Kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha, hivi sasa watu wengi zaidi wa China wanazingatia zaidi hali ya nyumba wanazoishi. Vijana wengi wanaoishi pamoja na wazazi wao wanapenda kumiliki nyumba zao wenyewe.
Kijana Pingping mwenye umri wa miaka 25 alihitimu chuo kikuu muda mfupi uliopita, hivi sasa anafanya kazi kwenye kampuni moja ya matangazo ya kibiashara hapa mjini Beijing. Pingping anaishi na wazazi wake kwenye mtaa uitwao Yongle uliopo magharibi mwa Beijing. Kwenye mtaa huo kuna wakazi karibu elfu 30.
Kijana huyo na wazazi wake wanaishi kwenye nyumba moja yenye mita 60 za mraba, ambayo ilinunuliwa na wazazi wake miaka 9 iliyopita kwa Yuan elfu 30. Pingping ana mpango wa kufunga ndoa na mchumba wake mwaka huu, na anapenda yeye na mke wake waishi peke yao. Kwa hiyo hivi sasa suala la nyumba ni suala kubwa linalomkabili kijana huyo. Alisema "Nyumba ya sasa ni ndogo. Kama nikipanga nyumba, gharama yake si ndogo, kiasi kwamba inalingana na fedha nitakazolipa benki kila mwezi nikinunua nyumba kwa kutumia mkopo, aidha nyumba ya kupanga si nyumba yangu. Baada ya kufikiria suala hili mara nyingi, nikaamua kununua nyumba."
Suala hilo la nyumba lilimkumbusha mama yake Bibi Wu, jinsi suala la nyumba lilivyomtatiza. Alisema katikati ya miaka ya 70 ya karne iliyopita, Bibi Wu alipoanza kufanya kazi alikuwa akiishi kwenye bweni la kiwanda, ambapo wasichana watano hadi sita walipaswa kulala kwenye chumba kimoja. Hadi kufikia mwanzoni mwa miaka ya 80 Bibi Wu alipokuwa amefunga ndoa, yeye na mume waliwahi kuishi kwenye chumba kilichoko chini ya nyumba na nyumba ya muda. Baada ya miaka mingi wanandoa hao walipata nyumba yao waliyopewa na kiwanda.
Kuhusu mpango wa mtoto wake wa kununua nyumba, mama huyo Bibi Wu alisema "Tulipokuwa vijana ilikuwa ni vigumu kwetu kupata nyumba, kununua nyumba kulikuwa ni kama ndoto ambayo hatukuwahi kufikiri. Wakati huo tuliona ni bahati kupata mahala pa kulala. Hivi sasa dunia imebadilika."
Katikati ya miaka ya 1990 mume wa Bibi Wu alipata nyumba kutoka kwenye kiwanda alichokuwa anafanya kazi, mwaka 1998 walinunua nyumba hiyo kwa Yuan elfu 30, gharama hizo nafuu ziliamuliwa na serikali kwa ajili ya watu waliofanya kazi kwa miaka mingi.
Kuhusu suala la nyumba, wakazi wengi wa Beijing walikuwa na maoni yanayofanana na Bibi Wu. Miaka zaidi ya 10 iliyopita, kwa wastani kila mkazi wa mji wa Beijing alikuwa na eneo la nyumba la mita 10 za mraba, hivi sasa eneo hilo limeongezeka na kuzidi mita 20 za mraba.
Akikumbusha jinsi hali ya nyumba ilivyoboreshwa katika miaka 30 iliyopita, Bibi Wu alieleza kuridhishwa kwake. Nyumba anayoishi hivi sasa ina vyumba viwili na jumla ya eneo la mita 60 za mraba, mama huyo alisema nyumba hiyo inatosha. Lakini mtoto wake Pingping ana maoni tofauti, yeye hafurahii kuishi kama wazazi wake. Hivi sasa kijana huyo ana pilika pilika nyingi ili kujiandaa kununua nyumba. Ametafiti habari mbalimbali kuhusu nyumba zilizoko Beijing, ama nyumba zile ambazo ujenzi umekamilika au zile ambazo ujenzi bado unaendelea. Na sasa anachofikiria ni eneo la nyumba anayotaka na jinsi ya kulipa.
Kijana huyo alisema, "Nataka kununua nyumba kubwa kadiri niwezavyo. Kununua nyumba si jambo dogo, nataka kupata nyumba ninayoridhika nayo. Kuhusu ulipaji wa mkopo, ni mzigo mkubwa kweli, lakini nitajaribu kubana matumizi. Aidha kampuni yangu imeshiriki kwenye bima ya nyumba, pia inatoa ruzuku, hivyo itanisaidia kupunguza mzigo wangu wa kulipa mkopo."
Mama alimshauria Pingping anunue nyumba yenye eneo la wastani na kuboresha hali ya nyumba hatua kwa hatua kadiri uwezo wake unapoongezeka. Sababu ya mama yake ni kwamba, kununua nyumba kunalenga kuinua maisha, lakini ukinunua nyumba kubwa ambayo gharama yake inazidi uwezo wako, kiwango cha maisha kinapungua kutokana na kuwa unapaswa kulipa kiasi kikubwa cha mkopo kila mwezi.
Profesa Dai Jianzhong wa Taasisi ya sayansi ya kijamii ya Beijing alieleza kuwa, familia ya Bibi Wu inaweza kutuonesha jinsi suala la nyumba lilivyoendelea katika miongo kadhaa iliyopita. Alisema "Kutoka uchumi wa mpango mpaka kufuata sera ya mageuzi na kufungua mlango, halafu kuanzisha na kukamilisha uchumi wa soko huria, hivi sasa maisha ya watu yameinuka sana. Mfano mmoja ni nyumba."
Hivi sasa kununua nyumba bado ni mzigo mkubwa kwa wakazi wa kawaida wa Beijing. Gharama kubwa za nyumba kuliko uwezo wa wanunuzi ni miongoni mwa matatizo yanayowasumbua wateja. Hivi sasa katika miji mikubwa na ya wastani nchini China, bei ya nyumba inaongezeka mara kwa mara. Katika mji mkuu Beijing, mwaka jana bei ya nyumba iliweka rekodi mpya ya kuongezeka kwa asilimia zaidi ya 10 kwa miezi 7 mfululizo, ongezeko hilo liliongoza kati ya miji mikubwa ya China. Kwa mfano katika eneo la makazi wanakoishi Pingping na wazazi wake, nyumba mpya ziliuzwa kwa Yuan elfu 4 kwa mita moja ya mraba miaka mitatu iliyopita, lakini sasa bei imekuwa maradufu.
Bei ya juu ya nyumba inaweza kuathiri utulivu wa uchumi wa taifa na maisha ya wananchi. Suala hilo sasa linafuatiliwa sana na serikali ya China. Ili kuzuia bei ya nyumba isipande kupita kiasi, mwaka jana serikali ya China ilitoa sera mbalimbali za kuimarisha udhibiti wa soko la nyumba. Mwaka huu serikali imetoa hatua kadhaa kuhusu nyumba zinazowalenga watu wenye pato la chini. Meya wa mji wa Beijing Bw. Liu Qi hivi karibuni alisema, serikali itajenga nyumba zenye bei nafuu za mita milioni 200 za mraba ndani ya miaka mitatu ijayo, ili kuzuia kupanda kupita kiasi kwa bei ya nyumba na kukidhi mahitaji ya wakazi wanaotaka kuboresha hali ya nyumba.
Ni baada ya muda fulani sera na hatua hizo za serikali zitaweza kuleta manufaa halisi, lakini kijana Pingping hawezi kusubiri, kwani anataka kufunga ndoa mwaka huu. Ameamua kununua nyumba mpya yenye vyumba viwili na eneo la mita 100 za mraba, iliyoko karibu na nyumba ya wazazi wake.
Idhaa ya kiswahili 2007-05-17
|