Hivi sasa jamii ya China ni jamii yenye idadi kubwa ya wazee. Kuhakikisha wazee wanakuwa na maisha mazuri ni suala linalofuatiliwa nchini China. Makala hii inaelezea hatua iliyochukuliwa na serikali ya mji wa Wuhan, mji ulioko katikati ya China, ambapo serikali ilitoa fedha za kuwalipa wahudumu wa nyumbani ili wawatunze wazee.
Mzee Xia Lianying mwenye umri wa miaka 86 anaishi peke yake huko Wuhan. Nyumbani kwake, mwanamke mmoja wa makamo alikuwa akipika chakula huku akizungumza na mzee aliyekaa sebuleni. Wasikilizaji wapendwa, labda mnaweza kudhani wao ni mama na mkwe, au mama na binti. Lakini ukweli ni kwamba hawana uhusiano wa damu, na mwanamke huyo wa makamo ni mhudumu wa nyumbani aitwaye Chen Hui ambaye analipwa na serikali kwa ajili ya kumpikia chakula mzee Xia.
Nyumbani kwa mzee Xia, mwandishi wetu wa habari aliona kwenye chumba chenye mita 20 za mraba, kuna samani chache tu kama vile kitanda, kochi, kabati ya nguo na meza, lakini zote zilionekana ni zenye usafi. Mzee Xia alisema "Ni mhudumu wa nyumbani anayesafisha chumba changu. Hivi sasa nimezeeka, siwezi kufanya kazi za nyumbani kama zamani. Na sasa nimepata mtu ambaye ananisaidia, na kuzungumza nami, nafurahi sana."
China yenye watu bilioni 1.3 sasa ni moja kati ya nchi ambazo idadi ya wazee inaongezeka kwa kasi kubwa. Hivi sasa watu wa China wenye umri wa zaidi ya miaka 60 wamefikia milioni 144, idadi hiyo ni nusu ya wazee wa bara zima la Asia. Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2020, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa watu milioni 100. Kutokana na hali hiyo, serikali ya China imezidi kutenga fedha katika shughuli za huduma za jamii, inaanzisha hatua kwa hatua mfumo wa kuhakikisha maisha ya wazee unaowanufaisha watu wengi zaidi, ili wazee waishi kwa raha mustarehe. Katika juhudi hizo, serikali ya China katika ngazi mbalimbali, pia imechukua hatua mbalimbali.
Huko Wuhan anakoishi mzee Xia, mwezi Juni mwaka jana serikali ya mji huo ilianza kutoa huduma iitwayo "serikali inalipia wahudumu wa nyumbani". Kwa mujibu wa mpango husika, serikali ya mji wa Wuhan inatoa fedha Yuan milioni 6 kila mwaka, sawa na dola za kimarekani laki 7.5. Fedha hizo zinatumika kuwaajiri wafanyakazi wanawake waliopunguzwa kazini, ambao wanatoa huduma ya saa moja kila siku kwa wazee wenye umri mkubwa elfu 2 ambao wanaishi peke yao na wanashindwa kujitunza.
Mzee Xia ni miongoni mwa wazee wa kwanza waliotangulia kupata huduma hiyo. Mzee huyo alisema, mhudumu wa nyumbani anayelipwa na serikali si kama tu anamsaidia kufanya kazi za nyumbani, bali pia anapiga gumzo na mzee ili kuondoa upweke wake. Mzee Xia alielezea furaha yake akisema "Nampenda sana. Naona huyo ni mwanamke mzuri ambaye sikumtarajia. Nimefurahishwa sana na hatua hiyo ya serikali."
Wakati mwandishi wa habari alipoongea na mzee Xia, mhudumu wa nyumbani Bibi Chen Hui alikuwa amemaliza kupika chakula na kuweka mlo mezani. Alimwambia mzee Xia ale kabla chakula hakijapoa, naye mwenyewe alikuwa akianza kufagia ndani. Bibi Chen Hui alikuwa akifanya kazi za nyumbani huku akizungumza na mwandishi wa habari, alisema "Mimi na wazee tunashirikiana vizuri na kujenga uhusiano wa karibu sana. Ninawachukulia ni kama wazazi wangu."
Mwanamke huyo alieleza kuwa, kutokana na mpango wa serikali, mhudumu mmoja wa nyumbani anatoa huduma kwa wazee kila mmoja kwa saa moja kwa siku, huduma hizo ni pamoja na kupika chakula, kufua nguo na kusafisha nyumba. Hata hivyo ni kawaida kuwa yeye na wahudumu wengine wa nyumbani wanaongeza muda wa kazi kwani saa moja haitoshi kumaliza kazi zote. Alisema baadhi ya wazee wana hali mbaya ya afya kiasi kwamba wana tatizo la kutembea, kwa hiyo wahudumu wa nyumbani wanakwenda kununua dawa kwa ajili ya wazee na kuwapeleka hospitali kuonana na madaktari, na baadhi ya wakati wanawasaidia wazee kuoga. Bibi Chen Hui aliongeza kuwa, wazee hao wenye upweke wanahitaji sana upendo wa wengine, kwa hiyo wahudumu wa nyumbani wanawahurumia wazee hao na kutozingatia posho wanazolipwa kutokana na kuongeza muda wa kazi.
Mzee Xia alisema kutokana na kutunzwa vizuri na wahudumu wa nyumbani, maisha yake na ya wazee wengine wanaoishi peke yao yamepata urahisi mwingi na wanaona furaha kubwa. Alisema anampenda Chen Hui, iwapo siku moja Chen Hui akichelewa kidogo kufika, mzee huyo anakuwa na wasiwasi, anamsubiri kwenye mlango kama anavyomsubiri binti yake. Na Chen Hui anapofika nyumbani kwake, mzee Xia alikuwa anamshika mkono wake, akimwangalia akiwa na tabasamu.
Mzee Tan Hongzhou pia amenufaika na huduma hiyo, alieleza kufurahia mhudumu wa nyumbani aliyetumwa na serikali. Alisema wazee wanataka serikali iendelee na sera hiyo nzuri. Ni kawaida kwa wazee kukumbwa na shida mbalimbali, inawezekana wanahitaji msaada wa wengine wakati wowote. Kwa kupiga simu tu mhudumu wa nyumbani anakuja mara moja, jambo ambalo hata watoto wao wanashindwa kufanya. Mzee Tan aliimba wimbo mmoja aliotunga akieleza kufurahia hali hiyo.
Idhaa ya kiswahili 2007-05-31
|