Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-23 16:06:08    
Mtunzi wa muziki wa kabila la Wa-mongolia Bwana Yong Rubu

cri

Wimbo "Mlima Tuguleji" ulitungwa na Bwana Yong Rubu ambaye pia ni mtunzi maarufu wa muziki wa kabila la Wa-mongolia. Unaposikia wimbo huo unaweza kuona kama unatembelea kwenye mbuga mkubwa wenye kondoo wengi weupe waliotapakaa hapa na pale.

Bwana Yong Rubu alizaliwa kwenye mbuga mzuri wa Kerqin wa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, ambako ni maskani maarufu ya nyimbo na ngoma ya kabila la wamongolia. Kutokana na kuathiriwa na muziki wa huko, Bwana Yong Rubu alikuwa anapenda sana muziki tangu utotoni mwake, alipokuwa na umri wa miaka 14 alijiunga na jeshi na kuwa askari wa michezo ya sanaa. Baada ya miaka minne, alitumwa kujifunza muziki katika chuo kikuu cha fasihi na sanaa cha Luxun cha Kaskazini mashariki cha China. Baada ya kuondoka jeshini Bw. Yong Rubu alianza kufanya kazi kwenye kikundi cha michezo ya sanaa cha Radio na Televisheni cha Mongolia ya ndani akiwa mwongozaji wa bendi na mtunzi wa muziki. Alisema:

"Muziki wa kabila la wamongolia una historia ndefu na umaalum wake wa kipekee, na bado una nafasi kubwa ya kuendelezwa. Hivi sasa natunga muziki wa simfoni na muziki wa mchezo wa ngoma, na nyimbo za kwaya ili kuwafahamisha zaidi walimwengu undani wa muziki wa kabila la Wamongolia."

Bwana Yong Rubu ambaye ni mzaliwa wa huko, alikuwa akijifunza kwenye mabanda ya maturubai ya wafugaji, wasanii wenyeji walikuwa walimu wake, mbuga, jangwa na misitu, vyote ni chimbuko la utungaji wake wa muziki. Aliwahi kutunga nyimbo nyingi za kabila la Wamongolia zinazoambatanisha umaalum wa kikabila na hali ya kisasa. Ufuatao ni wimbo wa kwaya aliotunga unaoitwa "ngamia mweupe aliyekaa kwa upweke".

Wimbo huo ulitumia mpangilio maalum wa sauti za muziki wa kabila la wamongolia kwa ajili ya kuonesha kidhahiri upweke wa ngamia mdogo aliyempoteza mama yake. Kikundi cha michezo ya sanaa cha Radio na Televisheni cha Mongolia ya ndani kiliimba wimbo huo kwenye tamasha la pili la kwaya la Olimpiki lililofanyika mwaka 2002 nchini Korea ya Kusini, na kunyakua nafasi ya kwanza ya kwaya ya sauti za mchanganyiko za waimbaji wanawake na wanaume.

Katika miaka mingi iliyopita nyimbo za kabila la wamongolia zilizotungwa na Bw. Yong Rubu kama vile "Majira manne" na "Bahari Nne" ambazo ziliimbwa katika sehemu mbalimbali nchini China na kikundi cha kwaya cha Radio na Televisheni cha Mongolia ya ndani. Mwaka 1989, Bw. Yong Rubu alifanikiwa kufanya maonesho ya kwanza ya upigaji wa muziki wa simfoni uliotungwa na mtunzi pekee wa kabila dogo mjini Beijing nchini China.

Mwezi Oktoba mwaka 2005, Bw. Yong Rubu alitumwa na wizara ya utamaduni ya China kuongoza kikundi chake kufanya maonesho kwenye ufunguzi wa tamasha la utamaduni la China nchini Marekani na kupata mafanikio makubwa. Kwenye maonesho maalum ya kwaya yaliyoandaliwa na Marekani kwa ajili yake, Bw. Yong Rubu si kama tu alikaribishwa sana na wasikilizaji, bali pia alikutana na kusifiwa na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Bwana Powell. Alisema:

"Wasikilizaji wa Marekani wameguswa hisia hata kutokwa na machozi baada ya kusikiliza nyimbo za kwaya. Naibu mkuu wa kituo cha sanaa cha Kennedy alisema, kama kweli mungu yuko, basi yeye pia atatokwa na machozi kutokana na nyimbo zenu, nyimbo zenu kweli ni kama sauti kutoka mbinguni."

Mwaka 1998 maonesho ya kwanza ya kwaya ya China yalifanyika mjini Harbin, kaskazini mashariki mwa China, kikundi cha kwaya kilichoongozwa na Bw. Yong Rubu kilipata mafanikio makubwa kwa ustadi wake mzuri wa uimbaji. Ingawa sasa Bwana Yong Rubu amezeeka, lakini anaendelea kujishughulisha na muziki. Mwaka 2006, alitoa mikusanyiko miwili ya simfoni na kwaya iitwayo "Roho ya Mbuga" na "Nyimbo za Mbuga". Alisema:

"Muziki umefuatana nami kwa maisha yote, mimi hujisikia kwamba jana imeshapita, na kesho maisha mazuri yanatusubiri. Napanga kutunga muziki nyingine 20 za okestra ili kuwaoneshea walimwengu muziki wa kabila la wamongolia wenye umaalum wa Hulunber, Zhelimu, Xilinguole, Erduosi na Alashan."

Wasikilizaji wapendwa mliosikiliza ni wimbo unaoitwa "Unakaribishwa Mbugani". Kama unapenda muziki na utamaduni wa kabila la wamongolia, unakaribishwa kutembelea mbuga za Mongolia ya ndani nchini China, ili ujioone kwa macho yako mwenyewe mahali pazuri penye nyimbo nzuri.

Idhaa ya kiswahili 2007-05-23