Kutokana na kuendelea kwa utandawazi wa miji nchini China, imejitokeza mitaa mbalimbali ya makazi mijini.
Mtaa wa makazi wa bustani ya vijana ni mtaa ulioanzishwa miaka mingi iliyopita huko Jinan, mji wa mashariki mwa China. Mtaa huo wa makazi una eneo lisilozidi kilomita moja ya mraba, lakini kwenye mtaa huo zinaishi familia zaidi ya elfu 6. Nyumba nyingi za huko ni nyumba kongwe, ambazo zina eneo dogo na haizna zana za kisasa, kama vile gesi na vifaa vya kuleta joto. Hata hivyo huu ni mtaa wa makazi wa kwanza katika China Bara uliopewa tuzo ya mtaa wa makazi salama iliyotolewa na shirika la afya duniani WHO.
Tuzo hiyo ilitolewa na shirika la afya duniani mwaka 2006 kutokana na juhudi za kuhakikisha usalama wa makazi zilizofanywa na wakazi wa mtaa huo.
Tangu mwaka 2002 wafanyakazi zaidi ya 40 wa kamati ya wakazi wa mtaa huo walifanya shughuli nyingi ili kuondoa hatari zinazotishia usalama wa mtaa wao mkongwe. Awali kulikuwa na wakazi ambao waliweka matangi ya gesi na majiko kwa pamoja kwenye vyumba vidogo vya kupikia chakula. Hali hii ni hatari sana kwani iwapo gesi ikivuja wakati majiko yanapotumika, itasababisha mlipuko na moto kubwa. Mbali na hayo kulikuwa na hali nyingine zilizoweza kuhatarisha usalama wa wakazi wa huko. Ili kuondoa hali hizo wafanyakazi wote wa kamati ya wakazi walishiriki kwenye mafunzo ya ujuzi kuhusu usalama, halafu waliwatembelea wakazi wa familia moja baada ya nyingine na kuwaelimisha ujuzi huo.
Bw. Dong Chuanshi ni mfanyakazi wa kamati ya wakazi anayeshughulikia mambo ya usalama, alisema "Tuliwafahamisha wakazi ujuzi kuhusu usalama na pia tuliwashirikisha kwenye mafunzo husika ili wafahamu mbinu za kujiokoa wakikabiliwa na hatari. Kazi kuu ya kamati ya wakazi ni kuzuia kutokea kwa hatari."
Kutokana na mafunzo hayo, wakazi wa mtaa huo wa makazi walielimishwa kuhusu ujuzi wa kujikinga dhidi ya hatari, na baada ya muda si mrefu walinufaika na ujuzi huo. Siku moja mzee Yang Dingsheng alisikia harufu mbaya kutoka jikoni, alikumbuka alichofundishwa na wafanyakazi wa kamati ya wakazi siku chache zilizopita, akagundua kuwa harufu hiyo huenda ni gesi inayovuja. Aliwapigia simu mara moja mafundi wa kampuni ya gesi, ambao walifika na kufanya ukarabati kwa haraka. Mzee huyo alifanikiwa kuzuia kutokea kwa ajali.
Bibi Dong Guilan ameishi kwenye mtaa huo kwa zaidi ya miaka 10. Awali alikuwa hafahamu hata kidogo namna ya kujikinga dhidi ya moto, hivi sasa amepata ujuzi mwingi kuhusu usalama. Alisema "Wafanyakazi wa kamati ya wakazi walitutembelea mara tatu mwaka huu na kutufundisha namna ya kujikinga dhidi ya moto. Pia waliwaonesha wakazi wote namna ya kuzima moto, walituelezea namna ya kuzima moto na jinsi ya kujiokoa na kukimbia wakati wa ajali ya moto."
Pamoja na hayo wakazi wa huko walifahamishwa ujuzi mwingine kuhusu kujikinga dhidi ya hatari mbalimbali, kama vile madhara kwa watoto yasiyotarajiwa, matumizi ya mabavu kwenye familia na ajali za barabarani.
Si kama tu wafanyakazi wa kamati ya wakazi wanajitahidi kuwaandaa wakazi wa mtaa huo mazingira mazuri ya kuishi, bali pia wakazi wenyewe wanafanya kwa hiari kulinda na kuboresha mazingira.
Kwenye mtaa mmoja wa makazi uitwao Xinghua Xili hapa mjini Beijing, mkazi mmoja Bibi Wang Zhongping anajitolea kuondoa kinyesi cha mbwa kila siku, na amekuwa akifanya hivyo kwa zaidi ya miaka mitatu.
Mzee huyo alisema "Ni zaidi ya miaka mitatu sasa, kila siku bila kujali siku za joto wala siku za baridi, natoka kuondoa kinyesi cha mbwa. Hivi sasa wakazi wengi wanafuga mbwa, na kinyesi cha mbwa kinaonekana kila mahali. Wazee wanatoka nje kufanya matembezi kwenye bustani, si jambo la kufurahisha kwa wazee kukanyaga kinyesi cha mbwa."
Mzee huyo aliongeza kuwa wenye mbwa wengi walipomwona wanajitolea kufanya kazi ya kuondoa kinyesi cha mbwa, walianza kuchukua mifuko ya plastiki na karatasi ya chooni walipotoka kuwatembeza mbwa wao, na kuweka kinyesi cha mbwa kwenye mfuko na kuiweka kwenye masanduku ya takataka.
Katika mitaa mbalimbali ya makazi mjini Beijing, kuna wakazi wengi kama mzee Wang wanaojitolea kuwahudumia wakazi wenzao. Bw. Li Zhen anaishi kwenye mtaa mmoja wa makazi uliopo magharibi mwa Beijing, anajitolea kuondoa vijikaratasi vya matangazo ya biashara vilivyobandikwa bila kufuata utaratibu. Katika miaka mitatu iliyopita bwana huyo ameondoa matangazo ya namna hiyo zaidi ya laki 4. Na Bw. Du Changan anaishi katika sehemu ya kusini mwa China, kila siku anajitolea kusafisha barabara ndani ya mtaa anakoishi. Vile vile mzee Du Jingrong ambaye ni mkazi wa mtaa mmoja ulioko kaskazini mwa Beijing, anajitolea kuwapelekea chakula cha asubuhi walinzi wa mtaa huo, walinzi hao wanamwita Mama Du kwa heshima.
Hivi karibuni chombo kimoja cha habari cha Beijing kiliandaa kinyang'anyiro cha kuchagua mitaa 10 bora ya makazi ya Beijing. Shughuli hiyo ilishirikisha mitaa zaidi ya elfu moja hapa Beijing, na wakazi zaidi ya milioni 2 wa mji wa Beijing walipiga kura. Bw. Li ni mkazi mmoja aliyepiga kura, alisema "Nini maana ya mtaa bora? Tunaona msingi wake ni wakazi wote kuishi kwenye mazingira yenye masikilizano. Kwa hiyo tunafurahia kushiriki kwenye shughuli hiyo."
Bw. Beiye ni mtaalamu wa masuala kuhusu mitaa, alieleza kuwa awali watu waliona sehemu zinazotumika na watu wote ni za serikali, na hazina uhusiano na watu binafsi. Lakini kutokana na mageuzi yanavyoendelea kwenye sekta ya makazi, nyumba sasa ni mali ya watu binafsi, na mtaa umekuwa ni mali ya pamoja ya wakazi wote wa mtaa huo. Kwa hiyo watu wanaanza kufanya kazi za kuboresha mtaa wanaoishi kwa hiari. Bw. Beiye alisema "Kwa mfano kama umenunua nyumba mpya, thamani yake inatokana na mazingira ya mtaa. Kwa hiyo watu wakitambua kuwa, uzuri wa mtaa si kama tu unahusiana na hali ya ndani ya nyumba zao, bali pia unahusiana na mazingira ya mtaa mzima, majirani na unahusiana na hali ya masikilizano ya mtaa huo, basi hii itachangia juhudi za kujenga jamii yenye masikilizano."
Idhaa ya kiswahili 2007-05-24
|