Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-28 16:27:30    
Maingiliano ya utamaduni kati ya China na Ufaransa yapamba moto nchini China

cri

Tokea mwanzoni mwa mwezi Aprili hadi mwishoni mwa mwezi Juni, shughuli za maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na Ufaransa zimekuwa zinapamba moto katika miji 14 ya China, shughuli hizo ni pamoja na muziki, mashairi, filamu na picha za kamera.

Mliosikia ni muziki uliopigwa na kundi la muziki wa ala za kugongwa kutoka Lyon Ufaransa, pamoja na ala za muziki za Kichina. Huu ni muziki uliochanganya ala za nchi za magharibi na za Kichina, ni ufanisi wa ushirikiano kati ya wanamuziki wa nchi hizi mbili. Muziki huo uliopigwa katika Ukumbi wa Muziki mjini Beijing ulipigiwa makofi kwa muda mrefu mpaka wanamuziki wakatoa shukrani mara tatu. Mtazamaji mmoja alisema,

"Mtindo wake ni mpya kabisa, licha ya kuwa na mtindo wa jadi wa muziki wa Kichina pia, wamechanganya mtindo wa kisasa. Hii ni mara ya kwanza kwangu kusikia mtindo kama huo."

Mtazamaji mwingine alisema,

"Mtindo wake ni uvumbuzi mpya, hapo kabla niliona ni vigumu kuchanganya ala za jadi za Kichina na ala za nchi za magharibi katika muziki mmoja, lakini muziki huu umechanganywa vizuri."

Muziki wa kale na wa kisasa wa Ufaransa si mgeni kwa wapenda muziki wa China. Tokea mwaka 2004 maingiliano ya utamaduni kati ya nchi mbili yalipoanza, muziki wa Ufaransa uliwahi kuoneshwa mara nyingi nchini China, na michezo ya sanaa ya Ufaransa inawavutia sana watu. Katika Tamasha la Sanaa la "Kukutana mjini Beijing" maonesho ya muziki wa kale, Jazz, picha za kuchorwa na opera kutoka Ufaransa yanachukua nafasi muhimu sana. "Kukutana mjini Beijing" ni tamasha kubwa la kimataifa, mpaka sasa limefanyika mara saba, na watazamaji zaidi ya milioni tatu wamehudhuria.

Kundi la muziki wa ala za kugongwa kutoka Ufaransa karibu kila mwaka linafanya maonesho mjini Beijing katika majira ya Spring na Autumn na kila linapofanya maonesho linapata watazamaji tele. Msimamizi mkuu wa kundi hilo Bw. Gerard Lecointe alipozungumza na waandishi wa habari alisema tokea mwaka 2005 alipoanza kushirikiana na wanamuziki wa China, kila mara anafurahia ushirikiano na kupata wazo jipya la namna ya kupiga muziki. Ufahamu na upendo wa Wachina kuhusu muziki wa Ufaransa ni mkubwa kuliko alivyofikiri zamani.

"Nilipokuwa katika Chuo Kikuu cha Muziki mjini Shanghai, nilitambua kuwa wanafunzi wote wanafahamu muziki wa wanamuuziki wakubwa wa Ufaransa Mozart na Debussy. Muziki wa China una utajiri mkubwa na tunaupenda, lakini hatujui namna ya kupiga, kwani mtindo wake ni tofauti kabisa na wa kwetu."

Bw. Gerard Lecointe alisema, kutokana na shughuli nyingi anaweza tu kukaa nchini China kwa wiki moja au mbili tu, muda mfupi kama huo hauwezi kumwezesha kuuelewa undani wa muziki wa Kichina.

Naibu meneja wa Ukumbi wa Muziki mjini Beijing Bi. Zhu Jing alisema, alianza kushirikiana na nyanja ya muziki ya Ufaransa tokea mwaka 2004. Mwaka huu katika shughuli za "Kukutana mjini Beijing" maonesho ya muziki wa Ufaransa yatafanywa katika ukumbi huo. Bi. Zhu Jing alisema, maonesho hayo yanawasaidia Wachina wauelewe zaidi muziki wa Ufaransa. Alisema,

"Kweli kufanya maonesho hayo ni fursa nzuri kwa Wachina kuwafahamu zaidi wanamuziki wakubwa na muziki wa Ufaransa."

Licha ya muziki, maingiliano katika nyanja ya tafsiri yalianza mapema. Katika karne iliyopita wafasiri wengi walitafsiri riwaya nyingi mashuhuri za Ufaransa kwa Kichina. Riwaya ya "Mzee Goriot" iliyoandikwa na Honore de Balzac, riwaya ya "Mwenye Kibyongo katika Kanisa la Mariam" (Hunchback of Notre Dame) iliyoandikwa na Victor Hugo na riwaya nyingine zinajulikana na kusomwa sana nchini China.

Kituo cha utamaduni wa Ufaransa mjini Beijing ni mahali pa kukutana kwa washairi na wasanii wa China na Ufaransa, huko wanaimba mashairi yao kupitia wakalimani, na wengine wanachora picha.

Mshairi wa Ufaransa Bw. Jean-Claude Pinson alianza kufanya utafiti kuhusu China toka miaka ya 70 ya karne iliyopita, anaelewa hali ya sasa na ya zamani ya mashairi ya China, anavutiwa zaidi na mshairi wa China Bw. Bai Juyi aliyeishi katika karne ya nane.

Katika Chuo Kikuu cha Filamu Beijing kinachoandaa waigizaji wa filamu, maonesho ya picha za kamera kwa jina la "Safari ya Utalii" yanawavutia wanafunzi wengi. Mmoja wa wanafunzi hao alisema,

"Maonesho hayo yanawaonesha wanafunzi wa China jinsi Ufaransa ilivyo na jinsi China ilivyo, yanasaidia kufahamisha mila na desturi za maisha ya watu wa nchi hizi mbili."

Profesa wa Chuo Kikuu cha Beijing Dong Qiang alisema, katika miaka miwili iliyopita China na Ufaransa zilifanya shughuli nyingi za maingiliano, na anatumai kuwa maingiliano hayo yataimarishwa zaidi. Alisema,

"Natumai kuwa kutakuwa na watu wengi zaidi wa pande mbili watakaofanya kazi za kimsingi za kuwafahamisha watu wa kila nchi historia, jiografia na siasa ya upande mwingine."

Idhaa ya kiswahili 2007-05-28