Karibuni katika kipindi hiki cha safari nchini China, wasikilizaji wapendwa, mlima wa Manjano uko kwenye sehemu ya kusini ya mkoa wa Anhui, ulioko kwenye sehemu ya kati ya China, Mlima huo unajulikana duniani kutokana na maajabu ya misonobari, mawe na mawingu, na ni moja ya sehemu maarufu za utalii nchini China, hivi sasa mlima wa Manjano umeorodheshwa kuwa mabaki ya utamaduni na maumbile duniani.
Mlima wa Manjano ni sehemu yenye mandhari nzuri ya kimaumbile yenye milima. Sehemu hiyo ina milima 72 ya kupendeza. Watu husema, "mtu ataishiwa shauku ya kuona milima mingine baada ya kuona milima ya Manjano". Ikilinganishwa na milima mingine ya ajabu nchini China, umaalumu mkubwa wa mlima wa Manjano ni kuweko kwa miti mingi ya misonobari kwenye vilele vya milima. Kwenye safu ya milima yenye urefu wa zaidi ya kilomita mia moja, mizizi ya misonobali inaonekana kwenye nyufa za mawe. Jambo linalostaajabisha zaidi ni kuwa, majani yote ya misonobali inayofanana na sindano yanaelekea juu, na kujaa hali ya ustawi mkubwa. Kiongozi wa kamati ya usimamizi ya sehemu ya mandhari ya mlima wa Manjano, Bw. Wang Heng Lai alisema,
"Misonobali ya mlima wa Manjano inaota kwenye urefu wa zaidi ya mita 800 juu ya usawa wa bahari, sehemu ya juu ya miti hiyo ni yenye umbo la bapa, majani yake yote yaelekea juu, hali ambayo inafaa kwake kupata unyevunyevu ulioko katika hewa ya huko. Miti hiyo imesimama kwa wima sana kwenye mazingira mabaya, mizizi ya miti inatoa aina ya kitu cha maji maji inayojulikana kuwa ni organic acid, mawe ya mlima wa Manjano ni granite, ambayo organic acid yake inafanya mawe hayo yayeyuke na kuwa aina ya mbolea kama ya samadi, na mbolea hiyo inafanya misonobali hiyo ikue vizuri zaidi, kwa hiyo tunasema miti hiyo inafaa kukua katika mazingira ya huko."
Kwenye mlima wa Manjano kuna jengo moja kubwa lenye ghorofa linalojulikana kwa jina la "Yuping", ambapo palisifiwa na Bw. Xu Xiake, mtalii maarufu sana wa nchini China katika zamani za kale, kuwa ni mahali pazuri sana pa kuangalia misonobali ya mlima wa Manjano. Kwenye genge la mlima lililoko mkabala na jengo hilo kuna misonobali mitatu maarufu sana inayojulikana kwa "misonobali ya kulaki wageni, kuwa pamoja na wageni na kuwasindikiza wageni". Msonobali wa kulaki wageni ulioko upande wa kushoto wa jengo la Yuping, kwa uchache ulianza kuota zaidi ya miaka 800 iliyopita, moja ya matawi ya mti huo yenye majani mengi yanajitokeza sana kwa nje, yanaonekana kama mwenyeji anayenyoosha mkono wake kukaribisha mgeni wake. Hivi sasa mti huo unachukuliwa kama ni mwakilishi wa misonobali ya ajabu ya mlima wa Manjano, na pia umekuwa alama ya mlima wa Manjano. Msonobali unaojulikana kama ni mti unaokuwa pamoja na wageni, unatazamana na jengo la Yuping, namna kama jitu mmoja lililovalia rangi ya kijani kusimama huko na kuwa pamoja na wageni kuangalia mandhari nzuri ya mlima wa Manjano. Msonobali wa kusindikiza wageni umeota kwa namna yake ya kipekee, matawi yake yameshikamana na mti, na kuelekea chini, jinsi inavyoonekana ni kama kuagana na wageni wanaotembelea huko.
Kiongozi wa kamati ya usimamizi wa sehemu ya mlima wa Manjano Bw. Wang Henglai alisema, misonobali 54 ya kipekee inayoota toka miaka mingi iliyopita kwenye mlima wa Manjano, ikiwa pamoja na mlima wa Manjano vimeorodheshwa kuwa mabaki ya kimaumbile ya duniani. Kuhifadhi vizuri miti hiyo kumekuwa moja ya majukumu muhimu ya sehemu ya mlima wa Manjano. Alisema,
"Msonobali wa kuwalaki wageni wa mlima wa Manjano, ambao unajulikana nchini China na duniani, ni alama ya taifa la China, mti huo unalindwa na mtu maalumu kwa saa 24 kwa siku, hali ambayo haijaonekana katika sehemu yoyote nyingine duniani. Kituo cha uchunguzi wa hali ya hewa kimejengwa karibu na mti wa kuwalaki wageni ili kusimamia hifadhi ya mti huo. Kuhusu misonobali 54 maarufu, kila mti umewekewa faili lake, na miti hiyo inashughulikiwa na mtu maalumu."
Mbali ya misonobali ya ajabu, mlima wa Manjano una mawe mengi ya ajabu yaliyoumbika katika kipindi cha kuyeyuka kwa barafu kwenye historia ya dunia. Mawe ya ajabu ya mlima wa Manjano yataonekana kuwa na maumbo tofauti yakitazamwa kutoka pande mbalimbali. Kwenye kilele cha mlima cha Shixin kilichoko katika sehemu ya mandhari ya Beihai ya mlima wa Manjano, kuna sehemu yenye mandhari inayojulikana kwa jina la "kima anaangalia bahari", kwa kuangalia kutoka mbali, jiwe moja kubwa linalofanana na kima aliyechuchumaa kwenye sehemu ya juu ya genge la mlima, akionekana anaangalia bahari ya mawingu. Wakati mawingu yanapoondoka, kima yule anaonekana anaangalia mandhari ya mashamba ya mji wa Mlima wa Manjano.
Mawe mengi ya mlima wa Manjano ni yenye hadithi nzuri. Inasemekana kuwa mtunzi mashairi wa mashuhuri wa enzi ya Tang aliwahi kufika kwenye mlima wa Manjano. Alipoona mandhari nzuri ya vilele vizuri vya milima kwenye sehemu ya Beihai, alifurahi na kutaka kutunga shairi, alinyanyua kichwa na kuimba shairi. Sauti yake ilimshitua mkuu wa hekalu la msitu wa simba. Mkuu wa hekalu aliposikia kuwa mtu yule ni Li Bai, akafanya haraka kumwagiza mtawa mdogo kuleta pombe iliyotengenezwa kwa maji safi ya chemchemi, watu hao wawili waliketi chini na kujadili mashairi huku wakinywa pombe. Mshairi Li Bai alivutiwa sana na udhati wa moyo wa mkuu wa hekalu, akaandika shairi moja, kisha alitupa brashi ya kuandikia, alimuaga mkuu wa hekalu na kuondoka. Mkuu wa hekalu aliporudi baada ya kumsindikiza Li Bai alipigwa na butwaa, punde tu pale mahali ambapo Li Bai alipotupa brashi ya kuandikia shairi, pakatokea mlima, na brashi ile ikabadilika kuwa mti wa msonobali, ambao unaonekana kama brashi iliyosimamishwa pale.
Kutembea kwenye vilele vya milima vinavyopendeza, watalii wanaburudika kutokana na hewa safi yenye unyevunyevu kidogo. Bw. Wang Lichang aliyezaliwa huko Shanghai na kuishi nchini Canada, alisema mlima wa Manjano ni mahali anapopenda sana kutembelea.
"Wakati nilipokuwa kijana, nilikuwa natamani sana kufika kwenye mlima wa Manjano, lakini sikupata nafasi. Safari hii nimejaliwa kutembelea mlima wa Manjano, ninaona hii ni mabeki mazuri ya kiutamaduni ya urithi wa China, hii ni rasilimali isiyoweza kuzalishwa tena, najivunia sana. Tofauti ninayoona kati ya mlima wa Manjano na sehemu nyingine ni kuwa, mlima wa Manjano unamagenge mengi, tena misonobali inaota kwenye nyufa za mawe ya mlimani."
Mtalii kutoka Japan dada Yuki Suenaga alisema, kutokana na kufanana kwa jadi za utamaduni, watalii wa Japan wanapenda sana kuona milima na mito mikubwa maarufu ya China, hususan mlima wa Manjano na mlima wa Emei ulioko mkoani Sichuan, sehemu ya kusini magharibi mwa China.
Licha ya mandhari nzuri za misonobali na mawe ya ajabu ya mlima wa Manjano, mawingu yaliyo kama maji ya bahari pia yanapendeza sana, lakini kuona madhari hiyo kunategemea bahati ya watalii, sehemu ya mlima wa Manjano ina siku 256 zenye ukungu kwa mwaka, kipindi chenye siku nyingi za ukungu ni kuanzia mwezi Novemba hadi mwezi Mei wa mwaka unaofuata, hususan baada ya kunyesha mvua na kuanguka theluji. Watu wakisimama kwenye kilele cha mlima, wanaona mawingu yanapita miguuni mwao, kwa hiyo mawingu ya huko yanaitwa "bahari ya mbinguni."
Idhaa ya kiswahili 2007-05-28
|