo.

Serikali ya mji wa Shanghai ilikuwa imehakikisha kuwa itagharamia utekelezaji wa mpango wa kinga maradhi kwa watoto, kuongeza fedha katika utoaji wa chanjo kwa watoto mwaka hadi mwaka, na kufanya juhudi kubwa ili kuwawezesha watoto wote waliozaliwa mjini humo na wanaohamahama wapate haki sawa ya kupewa chanjo bila malipo.

Hivi sasa licha ya chanjo ya ugonjwa wa kifua kikuu, polio, kifaduro, dondakoo na pepopunda, surua na chanjo dhidi ya homa ya maini aina ya B (Hepatitis B), kutokana na mpango wa kinga uliowekwa na serikali, mji wa Shanghai pia umeongeza chanjo mbili dhidi ya magonjwa ya maambukizi ya ugonjwa aina ya B na homa ya uti wa mgongo, na kazi hizo zimechangia sana kuboresha afya ya watoto.

Kwa mfano kutokana na uchunguzi uliofanywa na wizara ya afya ya China, zaidi ya asilimia 50 ya wachina wameambukizwa virusi vya homa ya maini aina ya B, na asilimia 10 ya wachina wanaishi na virusi hivyo. Baada ya mji wa Shanghai kuiweka kazi ya utoaji wa chanjo dhidi ya virusi vya homa ya maini aina ya B kwenye mpango wa kinga maradhi mwaka 1992, watoto walioambukizwa virusi vya homa ya maini aina ya B wamepungua kwa kiwango kikubwa hata kufikia chini ya asilimia moja.

Katika siku ya watoto kupewa chanjo nchini China, licha ya kufanya shughuli za aina mbalimbali za kuwaelimisha wakazi na watu wanaohamahama wa huko kuhusu umuhimu wa kuwapa watoto chanjo, mji wa Shanghai pia ulivishirikisha vituo vya afya vya mitaani kufanya uchunguzi kuhusu hali ya watoto wanaohamahama waishio mjini humo katika wiki mbili ili kila mtoto aweze kupata chanjo hasa chanjo dhidi ya homa ya maini aina ya B na ugonjwa wa ubongo aina ya B.

Kauli mbiu ya siku ya watoto kupewa chanjo nchini China kwa mwaka huu ni "serikali kwenye ngazi mbalimbali zinawajibika kumpa kila mtoto chanjo kwa wakati". Wizara ya afya ya China iliziagiza sehemu mbalimbali na idara husika kufanya shughuli za aina mbalimbali kueneza umuhimu wa watoto kupewa chanjo dhidi ya maradhi yaliyoorodheshwa na serikali, na kuweka mazingira mazuri ya kutoa chanjo kote nchini. Idara husika zimeagizwa kuchukua hatua mbalimbali kufanya uenezi kwenye sehemu wanakoishi watoto wengi wanaohamahama, na idara za kinga na udhibiti za maradhi na kutoa chanjo kwenye ngazi mbalimbali zilitakiwa kwenda katika sehemu za vijijini hasa sehemu za mbali na mijini, na sehemu zilizoko nyuma kimaendeleo kufanya uenezi na kufanya uchunguzi kuhusu watoto wasiopewa chanjo hizo, ili kuzifahamisha familia zote sera ya serikali ya kutoa chanjo bila malipo, na kuwapa watoto wote chanjo husika.

Idhaa ya kiswahili 2007-05-16