Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao tarehe 16 huko Shanghai alisema kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika kunatakiwa kuvumbua wazo jipya ili kuinua kiwango cha ushirikiano, na kupata maendeleo na manufaa kwa kila upande.
Bw. Wen Jiabao alisema hayo kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka 2007 wa baraza la benki ya maendeleo ya Afrika. Mkutano wa mwaka 2007 wa Baraza la Benki ya maendeleo ya Afrika ulifunguliwa tarehe 16 Mei huko Shanghai, China. Kwenye ufunguzi wa Mkutano huo, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alisema, kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika kunapaswa kuhusisha msaada wa serikali na ushirkiano wa viwanda, kuzingatia zaidi ujenzi wa mradi inahusu maslahi ya umma, kutilia maanani ushirikiano wa teknolojia na kuwaandaa watu wenye ujuzi, ili kuzinufaisha kihalisi nchi za Afrika na wananchi wake.vilevile Bw. Wen Jiabao alitoa mwito wa kuitaka jumuiya ya kimataifa iisaidie Afrika kuongeza uwezo wa kujiendeleza, na kutimiza maendeleo endelevu ya uchumi na jamii.
Benki ya maendeleo ya Afrika ni benki kubwa kabisa ya kikanda barani Afrika, lengo lake ni kusukuma mbele maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi wanachama wake barani Afrika. Kauli mbiu ya Mkutano huo wa mwaka ni: "Afrika na Asia: washirika wa maendeleo", Mkutano huo ulijadili hasa ujenzi wa miundo mbinu barani Afrika, utandawazi wa uchumi wa kikanda na kuondoa umaskini. Vyombo vya habari vinaona kwa kauli moja kuwa, Mkutano huo wa mwaka utakuwa ni Mkutano mkubwa kabisa katika historia ya Benki ya maendeleo ya Afrika. Mkuu wa Benki ya maendeleo ya Afrika Bwana Donald Kaberuka alitoa hotuba kwenye ufunguzi akisema:
Mawasiliano ya kiuchumi kati ya Afrika na Asia yameanzia tangu enzi na dahari, ambayo yameendelezwa kwa kasi katika miaka mitano iliyopita. Bara la Asia likiwa ni soko lenye ongezeko kubwa kabisa duniani, maendeleo yake yameleta changamoto kwa Afrika, pia yameleta fursa na uhimizaji kwa nchi za Afrika. Mkutano huo wa mwaka umeleta fursa kwa Afrika na Asia kubadilishana uzoefu na kuendeleza zaidi uhusiano wa kiwenzi.
Kwenye ufunguzi wa Mkutano, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao amesifu sana kuitishwa kwa Mkutano huo wa mwaka, akisema:
Katika zaidi ya miaka 40 iliyopita tangu Benki ya maendeleo ya Afrika ianzishwe, benki hiyo imefanya juhudi zisizolegea kusukuma mbele maendeleo ya uchumi na jamii ya Afrika, na kupata mafanikio dhahiri. Katika miaka miwili iliyopita, Benki ya maendeleo ya Afrika imesukuma mbele mageuzi yake na kujitahidi kutafuta njia mpya ya kutoa huduma bora zaidi kwa nchi za Afrika. Kuitishwa kwa Mkutano huo hakika kutaendelea kuhimiza ujenzi wa benki hiyo yenyewe, na kuongeza zaidi umuhimu na ushawishi wake.
Katika miaka ya hivi karibuni, uchumi wa Afrika umeongezeka kwa nguvu, na jamii za nchi za Afrika zinaendelea siku hadi siku, ambapo nchi za Afrika zinapiga hatua imara kwenye njia ya usitawishaji wa uchumi, lakini jukumu la maendeleo ya uchumi na jamii za nchi za Afrika bado ni kubwa.
China ikiwa moja kati ya nchi za jumuiya ya kimataifa, siku zote inajitahidi kuzisaidia nchi za Afrika. Katika zaidi ya miaka 50 iliyopita, China imezisaidia nchi za Afrika kufanya ujenzi wa miradi zaidi ya 900 ya miundo mbinu na miradi inayohusika na maslahi ya umma.
Mkutano huo wa kimataifa umeandaliwa na Benki ya umma ya China na serikali ya Mji wa Shanghai, ambao ni Mkutano mwingine kuhusu masuala ya Afrika unaoandaliwa na China baada ya Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika. Mkuu wa Benki ya maendeleo ya Afrika Bwana Donald Kaberuka alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari huko Shanghai alifurahia China kuandaa Mkutano huo wa mwaka wa Benki ya maendeleo ya Afrika. Alisema:
Umuhimu wa kuitishwa kwa Mkutano huo ni sehemu inayofanyika mkutano huo, na wakati wa kufanyika kwa Mkutano huo. Hivi sasa uhusiano kati ya China na Afrika uko katika wakati muhimu. Kuitishwa kwa Mkutano huo kumeleta fursa ya kuendeleza uhusiano kati ya Afrika ya China kwenye kiwango kipya. China ni nchi inayoendelea kwa kasi zaidi kuliko nchi nyingine duniani, vilevile ni soko lenye maendeleo ya haraka kabisa duniani. Benki ya maendeleo ya Afrika inataka kushuhudia namna gani China inavyopata maendeleo hayo. Tunapenda kufuata mwelekeo uliothibitishwa kwenye Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Afrika na China.
Benki ya maendeleo ya Afrika iliyoanzishwa mwaka 1964 ni benki kubwa zaidi barani Afrika, ambayo ina nchi wanachama 77, miongoni mwake nchi 53 ni za Afrika na nyingine 24 ni nchi zilizo nje ya Bara la Afrika zikiwemo pamoja na China, Japan, Korea ya kusini na India. Kufanyika kwa mkutano wa mwaka huu wa benki hiyo katika hali ambayo makampuni mengi zaidi za China, India na nchi nyingine za Asia yanashiriki zaidi siku hadi siku katika shughuli zinazohusiana na maendeleo ya Bara la Afrika.
Kuanzia mwaka 1995, uchumi wa Afrika umepata ongezeko la zaidi ya asilimia 3 katika miaka 12 iliyopita. Uchumi wa Afrika umeingia katika kipindi cha maendeleo endelevu na ongezeko la utulivu. Bwana Kaberuka alisema, maendeleo ya uchumi wa Afrika yanasukumwa na uwekezaji wa moja kwa moja wa China na nchi nyingine duniani. Alisema:
Thamani ya uwekezaji wa China barani Afrika inakadiriwa kufikia dola za kimarekani bilioni 2 kwa mwaka. Benki ya maendeleo ya Afrika inataka kuona vitega uchumi kutoka China kwa Afrika vitaendelea kuongezeka. Katika miaka 6 iliyopita, thamani ya biashara kati ya Afrika na China imeongezeka mara 5, na Benki ya maendeleo ya Afrika inataka kuona ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Afrika na China unaendelezwa siku hadi siku. Na Benki ya maendeleo ya Afrika inapenda kuchangia zaidi maendeleo ya uhusiano kati ya Afrika na China.
Mwaka jana kwenye Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, serikali ya China ilitangaza hatua nane za kusukuma mbele uhusiano wa kimkakati na kiwenzi wa aina mpya kati ya China na Afrika. Na kabla ya kufunguliwa kwa Mkutano wa mwaka wa Benki ya maendeleo ya Afrika, naibu waziri wa biashara wa China Bwana Wei Jianguo ameziahidi tena nchi mbalimbali za Afrika kwamba, serikali ya China inatilia maanani sana utekelezaji wa hatua hizo. Serikali ya China inapenda kushirikiana na nchi mbalimbali za Afrika katika kuboresha kiwango cha matibabu na elimu, kupunguza umaskini na kutimiza malengo yote ya maendeleo ya uchumi na jamii.
Idhaa ya kiswahili 2007-05-18
|