Katika kipindi hiki cha leo tunawaletea maelezo kuhusu bustani ya jiolojia yenye maziwa matano yanayopakana mkoani Helongjing, sehemu ya kaskazini mashariki mwa China. Sehemu hiyo inaitwa na wanasayansi kuwa ni "jumba la makumbusho ya volkano" ya dunia kutokana na sehemu hiyo kuwa na volkano nyingi zilizo hai, maziwa matano yanayopakana nchini China pia yalikuwa ya kundi la kwanza yaliyothibitishwa kuwa bustani ya jiolojia ya dunia.
Maziwa matano yanayopakana yako kwenye ukanda wenye volkano zinazolipuka mara kwa mara, na mara ya mwisho ililipuka mwaka 1719, ambayo iliumba jiolojia ya ajabu ya maziwa matano yanayopakana. Baada ya volkano kulipuka, mawe yaliyoyeyushwa kuwa uji uliopoa na kubadilika kuwa mawe ya volkano yenye rangi nyeusi. Wakati ule kulikuwa na mto mmoja uliojulikana kwa mto mweupe, mto huo ulikatishwa na uji ulioganda kuwa maziwa matano yanayopakana, ambayo wakazi wa huko wanayaita kuwa ziwa la kwanza, ziwa la pili, ziwa la tatu, ziwa la nne na ziwa la tano. Naibu mkuu wa jumba la makumbusho ya jiolojia la dunia la maziwa matano Bibi Zhang Lili alisema,
"Maziwa hayo yameungana, chanzo cha maji ya maziwa ni maji yaliyoko chini ya ardhi, ambacho kiko kwenye ziwa la tano, ziwa la tatu ni kubwa zaidi kuliko maziwa mengine manne, maji yakijaa eneo la ziwa hilo linaweza kufikia kilomita za mraba 21.5. Kwetu hapa kuna sehemu moja yenye mandhari nzuri ya maji, ambapo watu wanaweza kusafiri kwa mashua kutoka ziwa la kwanza hadi ziwa la pili bila kipingamizi chochote."
Habari zinasema, ingawa maji ya maziwa matano yanaunga pamoja, lakini kila ziwa kati ya maziwa hayo matano lina umaalumu wake: katika ziwa la kwanza imeota mimea mingi ya yungiyungi, ziwa la pili ni mahali pa kufugia samaki, ziwa la tatu lina eneo kubwa lenye mandhari nzuri zaidi, katika ziwa na nne na ziwa la tano yameota matete (reed), na ni mahali pazuri kwa ndege. Samaki wa maziwa hayo wanapendwa sana na wakazi wa huko. Mkazi mmoja wa sehemu hiyo Bw. Zhao Ming alisema,
"Samaki hao wanaishi katika maji baridi ya chemchemi yenye madini, hivyo wakazi wa hapa wanawaita samaki hao ni samaki wanaoishi katika maji yenye madini. Nyama ya samaki wa sehemu nyingine hazina harufu na ladha nzuri, lakini samaki wa kwetu hapa wanaishi katika maji baridi, hivyo wanakua polepole na wanakua na nyama laini, licha ya hayo maji ya maziwa ya kwetu hapa ni yana silicic acid, samaki wa hapa wakipikwa kwa kutumia maji ya maziwa hayo, ladha yake inakuwa nzuri sana.
Ingawa nyama ya samaki wa huko ni nzuri sana, lakini idara husika ya huko imeweka mpango na kanuni kamili kuhusu hifadhi ya mazingira ya kupatana kwa viumbe ya huko, hivyo samaki hao hawawezi kuvuliwa kiholela. Mkurugenzi wa idara ya utalii ya sehemu ya mandhari ya maziwa matano, Bibi Zhang Lijun alisema,
"Tumeweka mpango kuhusu hifadhi ya mazingira ya kimaumbile, pia kuna kanuni za kuhifadhi bustani ya jiolojia ya dunia, shughuli zetu zote zinaendeshwa kwa kufuata mpango na kanuni hizo zilizowekwa. Kwa mfano katika kipindi cha kuzaliana na kukua kwa samaki wanaoishi katika maziwa matano yanayopakana ya hapa, watu wamekatazwa kabisa kuwavua.
Sehemu iliyoko pembezoni mwa maziwa matano, imesimama milima 14 ya volkano, urefu wake ni kati ya mita 400 na 600 kutoka usawa wa bahari. Volkano 12 kati ya volkano 14 za huko zimekufa kabisa, ambapo nyingine mbili sasa ziko katika muda wa mapumziko. Wakazi wa huko wanaziita volkano hizo mbili kuwa ni mlima mweusi na mlima wa moto. Volkano hizi mbili ni kubwa na ni kamili, hivyo ni kitu cha kwanza ambacho watalii wengi wanaofika huko wanataka kukiona.
Baada ya kupita kwenye njia inayozunguka-zunguka mlimani, ukifika kileleni unaweza kuona mdomo wa volkano, mfano wa chujio kubwa, na pia unaonekana kama ni mdomo mkubwa wa mnyama mkali. Kutazama chini ya mdomo wa volkano, watu wanaweza kupata taswira kuhusu hali ya kulipuka kwa volkano, ambapo milima inaporomoka, ardhi inapasuka na kutoka moshi mnene wenye moto. Wanasayansi wamekadiria kuwa, joto la mawe yaliyoyeyuka linaweza kufikia nyuzi 1,200 kwa kipimo cha Celsius, mawe yaliyoyeyuka yalitiririka kama maji ya moto, hatimaye yalipoa na kugeuka kuwa mawe meusi kwenye sehemu kubwa, ambayo watu wanaiita kuwa bahari ya mawe. Mawe mengi hayo ni yenye alama, ambayo wakati ule yalikuwa yakitiririka, hivyo mawe hayo yamekuwa na maumbo ya aina mbalimbali na kuwaacha watu kuyafikiria wao wenyewe. Kutokana na bahari hiyo yenye mawe ya maumbo mbalimbali, watu wanaweza kupata taswira ya wakati ule wakati mlipuko mkubwa wa volkano ulipotokea.
Kutokana na mlipuko wa volkano, sehemu ya maziwa matano imekuwa na maji mengi mazuri yenye madini chini ya ardhi. Maji ya sehemu ya maziwa matano yanafanana na soda, isipokuwa ni machungu na yana ukali, maji hayo yenye silicic acid licha ya kuweza kunywa, tena yanafaa sana kutumiwa kuoga, kwani maji hayo yana aina zaidi ya aina kumi za madini yanayonufaisha afya ya watu, ambayo yanafanya kazi ya kuponya ugonjwa wa utumbo wa chakula, ugonjwa wa ngozi pamoja na shinikizo kubwa la damu. Bibi Yang mwenye umri wa miaka 77 kutoka mkoa wa Liaoning, sehemu ya kaskazini mashariki mwa China, alikwenda huko mahususi kwa ajili ya kuponya ugonjwa wake kwa kuoga kwa maji ya huko.
"Unalowesha kichwa chako kwenye maji ya hapa, ukitaka kuponya ugonjwa gani?"
"Ninataka kuponya ugonjwa wa shinikizo kubwa la damu."
"Umekuja hapa kwa ajili hiyo tu?"
"Ndiyo."
"Uliambiwa na mtu kuwa, maji ya hapa yanaweza kuponya ugonjwa?"
"Nafahamu toka zamani. Watu wanasema wameona matokeo mazuri ya maji ya hapa."
Kila mwaka kuna watu wengi wanaovutiwa na sifa za maziwa matano yanayopakana, siyo kwa ajili ya kuona mandhari nzuri ya kimaumbile, bali wanakaa kwa siku nyingi katika nyumba ya mapumziko na kuponya magonjwa yao kwa kutumia maji ya chemchemi na matope ya mlima wa volkano. Sehemu ya pembezoni mwa maziwa matano, zimejengwa nyumba za mapumziko zaidi ya 50 zenye vitanda elfu kadhaa. Aidha ili kuwarahisishia watalii, vimejengwa vibanda vya kukinga upepo na mvua kwenye sehemu zinazotoka maji ya chemchemi kwenye sehemu ya maziwa matano, watu wakifungua bomba la maji wanapata maji safi yenye madini.
Idhaa ya Kiswahili 2007-06-04
|