Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-12 15:24:21    
Shirikisho la ushirikiano vijijini mjini Ruian nchini China

cri

Kubaki nyuma kwa maendeleo ya mambo ya fedha siku zote kumekuwa tatizo kubwa linalokwamisha maendeleo ya uchumi wa vijiji nchini China, lakini mjini Ruian mkoani Zhejiang, mashariki mwa China, ukusanyaji wa mitaji sio tatizo tena kwa wakulima wa huko, kwani wanaweza kupata mikopo midogo yenye riba ndogo kutoka kwa shirikisho la ushirikiano vijijini ili kufanya shughuli za uzalishaji.

Bw. Zhu Yingdi mwenye umri wa miaka 40 anaishi katika kijiji cha Zhuaodi mjini Ruian mkoani Zhejiang. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kijiji cha Zhuaodi ni kijiji maarufu cha kutengeneza fagio. Kuna familia zaidi ya 200 kijijini, na zaidi ya nusu ya familia hizo zinaishi maisha kwa kutegemea kazi za kutengeneza fagio. Alisema utengenezaji wa fagio ni kazi ya mikono tu, hivyo ukitaka kuchuma pesa ni lazima kupanua utengenezaji, na wanavijiji ambao hawana fedha za kutosha wanaweza tu kukopa kutoka benki. Lakini zamani kukopa fedha kutoka benki kuna masharti mengi na utaratibu mgumu, hivyo ni vigumu kwa wanavijiji kupata mikopo katika muda mfupi. Sasa wanavijiji wengi wamejiunga na shirikisho la ushirikiano vijijini. Alipozungumzia huduma rahisi ya utoaji mikopo wa shirikisho hilo, alitabasamu na kusema, wanaweza kupata mikopo kwa urahisi. Shirikisho hilo sio tu limerahisisha utaratibu, bali pia riba ya mikopo ni ndogo kuliko zamani.

Shirikisho la ushirikiano vijijini lililotajwa na Bw. Zhu Yingdi ni jumuiya inayotoa huduma mahususi kwa wakulima, linaundwa na shirika la fedha vijijini, shirika la maduka na shirika la shughuli maalum vijijini, mashirika hayo matatu yanatoa huduma za fedha, uuzaji bidhaa kwenye masoko na uelekezaji wa ufundi kwa wakulima. Shirika la fedha vijijini la Ruian pia ni benki ya kwanza ya ushirikiano vijijini katika kijiji hicho. Naibu meya wa mji huo Bw. Chen Lin aliona kuwa, shirikisho la ushirikiano vijijini limetoa njia rahisi kwa wakulima kupata mikopo. Alisema,

"Shirikisho la ushirikiano vijijini lenyewe sio benki, bali ni jumuiya inayoambatana na benki. Kwa upande wa wakulima, kujiunga na shirikisho hilo pia ni njia rahisi ya kupata huduma za fedha zenye ufanisi na urahisi zaidi. Shirikisho hilo ni sawa na benki ya Grameen, yaani lengo letu ni kuwasaidia wakulima, hasa familia za wakulima ambazo maisha yao yako kwenye kiwango cha kati na cha chini vijijini."

Benki ya Grameen iliyoanzishwa na mshindi wa tuzo ya Nobel ya amani Bw. Muhammad Yunus, ambayo inashughulikia utoaji wa mikopo midogo midogo. Benki hiyo inatoa mikopo kwa watu wenye matatizo ya kiuchumi, ili kuwasaidia watu hao hasa wanawake kuondokana na umaskini.

Kama alivyosema Bw. Chen Lin, shirikisho la ushirikiano vijijini lenyewe halitoi mikopo, linatoa huduma za kuthibitisha uwezo wa wakulima wa kurudisha mikopo na kusaidiana kwa kutoa dhamana ya pamoja. Ni kutokana na mashirika hayo matatu kufanya kazi pamoja kuhakikisha mchakato kutoka uzalishaji hadi uuzaji kwenye masoko, uwezo wa wakulima wa kulipa mikopo unaongezwa, pia inawafanya watu kuwa na imani kuhusu dhamana za shirikisho la ushirikiano vijijini.

Bw. Chen Lin alisema, wakulima wa huko wana sifa za uaminifu. Akisema:

"Sisi na benki ya Grameen tuna wazo la namna moja yaani watu maskini sio watu wasiofuata ahadi. Wakulima wakiagiza kitu fulani kwako katika usiku wa manane, ambapo hakukuwepo mtu mwingine, wala hawasaini makubaliano, lakini watakirudisha. Sifa za uaminifu wa wakulima zinafanya kazi muhimu katika eneo wanakoishi. Lakini kutokana na mfumo wetu wa benki, kila kitu kinahitaji kuweka dhamana za hati za mali na kutoa fomu za uhasibu, lakini wakulima hawawezi kutoa vitu hivyo."

Mwaka jana, baada ya shirikisho la ushirikiano vijijini kuanzishwa, mkulima Zhu Yingdi na wakulima wengine wanaotengeneza fagio waliunda kikundi. Wakati mmoja wa wanakikundi hicho anapohitaji fedha, wengine wanatoa dhamana kwake kwa pamoja, halafu anaweza kupata mkopo. Bw. Zhu Yingdi alisema, benki ya ushirikiano vijijini kweli inaleta manufaa kwao. Alisema,

"Hakika manufaa ya mikopo ni makubwa. Kwa mfano, fedha za mikopo inayotolewa na shirika la fedha vijijini ni karibu Yuan milioni kadhaa kwa mwaka, kufanya hesabu kwa kufuata kiwango cha riba kilichowekwa, fedha zilizopungua za malipo ya riba ya wakulima wa kijiji chetu ni nyingi, ambazo ni kiasi cha Yuan elfu kumi kadhaa katika kijiji chetu, kweli imewanufaisha wakulima."

Kama tunavyojua, ingawa kazi ya benki ya Grameen iliyoanzishwa na Bw. Yunus katika vijiji nchini Bangladesh ni kuwasaidia watu maskini, lakini benki hiyo haikupata hasara. Sawa na benki hiyo, benki ya ushirikiano vijijini mjini Ruian inatoa mikopo midogo midogo kwa wakulima kupitia shirikisho la ushirikiano vijijini. Kwa njia hiyo wakulima wanapata fedha, benki pia inadhibiti hatari na kupata faida. Hatua hiyo kweli inatimiza kuzinufaisha pande zote mbili benki na wakulima.

Mkurugenzi wa ofisi ya shirikisho la ushirikiano vijijini mjini Ruian Bw. Lin Zhiyin alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

"Mikopo inayotolewa kwa kijiji cha Zhuaodi ni mingi. Kwa kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa wakulima kutokana na dhamana ya kikundi, hivyo matumizi na urudishaji wa fehda hizo unasimamiwa na shirika la fedha vijijini. Shirika hilo vijijini linaweza kutoa habari sahihi kuhusu lini wakulima watarudisha mikopo hiyo, hivyo inapunguza hatari ya usalama wa fedha."

Inafahamika kwamba shirika la fedha vijijini la Ruian ni idara ya kwanza ya kufanyiwa majaribio ya mageuzi ya fedha vijijini nchini China. Mageuzi hayo ya fedha yanakaribishwa na wakulima, na wataalamu wengi vilevile wana matarajio hukusu mageuzi hayo. Mtaalamu wa chuo kikuu cha umma cha China anayefanya utafiti kuhusu suala la vijiji Bw. Wen Tiejun alisema, kuanzisha shirikisho la ushirikiano vijijini kwenye ngazi ya miji na wilaya ni majaribio muhimu, na mji wa Ruian umepata mafanikio. Alisema shirikisho kama hilo linaweza kuenezwa kote nchini China katika wakati unaofaa.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-12