Mwezi Machi mwaka 1997, ili kutatua masuala kadhaa yaliyotokana na ujenzi wa mradi wa maji wa magenge matatu ya Mto Changjiang yakiwemo uhamiaji wa wakazi milioni moja katika sehemu ya magenge matatu na hifadhi ya mazingira ya viumbe, mji wa Chongqing uliamuliwa kuwa mji unaotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu ya China, na wilaya na miji ya sehemu ya magenge matatu ziliwekwa chini ya utawala wa mji wa Chongqing, mji wa Chongqing ukawa mji mkubwa wenye eneo la kilomita za mraba elfu 8 na idadi ya watu zaidi ya milioni 30. Serikali ya China imetenga fedha nyingi ili kuunga mkono maendeleo ya mji huo.
Mkurugeni wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya mji wa Chongqing Bw. Yang Qingyu alipoeleza hali ya maendeleo ya uchumi wa mji wa Chongqing katika miaka kumi iliyopita, alisema,
"Miaka kumi iliyopita tangu mji wa Chongqing kuamuliwa kuwa mji unaotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu ya China ilikuwa ni kipindi ambacho mji huo ulipata maendeleo ya haraka zaidi na wakazi walipata manufaa mengi zaidi katika historia ya mji huo."
Takwimu zinaweza kuonesha mafanikio makubwa ya mji wa Chongqing katika miaka kumi iliyopita. Katika kipindi hicho, wastani wa ongezeko la thamani ya uzalishaji wa mji huo kwa mwaka ulikuwa asilimia 10.2; katika mwaka 2006 wastani wa thamani ya uzalishaji kwa mtu ulikuwa zaidi ya dola za kimarekani 1500, ambao ulikuwa mara tatu ya mwaka 1996; wastani wa mapato ya wakazi wa mijini uliongezeka kuwa yuan elfu 11 kutoka yuan elfu 5, na wastani wa mapato ya wakulima uliongezeka kwa mara mbili. Bw. Zhou Yuan ambaye alizaliwa na kukuliaa mjini Chongqing ni mmoja wa watu walioshuhudia maendeleo ya haraka ya mji huo, alisema,
"Zamani mshahara wa yuan elfu 2 hadi elfu 3 ulichukuliwa kuwa ni mshahara mkubwa mjini Chongqing; lakini hivi sasa mshahara huo si mkubwa hata kidogo. Baada ya mji wa Chongqing kuamuliwa kuwa mji unaotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu, kuna fursa nyingi za biashara na ajira mjini humo. Kwa mfano katika kampuni yangu mshahara wa yuan elfu 7 na elfu 8 kwa mtu ni jambo la kawaida. Wafanyakazi wanazungumzia zaidi nyumba na magari badala ya chakula na nguo."
Jambo moja linaloweza kuonesha maendeleo ya uchumi na jamii ya mji wa Chongqing ni kuboreshwa kwa miundo mbinu. Naibu katibu wa kamati ya Chama cha Kikomunisiti cha China ya mtaa wa Dadukou mjini Chongqing Bw. Wu Daopan alipozungumzia mabadiliko ya mji wa Chongqing katika miaka kumi iliyopita alisema,
"Mabadiliko ni makubwa. Zamani miundo mbinu ilikuwa ni ya hali duni sana, katika miaka ya karibuni mji wa Chongqing ulitenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu. Zamani ulitenga yuan bilioni 20 hadi bilioni 30 kwa mwaka, hivi sasa unatenga yuan bilioni mia 2 hadi bilioni mia 3 kwa mwaka.
Kabla ya miaka kumi iliyopita, mtaa wa Dadukou ulikuwa ni mtaa wa wafanyakazi wa kampuni ya chuma na chuma cha pua ya Chongqing ambao eneo lake lilikuwa ni kilomita za mraba 7 tu, na ulikuwa na barabara moja tu. Lakini hivi sasa mtaa huo umekuwa mtaa wenye eneo la kilomita za mraba 103, hali ya mawasiliano imeboreshwa kutokana na ujenzi wa barabara kubwa, reli na daraja kubwa linalopita Mto Changjiang, na nyumba nzuri zinaonekana hapa na pale. Baada ya kampuni ya chuma na chuma cha pua ya Chongqing kuhamia sehemu nyingine, mtaa huo utakuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi.
Maendeleo ya mtaa wa Dadukou ni sehemu moja ya maendeleo ya mji wa Chongqing. Hali ya mji huo imekuwa nzuri zaidi kutokana na ujenzi wa barabara kubwa, reli, madaraja, uwanja wa ndege na bandari.
Mkazi wa mji huo Bw. Zhou Yuan aliisifu sana hali ya mawasiliano mjini humo, alisema,
"Baada ya mji wa Chongqing kuamuliwa kuwa mji unaotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu mwaka 1997, serikali imetenga fedha nyingi kwa ujenzi wa miundo mbinu, na kujenga reli mjini. Zamani kulikuwa na daraja la Mto Jialing na daraja la Mto Changjiang tu, hivi sasa madaraja na mahandaki mengi yamejengwa, ni rahisi kusafiri mjini."
Tukisema ujenzi wa mradi wa maji wa magenge matatu ya Mto Changjiang ni fursa kwa maendeleo ya mji wa Chongqing, na utawala wa moja kwa moja wa serikali kuu ya China umeupatia mji huo mazingira mazuri ya kupata maendeleo, basi utekelezaji wa sera ya kuendeleza sehemu za magharibi mwa China umesukuma mbele maendeleo ya haraka ya mji huo. Kuanzia mwaka 2000, China ilianza kutekeleza sera kadhaa zenye unafuu katika sehemu za magharibi ambazo uchumi wao ulikuwa nyuma kimaendeleo ili kusukuma mbele maendeleo ya sehemu hizo. Mji wa Chongqing ulioko magharibi mwa China unanufaika na sera hizo, na katika miaka 6 iliyopita wastani wa ongezeko la thamani ya uzalishaji ulikuwa asilimia 10.6
Mji wa Chongqing ukiwa ni mji mkubwa mwenye eneo zaidi ya kilomita za mraba elfu 80, unaipatia mitaa na wilaya zake zijitafute maendeleo yao kutokana na hali ya halisi. Mitaa na wilaya mbalimbali zilianzisha njia tofauti ya maendeleo kwa sifa zao za kipekee, na zinatafuta maendeleo kwenye sekta tofauti ili kuzuia ujenzi wa miradi usiwe sawasawa na kuwepo matumizi mabaya ya maliasili.
Mtaa wa Yuzhong wenye eneo la kilomita za mraba 18 ambao uko sehemu ya katikati ya mji wa Chongqing una wakazi wengi na maduka mengi. Mtaa huo ni sehemu ambayo sekta za biashara na huduma zinapata maendeleo makubwa zaidi mjini humo. Katibu wa kamati ya Chama cha Kikomunisti cha China ya mtaa huo Bw. Liu Xuepu alisema, eneo la biashara lenye kilomita za mraba 1.6 limeanzishwa mtaani humo, na limekuwa eneo kubwa zaidi la biashara katika sehemu ya magharibi mwa China, alisema,
"Eneo hili la biashara linaweza kukusanya wafanyabiashara, maliasili za uzalishaji na makao makuu ya makampuni, limekuwa njia moja ya makampuni ya nchini na nchi za nje kuwekeza vitega uchumi mjini Chongqing."
Mtaa wa Jiangbei unaendeleza uchukuzi wa bidhaa kwa hali nzuri ya safari za ndege na uchukuzi kwenye magati; mtaa wa Shapingba ambao vyuo vikuu vingi maarufu viko mtaani humo unafanya juhudi kujenga eneo kubwa la vyuo vikuu na eneo la makampuni ya teknolojia ya upashanaji habari; mtaa wa Hechuan ambao uko kando ya Mto Jialing na una maliasili nyingi za makaa ya mawe unafanya juhudi kuendeleza vituo vya uzalishaji wa umeme kwa nishati ya maji na makaa ya mawe; na mtaa wa Changshou unajenga eneo la viwanda vya kemikali vyenye teknolojia za kisasa.
Mwezi Machi mwaka huu, Rais Hu Jintao wa China alisema, "Ni lazima kuharakisha ujenzi wa mji wa Chongqing ili kuuhimiza mji huo uwe mji mwenye maendeleo makubwa zaidi kwenye sehemu za magharibi mwa China, uwe kituo cha uchumi kwenye sehemu ya juu ya Mto Changjiang, na maendeleo ya mji na vijiji yaendelee sambamba, na kuwa mji utakaotangulia kutimiza lengo la kujenga jamii yenye maisha bora katika sehemu za magharibi mwa China."
|